China ina idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.3, na miongoni mwake milioni 300 ni watoto. Nchini China vijana na watoto siku zote wanafuatiliwa sana na jamii, si kama tu imetungwa sheria ya kuwalinda watoto, bali pia kuna mashirika maalum yanayowahudumia watoto. Mfuko wa Soong Ching Ling wa China unalenga kushughulikia maendeleo ya watoto.
Marehemu Bi. Soong Ching Ling alikuwa mwenyekiti wa heshima wa taifa la China alipoaga dunia mwaka 1981, alikuwa ametoa mchango mkubwa katika harakati za ukombozi wa taifa la China na maisha mazuri ya wananchi. Alipokuwa hai alisifu shughuli za watoto ni shughuli za kujenga siku nzuri za mbele.
Mkurugenzi mkuu wa mfuko wa Soong Ching Ling Bwana Li Ning alisema, katika miaka 25 iliyopita tangu mfuko huo uanzishwe, umerithi matakwa ya Bi. Soong Ching Ling. Akisema:
"Mfuko wetu umefanya shughuli nyingi katika kuinua sifa ya watoto na kuwaelimisha wawe na maadili, kwa mfano umeanzisha tuzo ya uvumbuzi na tuzo ya fasihi ya watoto. Katika sehemu zilizo nyuma kimaendeleo mfuko wetu umewasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi wajiendeleza na kuwasaidia watoto wa familia zenye matatizo ya kiuchumi kwenda shule, kuboresha miundo mbinu ya shule, kutoa huduma za matibabu kwa wanawake na watoto."
Tuzo ya uvumbuzi wa watoto ya Soong Ching Ling ni moja ya tuzo nyingi zilizowekwa kwenye mfuko huo, mpaka sasa vijana na watoto laki moja hivi wameshiriki kwenye shughuli za kufanya uvumbuzi,na watoto zaidi ya elfu moja wamepewa tuzo hiyo. Naibu mkurugenzi wa kamati ya maandalizi ya tuzo hiyo Bwana Lu Shan alisema:
"Kuweka tuzo ya uvumbuzi kunalenga kuhamasisha watoto wawe na moyo wa kufanya uvumbuzi na kuongeza uwezo wa kusanifu na kutengeneza vitu. Maendeleo ya nchi yanategemea sayansi na teknolojia, kukuza sayansi na teknolojia kunategemea watu wenye ujuzi, na watu wenye ujuzi wanatakiwa kuandaliwa tangu utotoni."
Mfuko wa Soong Ching Ling wa China pia unafuatilia sana maendeleo ya watoto waishio kwenye sehemu zilizo nyuma kimaendeleo na vijijini. Kwa mfano mfuko huo umeanzisha mpango wa afya kwa wanawake na watoto wachanga wa sehemu ya magharibi, kuwapa kinamama na watoto waishio katika vijiji vya pembezoni matibabu na dawa bila malipo. Kuanzisha mpango wa kutoa mafunzo kwa walimu wa sehemu ya magharibi, ili kuboresha sifa ya walimu wa shule za msingi wa sehemu za vijijini zilizo nyuma kimaendeleo.
Katika jumba la maonesho ya sayansi na teknolojia la watoto la Soong Ching Ling mjini Beijing, kilianzishwa kituo cha kueneza ujuzi wa sayansi cha kuwahudumia watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini ili kuwafahamisha watoto hao ujuzi mwingi zaidi za sayansi. Katika siku ya watoto duniani ya tarehe 1 Juni ya mwaka huu, yalifanywa mashindano ya kutengeneza magari ya mfano yanayotumia nishati ya jua, mashindano hayo yaliwashirikisha tu watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mjini Beijing.
Katibu mkuu wa mfuko huo Bw. Li Ning alisema, siku zijazo mfuko huo utaweka mkazo zaidi katika kuwashughulikia watoto waishio vijijini na sehemu zilizo nyuma kimaendeleo. Alisema:
"Katika sehemu ya vijijini, kuna watoto wengi ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini, watoto wa aina hiyo hasa waishio katika sehemu zilizo nyuma kimaendeleo wanakumbwa na ukosefu wa nguo na dawa, hivyo katika siku zijazo tunapaswa kuzingatia zaidi namna ya kutatua matatizo ya watoto hao."
|