Tarehe mosi Julai mwaka huu, Wachina wataadhimisha miaka 10 tangu China irudishe mamlaka yake Hong Kong. Katika miaka hiyo 10 iliyopita, idadi ya wakazi wa Hong Kong waliopata ajira hapa China Bara imekuwa inazidi kuongezeka. Leo katika kipindi hiki cha Tazama China, tunazungumzia Wahongkong wanaofanya kazi hapa mjini Beijing. Karibuni.
Bibi Pan Huixin ni mtumishi wa idara ya maendeleo ya biashara ya Hong Kong. Mwanzoni mwa mwaka 2006 alitumwa kufanya kazi kwenye ofisi ya idara hiyo hapa Beijing. Anasema "Hii ni mara ya kwanza kwangu kuondoka Hong Kong na kuishi katika mji mwingine kwa muda mrefu. Nimeshuhudia majira manne hapa Beijing, ambapo hali ya hewa ni tofauti na ile ya Hong Kong. Ilinichukua muda kuzoea hali hii. Nimevutiwa na tofauti hizo."
Pamoja na tofauti ya hali ya hewa, Bibi Pan pia alieleza tofauti nyingine kati ya Beijing na Hong Kong akisema, Beijing ni mji mkubwa zaidi kuliko Hong Kong.
Anasema "Nakumbuka mwanzoni nilipofika Beijing, niliuliza njia za kufika kwenye uwanja wa mashariki, nikaambiwa kuwa si mbali, tembea mpaka njia panda inayofuata. Kule Hong Kong, kati ya njia panda mbili si mbali, kwa kutembea inachukua muda wa dadika 3 hadi 5, inatosha. Lakini hapa Beijing, ilinichukua muda wa dakika 20 kutembea mpaka njia panda inayofuata. Jambo hilo lilinifanya nifahamu kwamba, Beijing ni mji mkubwa sana."
Kuhusu tofauti nyingine kati ya Beijing na Hong Kong, Bibi Pan alieleza kuwa, huko Hong Kong watu wanaishi kwa kuwa na pilikapilika nyingi zaidi, watu wanafanya kazi kwa muda mrefu na ni jambo la kawaida kuendelea kufanya kazi hata katika siku za mapumziko. Lakini hapa mjini Beijing, pamoja na kuwa watu wanachapaji kazi, lakini watu wana muda mrefu pia wa kufanya shughuli zao binafsi baada ya kazi.
Anasema "Kusema kweli Beijing ni mji wa utamaduni, kuna mambo mengi ambayo ningependa kuyaona. Kwa hiyo katika wikiendi, napenda kutembelea sehemu mbalimbali na kuona mambo mbalimbali ya aina tofauti za utamaduni. Naona nina muda mwingi zaidi binafsi, ambapo naweza kuburudishwa na mambo ya kiutamaduni ambayo niliyapuuza nilipokuwa huko Hong Kong."
Bibi Pan pia alieleza jambo moja la kuwachekesha watu lililomkumba mwanzoni alipofika Beijing. Anasema "Kabla kufika Beijing, nilikuwa sina ufahamu wa kutosha kuhusu mji huu. Wakati huo nilidhani kuwa China Bara ilikuwa nyuma sana kimaendeleo, kwa hiyo nilinunua mahitaji mengi ya kila siku huko Hong Kong na kuyasafirisha hadi Beijing. Lakini baada ya kufika Beijing, nikagundua kuwa bidhaa zinazouzwa Hong Kong pia zinapatikana hapa Beijing. Na ni rahisi zaidi kuzinunua."
Gao Qibin ni kijana kutoka Hong Kong anayesoma kwenye chuo kikuu cha Beijing. Alipozungumzia sababu yake ya kuamua kusoma katika chuo kikuu hapa Beijing, kijana huyo alisema dunia nzima inavutiwa na nguvu kubwa ya kujiendeleza ya China, aliona kuwa kama akiweza kuja mapema na kupata ufahamu kuhusu China Bara, hakika itamsaidia kwenye masomo yake ya kibiashara.
Anasema "Kusoma hapa Beijing kunaninufaisha kwa pande mbili, mimi ni mwanafunzi niliyezaliwa na kukua huko Hong Kong, na sasa napata uzoefu wa kusoma China Bara. Naona hali hii itanipa fursa nyingi zaidi za kujiendeleza."
Mbali na masomo kijana Gao Qibin anapenda kushiriki kwenye shughuli mbalimbali za wanafunzi, hivi sasa yeye ni mkurugenzi wa jumuiya ya utamaduni wa Hong Kong katika chuo kikuu cha Beijing. Mbali na wanafunzi kutoka Hong Kong, jumuiya hiyo pia inawashirikisha wanafunzi kutoka China Bara. Kijana huyo alisema kutokana na shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, sasa anaweza kuwasiliana na wanafunzi kutoka sehemu mbalimbali za China Bara. Alisema kama angesoma chuo kikuu huko Hong Kong, asingeweza kupata fursa ya kupata marafiki wengi kutoka sehemu tofauti.
Kijana huyo atahitimu chuo kikuu mwakani, alisema anataka kupata ajira hapa China Bara.
Hivi sasa wafanyabiashara wengi kutoka Hong Kong wanawekeza China Bara. Bw. Zeng Zhiming ambaye ni mkurugenzi mkuu wa kampuni ya goldline ni mmojawapo wa wafanyabiashara hao. Kampuni hiyo ya kutengeneza nguo na tai ilianza kuingia kwenye soko la China Bara miaka ya 1980.
Bw. Zeng anasema "Kutokana na utekelezaji wa sera ya maguezi na kufungua mlango nchini China, kasi kubwa ya maendeleo ya taifa letu ni ya ajabu kweli, ikilinganishwa na ile ya nchi na sehemu nyingine duniani."
Bidhaa za kampuni ya goldline zinajulikana China Bara, hasa mavazi ya wanaume ya kampuni hiyo ni ya hali ya juu. Bw. Zeng alieleza kuwa, China Bara ina hali ya utulivu na sera nafuu zinazovutia uwekezaji wa wafanyabiashara kutoka Hong Kong, yeye na wenzake kutoka Hong Kong wana imani kubwa ya kuendeleza zaidi shughuli zao za kibiashara hapa China Bara.
Anasema "Sisi wafanyabiashara tunazingatia mambo matatu tu kabla ya kuamua kuwekeza katika sehemu fulani, yaani utulivu wa kisiasa, hali ya usalama na kiwango cha kodi. Kusema kweli mazingira ya uwekezaji ya China Bara yanaboreshwa siku hadi siku."
Katika miaka 10 iliyopita tangu Hong Kong irudi China, watu wengi zaidi kutoka Hong Kong wamekuwa wanakuja China Bara, kufanya kazi au kuishi. Kutokana na utulivu wa kisiasa na kiuchumi huko Hong Kong, watu hao hawana wasiwasi wa kuondoka nyumbani na kupata nafasi za kujiendeleza, wakati China Bara inawaandalia nafasi kubwa za kupata maendeleo.
Idhaa ya kiswahili 2007-06-28
|