Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-05 16:33:53    
Mwandishi wa habari aliyejikita kwenye uhifadhi wa mazingira

cri

Bw. Huang Chengde ni mwandishi wa habari na mpiga picha mzoefu wa gazeti la Guiyangribao, mkoani Guizhou, kusini magharibi mwa China. Mpaka sasa amefanya kazi kwenye gazeti hilo kwa miaka 25. Katika miaka 10 iliyopita, mara kwa mara alikuwa anatembelea sehemu ya magharibi ya China. Kwa kutumia kalamu na kamera, alifichua vitendo vilivyokuwa vinasababisha uharibifu wa mazingira, na kuhamasisha jamii izingatie umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Bw. Huang Chengde mwenye umri wa miaka 53 anaonekana ni kijana zaidi kuliko umri wake, ni mwembamba na mwenye kimo cha wastani.

Tokea miaka ya 80 ya karne iliyopita, matukio ya kuharibu mazingira yalianza kutokea kwenye sehemu ya magharibi ya China kwenye mchakato wa kuendeleza uchumi, matukio hayo yalifuatiliwa na Bw. Huang. Ili kufahamu hali halisi kuhusu matukio hayo, aliamua kwenda kwenye sehemu hizo kufanya ukaguzi.

Bw. Huang Chengde alisema, "Sehemu ya magharibi inaweza kupata maendeleo ya kasi ya uchumi au la, suala muhimu la kwanza ni suala la uhifadhi wa mazingira ya viumbe. Nafanya kazi ya uandishi wa habari kwa kufuata kanuni ninazofuata katika maisha yangu, nazo ni kwamba ninapaswa kubeba wajibu kwa jamii. Nina kauli mbiu rahisi, yaani nafanya kila niwezalo kwa ajili ya sayari ya dunia ambayo ni maskani yetu. Natumai kutoa mchango wangu kutokana na kazi yangu ya uandishi wa habari."

Mwaka 1997 Bw. Huang Chengde akiendesha motokaa alianza safari yake ya kwanza kwenda sehemu ya magharibi ya China, ambapo alichukua kamera na nguo chache tu.

Sehemu ya magharibi ya China ina theluthi moja ya idadi ya watu wa China, lakini eneo la sehemu hiyo linachukua asilimia 70 ya ardhi ya China. Kutokana na sababu za kimaumbile na kihistoria, sehemu hiyo iko nyuma kimaendeleo ikilinganishwa na sehemu ya mashariki ya China.

Bw. Huang alisema hakujali uchovu na upweke uliomkabili kwenye safari hiyo, lakini aliona huzuni aliposhuhudia misitu iliyokatwa kabisa, mito iliyokauka, na jinsi jangwa lilivyofunika makazi ya wafugaji.

Mwandishi huyo wa habari aliandika kumbukumbu na kupiga picha za hali yote aliyoona. Alisema kitu kilichomhuzunisha zaidi ni kwamba, watu wa baadhi ya sehemu hawakuwa na ufahamu wowote kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

Alisema "Baadhi ya watu hawakufahamu uhifadhi wa mazingira ni kitu gani. Ukiuliza kuhusu hali mbaya ya uchafuzi kwenye sehemu fulani, viongozi wa huko wanalalamika wakisema, wanajitahidi kuendeleza uchumi kwa nini wanakosolewa sana namna hii? Wakazi wa huko pia hawafurahii, wakiulizwa wanasema nimefyeka miti ili iwe mashamba kwa sababu hatuna chakula, kwa nini mnataka kukwamisha mbinu zetu za kujipatia chakula? Mambo kama hayo yalikuwa mengi, pia nilikumbwa na vizuizi kutoka pande mbalimbali, hali ambayo ilinibidi niwatolee ufafanuzi mmoja baada mwingine."

Baadaye Bw. Huang Chengde alikuwa anakwenda kwenye sehemu ya magharibi ya China kufanya ukaguzi kwa mara nyingine tano. Hadi hivi sasa amemaliza safari yenye urefu wa kilomita zaidi ya laki mbili, amepita kwenye mikoa 12 iliyoko magharibi mwa China.

Katika safari hizo, mbali na gazeti analofanyia kazi, magazeti mengine ya China pia yalichapisha makala zake kuhusu hali ya uhifadhi wa mazingira. Katika miaka mitano iliyopita, magazeti zaidi ya 30 ya China yalichapisha makala zake zenye jumla ya maneno laki 2 na picha zaidi ya 300 alizopiga. Vituo vya televisheni na radio vilimwalika atengeneze filamu zinazohusu uhifadhi wa mazingira na awe mwongozaji wa kipindi cha radio cha uhifadhi wa mazingira.

Makala za Bw. Huang Chengde ziliwafahamisha watu jinsi hali halisi ya mazingira ilivyo kwenye sehemu ya magharibi ya China. Makala hizo ziliwavutia watu wengi na idara za serikali. Mwaka 2000 kwenye mkutano mmoja uliohudhuriwa na viongozi wa mikoa 12 ya sehemu ya magharibi ya China, zilioneshwa picha alizopiga, na picha hizo ziliwavutia sana maofisa hao. Miaka miwili baada ya hapo, mwandishi huyo wa habari alialikwa na baraza la serikali ya China kuhudhuria kwenye mkutano mmoja, na alitoa hotuba kuhusu uhifadhi wa mazingira kwa msingi wa habari alizokusanya kwenye ziara zake za ukaguzi katika sehemu ya magharibi ya China.

Bw. Huang Chengde alieleza kuwa jitihada alizofanya siyo za bure, kwani alipotembelea sehemu hiyo katika miaka ya hivi karibuni, aliona watu wameimarisha mwamko kuhusu uhifadhi wa mazingira, na serikali za sehemu hiyo pia zimeongeza kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya mazingira. Alisema  "Hivi sasa hali imeboreshwa sana. Sasa hakuwepo matukio ya kufyeka ovyo miti na kulifanya eneo la misitu liwe mashamba kama ilivyokuwa miaka ya awali. Serikali inatekeleza hatua za mfululizo za kupiga marufuku ufyekaji miti, na mazingira ya viumbe yanaboreshwa hatua kwa hatua."

Mwandishi huyo wa habari pia anashirikiana na wenzake kuhimiza uhifadhi wa mazingira kwenye maskani yake, mjini Guiyang. Kutokana na pendekezo lao, maji ya mto yaliyowahi kutoa harufu mbaya kutokana na uchafuzi hivi sasa umeshughulikiwa kuwa safi. Vitendo vyake vinasifiwa sana na jamii. Bosi wake ambaye ni mhariri mkuu wa gazeti la Guiyangribao Bw. Sun Fengqi alimsifu sana Bw. Huang Chengde, akisema "Yeye ni mtu mwenye moyo wa dhati na ushujaa, ana mawazo mengi mapya. Shughuli zake za kukusanya habari zinaungwa mkono na watu wa hali mbalimbali kwenye jamii. Makala zake na picha alizopiga sasa ni data muhimu kuhusu mambo ya uhifadhi wa mazingira katika sehemu ya magharibi ya China. Na kutokana na vitendo vyake, tunaona wajibu wa waandishi wa habari kwa jamii."

Idhaa ya kiswahili 2007-07-05