Hekalu la Tanzhe lililoko sehemu ya magharibi mwa Beijing lilijengwa kwenye mteremko wa mlima, ambao umezungukwa na vilele vingine 9 vikubwa. Hekalu hilo lilijengwa mwaka 307, kabla ya kujengwa mji wa Beijing. Msaidizi wa mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa hekalu la Tanzhe, Bw. Hao Xinjian alisema,
"Gavana wa sehemu ya kaskazini katika wakati ule aliitwa Wang Jun, mke wake Hua Fang alifariki dunia mwaka 307, na mwili wake ulizikwa katika sehemu ya Babaoshan, magharibi mwa Beijing. Ili aweze kuwaombea mkewe na watu wa nchi yake wabarikiwe na mungu, alijenga hekalu la Jiafu katika sehemu ya magharibi mwa Beijing, ambalo ndilo hekalu la Tanzhe la hivi sasa."
Tangu kujengwa hekalu la Tanzhe, jambo la kwanza walilofanya baadhi ya wafalme baada ya wao kuwa wafalme ni kwenda kuabudu budha katika hekalu la Tanzhe. Kutokana na kupendwa na wafalme wa enzi mbalimbali, hekalu la Tanzhe linachukua nafasi ya kwanza kati ya mahekalu mengi ya Beijing iwe ukubwa wa majengo au hadhi yake katika dini ya kibudha nchini China.
Umaalumu wa hekalu la Tanzhe ni majengo yake makubwa, ambayo eneo lake linafikia hekta 2.5. Majengo ya hekalu la Tanzhe yalijengwa kwenye mstari ulionyooka, ambayo majengo yaliyoko upande wa kushoto ni sawa kabisa na yale ya upande wa kulia, na kulingana na kanuni za elimu ya uzuri. Majengo ya hekalu la Tanzhe ni nadhifu, ya fahari na yenye mtindo wa majumba ya mfalme.
Sufuria kubwa ya shaba ni kitu wasichokosa kukiona watalii katika hekalu la Tanzhe, ambayo inasifiwa kuwa ni kitu cha maana sana katika hekalu hilo. Kupika uji katika sufuria hiyo, ambayo kipenyo wake ni mita 4, na yenye kimo cha mita 2, kunahitaji muda wa saa zaidi ya kumi. Wakati wa kusafisha sufuria hiyo, inawabidi watawa wapande ngazi na kuingia katika sufuria. Kwenye jiko lake kubwa yamechongwa maneno makubwa ya "Hekalu la Tanzhe". Haya, mbona maneno hayo ya "Hekalu la Tanzhe" yalichongwa kwenye jiko la hekalu? Msaidizi wa mkurugenzi wa ofisi ya usimamizi wa hekalu la Tanzhe Bw. Hao Xinjian alisema,
"Inasemekana kuwa mtawa kiongozi wa hekalu la Tanzhe aliogopa sana hekalu hilo kupatwa na maafa ya kuwaka moto, kwani majengo ya kale ya hekalu yalijengwa kwa miti, hivyo ni rahisi kupatwa na maafa ya moto. Siku moja aliota ndoto kuwa, ikiwa hekalu la Tanzhe litawekwa katika moto, basi hekalu hilo halitapatwa na maafa ya moto. Alipoamka kutoka katika usingizi, aliwaza sana, ghafla aling'amua kuwa, ikiwa wanachonga jina la hekalu la Tanzhe kwenye jiko, si sawasawa kuliweka hekalu katika moto kila siku? Hivyo hekalu hilo halitapatwa na maafa ya moto tena. Ndivyo hivyo, walivyochonga jina la hekalu hilo kwenye jiko."
Licha ya sufuria kubwa ya shaba, kitu kingine cha maana sana katika hekalu la Tanzhe ni "samaki wa jiwe". Samaki wa jiwe wa rangi ya kijani nzito, ana urefu wa mita 1.7 na uzito wa kilo 150. Mwongozaji wa safari ya matembezi dada Li Lu alisema,wakazi wa huko wana imani kuwa samaki huyu wa jiwe ana uwezo wa kuponya wagonjwa.
"Ilisemekana kuwa samaki huyo ni azizi ya mfalme dragon wa bahari ya kusini, siku moja mfalme dragon alimpa mungu wa mbinguni zawadi ya samaki yule. Hapo baadaye mungu alilipa hekalu la Tanzhe zawadi ya samaki huyo ili kuondoa taabu za watu wa duniani. Samaki huyo ana uwezo wa kuponya wagonjwa na kuepusha watu na maafa. Wakati ule watu walisadiki sana, walipoumwa kichwa walipenda kupapasa kichwa cha samaki, na walipoumwa tumbo walipenda kupapasa tumbo la samaki wakiamini watapona."
Ukweli ni kuwa, samaki huyu alichongwa na mafundi kwa kutumia kimondo kilichoanguka chini chenye madini ya shaba na madini mengine adimu. Samaki huyo anatoa sauti tofauti akigongwa katika sehemu zake mbalimbali, sauti yake ni nzuri kama ya kutolewa na ala za muziki. Baada ya miaka mingi kupita, "samaki wa jiwe" huyo akawa kama jini mwenye uwezo mkubwa nyoyoni mwa watu.
Kitu kingine cha kuvutia watu katika hekalu la Tanzhe ni miti ya kale inayojulikana kwa three-bristle cudrania, ambayo katika lugha ya Kichina miti hiyo inaitwa kuwa miti ya Zhe. Miti ya Zhe ni mizuri, ambayo majani yake ni chakula kizuri kwa funza wa hariri, miti yake inaweza kutumiwa kutengeneza samani za hali ya juu. Kutokana na kuwepo kwa "Longtan" yaani dimbwi la maji lenye sanamu ya mawe ya dragon nyuma ya hekalu hilo, na kuwepo miti ya Zhe yaani three-bristle cudrania katika mlima wa huko, hivyo hekalu hilo lilianza kuitwa kuwa hekalu la Tanzhe. Ndani ya hekalu la Tanzhe kuna miti mikubwa sana ya kale, hususan mti mmoja unaojulikana kwa "mti mfalme", ambao ni gingko tree iliyoanza kuota kabla ya miaka zaidi ya elfu moja iliyopita. Mti huo una urefu wa zaidi ya mita 40, mti huo ni mkubwa sana, kiasi cha watu 7 au 8 wakishikana mikono wanaweza kuuzungushia. Katika majira ya joto, kivuli cha mti huo wa kale kinaweza kufunika eneo la mita za mraba 600 hivi. Katika majira ya kupukutika majani, majani yote ya mti yanabadilika kuwa ya rangi ya dhahabu yakionekana kama vipepeo wa rangi ya manjano wanaorukaruka. Habari zinasema kuwa, hapo zamani, kila mfalme mpya aliporithi ufalme, huchipuka kijiti kutoka kwenye mizizi ya mti, na kila mfalme alipofariki dunia, huwepo tawi la mti lililokatika, hivyo watu waliuita mti huo kuwa "mti mfalme".
Mbali na "mti mfalme", katika hekalu la Tanzhe imeota miti miwili ya magnolia conspicus. Ingawa katika mji wa Beijing kuna miti mingi ya magnolia conspicus, lakini miti hiyo miwili iliyoota katika hekalu hilo ni ya miaka zaidi ya 400 iliyopita. Kila mwaka katika majira ya Spring, maua ya miti hiyo yanapochanua, watu wengi sana wanakwenda huko kuyaangalia. Bibi Wang Lin, ambaye ni mkazi wa Beijing anayependa sana maua ya miti ya magnolia conspicus alisema,
"Mimi ninakaa mjini Beijing, nilisikia kuwa maua ya magnolia conspicus yamechanua, hivyo leo nimekuja mahususi kuangalia maua. Yamechanua maua mengi, na mimi ninafurahi sana."
Idhaa ya kiswahili 2007-06-25
|