Kati ya sehemu maarufu za utalii za nchini China, pengine umewahi kusikia "Magenge Matatu" ya mto Changjiang na "Sanamu yenye Miguu Mikubwa", ambazo ziko katika mji wa Chongqing. Mji wa Chongqing, ambao ulifanywa kuwa mji unaosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu miaka michache iliyopita, unavutia idadi kubwa ya watalii kutokana na sehemu zake nyingi zenye mandhari nzuri ya kimaumbile pamoja na utamaduni wa jadi.
Matembezi kwenye Magenge Matatu ni ya kuvutia watalii zaidi katika utalii wa mji wa Chongqing. Magenge Matatu yako kwenye bonde kubwa lenye mandhari nzuri ya milima na mto, na ni sehemu yenye mandhari nzuri zaidi kwenye mtiririko wa mto Changjiang wenye urefu wa kilomita zaidi ya 6,300, ambao ni mto mrefu kabisa nchini China. Magenge Matatu ambayo yana urefu wa kilomita 90 yananzia Baidicheng, wilaya ya Fengjie ya mji wa Chongqing kwa upande wa magharibi, na yanaishia Nanjinguan mjini Yichang, mkoani Hubei.
Bonde la magenge Matatu ya mto Changjiang linachukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa duniani, ambalo watalii wanaweza kuangalia mandhari ya magenge na bonde, pamoja na vitu vya utamaduni katika meli ya utalii, tena wanaweza kushuka kutoka kwenye meli na kufanya matembezi katika kando mbili za mto. Mtalii kutoka mkoa wa Shandong, Bw. Li alipanda meli na kuangalia mandhari ya Magenge Matatu. Alisema,
"Mimi nilipanda meli kwenye lango la Chaotianmen la mji wa Chongqing, mimi ninafurahi sana kuona meli ikienda taratibu kwenye sehemu ya chini ya mtiririko wa mto, niliweza kuangalia milima mirefu, mabonde na vijiji nikiwa kwenye sehemu ya juu ya meli, ninaweza kuona mandhari nzuri kutoka pande zote."
Utalii kwenye Magenge Matatu ni moja kati ya njia tatu za dhahabu za utalii zinazopendekezwa na idara ya utalii ya China kwa watalii. Pamoja na ujenzi wa mradi wa maji wa Magenge Matatu na kuanza kulimbikiza maji kwenye Magenge Matatu, mandhari mpya nzuri imeonekana kwenye Magenge Matatu, watalii wanaweza kuangalia Magenge Matatu madogo yaliyoko kwenye mto Daning, ambao ni tawi la mto Changjiang, huko pia kuna mandhari nzuri pamoja hadithi nzuri kuhusu mandhari mbalimbali.
Mbali na kutembelea Magenge Matatu, watalii waliofika Chongqing, wanakwenda kuangalia sanamu za mawe zenye miguu mikubwa. Sanamu hizo zilichongwa miaka zaidi ya 1,000 iliyopita, sanamu nyingi ni za dini ya kibudha, na baadhi yake ni za dini ya kidao na za msomi Confucius, sanamu hizo zinawakilisha sanaa ya sanamu zilizochongwa kwenye mapango ya mlima. Mwaka 1999, kundi la sanamu za mawe zenye miguu mikubwa liliorodheshwa na shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa kuwa mabaki ya urithi wa utamaduni wa dunia.
Sanamu za miguu mikubwa ziko katika wilaya ya Dazu ya mji wa Chongqing, sanamu za mawe zilizoko kwenye mlima wa Baoding na mlima wa kaskazini zimehifadhiwa vizuri zaidi na ni maarufu zaidi. Sanamu za mawe karibu elfu kumi zilizoko kwenye mlima wa Baoding, zilichongwa kwenye milima ya mawe iliyoungana kwa umbo la herufi ya U, sanamu nyingi zilizopangwa zinaonesha ukubwa wa kimaumbile kwa watu. Mfanyakazi wa jumba la makumbusho ya sanaa ya sanamu zenye miguu mikubwa, bi Yang Qin alisema,
"Sehemu hiyo ilianza kujulikana katika enzi ya Song ya kusini mwaka 1174?1252, mtawa aliyekomaa kwa dini ya kibudha Zhao Zhifeng akiwa na nia ya kuendeleza dini ya kibudha, alichonga sanamu za mawe kwa zaidi ya miaka 70 toka alipokuwa na umri wa miaka 19."
Ili kuelimisha watu, sanamu hizo zinafanana na watu wa kawaida, ambazo baadhi yake zinawaelimisha watu kuwaheshimu na kuwatunza vizuri wazazi wao, na baadhi ya nyingine zinaeleza hali ya kuwa na uhai kwa mara nyingine. Ikilinganishwa na sanamu kubwa za mawe za mlima wa Baoding, sanamu za mawe za Buddha karibu elfu kumi zilizoko kwenye mlima wa kaskazini, zilichongwa vizuri zaidi. Bibi Hilde Andresen kutoka Ujerumani baada ya kuangalia sanamu hizo alisema,
"Hizo ni sanamu ninazozipenda zaidi kati ya sanamu nilizoziona hadi hivi sasa. Naona nimebahatika kuziona sanamu hizo na kufahamu historia yake."
Mji wa Chongqing pia ni wa kupendeza sana mbali na Magenge Matatu ya mto Changjiang na sanamu za mawe zenye miguu mikubwa. Chongqing ni mji maarufu wa utalii nchini China, sehemu ya kati ya mji wa Chongqing, ambayo imejengwa kwenye mteremko wa mlima, inazungukwa na mto Changjiang na mto Jialing, hivyo mji huo pia unajulikana kama mji wenye mlima na mji wenye mito. Mji huo unaonekana unapendeza zaidi wakati wa usiku, ambapo taa za nyumba za wakazi na nyota za angani zinaungana pamoja.
Mandhari nzuri, chemchemi safi na chakula kitamu, vitu hivyo vitatu vimeongeza sifa za mji wa Chongqing. Mji wa Chongqing ni mji wenye raslimali nyingi ya chemchemi duniani, ambayo iliendelezwa tangu zamani za kale. Chemchemi ya maji moto ya Kaskazini ilijulikana na kutumika toka zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, ambayo ni chemchemi ya maji moto iliyoanza kutumika mapema zaidi hapa duniani, hadi hivi sasa chemchemi hiyo ya maji moto bado inatumika, hivyo inajulikana kama ni chemchemi kuu ya nchini China. ili kuinua kiwango cha chemchemi za maji ya moto, mji wa Chongqing umeanzisha ujenzi na kuboresha chemchemi tano za maji moto ikiwemo chemchemi ya maji moto ya kaskazini ukiwa na lengo la kufanya mji wa Chongqing uwe mji mkuu wa chemchemi za maji moto duniani.
Wakazi wa Chongqing wanapenda sana kula chakula cha "Huoguo". Wakazi wa Chongqing wanapenda sana kula pilipili hoho ya rangi nyekundu, katika sufuria ya "Huoguo" kuna mafuta ya rangi nyekundu yenye pilipili hoho yanayoelea juu ya maji ya supu, chakula kinachoweza kutiwa ndani ya sufuria yenye maji ya supu iliyochemka ni cha aina mia kadhaa, chakula kikuu ni nyama, ambayo ni pamoja na utumbo wa ng'ombe au samaki wa aina za eel na hairtail, pamoja na mboga na uyoga. Ukitembea kwenye barabara za mji wa Chongqing, unaweza kusikia harufu ya pilipili. Kwani mjini Chongqing kuna migahawa mingi sana ya chakula cha "Huoguo", wakazi wa mji huo karibu kila siku wanakula chakula hicho. Inasemekana wakazi wa huko wanapenda sana kula pilipili kutokana na hewa ya unyevunyevu, pilipili inafanya kazi ya kuondoa madhara ya unyevunyevu. Watu wanaotoka kwenye sehemu nyingine huenda hawapendi kula pilipili, hiyo si kitu, migahawa ya "Huoguo" ya Chongqing ina uzoefu mkubwa, na ni ya hakika kuwa itaandaa chakula na kukuridhisha.
Katika miaka ya hivi karibuni utalii wa mji wa Chongqing umepata maendeleo ya kasi, idadi ya watalii na pato kutokana na utalii vinaongezeka kwa mfululizo. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya mji wa Chongqing, Bw. Wang Aizu alisema, idadi ya watalii waliotembelea Chongqing ilifikia milioni 68, na mwaka jana pato la sekta ya utalii lilifikia Yuan bilioni 36.4.
Idhaa ya kiswahili 2007-07-02
|