Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-09 14:59:30    
Li Yuchun mwanafunzi wa kike aliyejulikana ghafla na kuwa maarufu

cri

Mwaka 2005 kipindi cha "mashindano ya kuchagua wanafunzi hodari wa kike" kilichotangazwa na kituo cha televisheni cha Mkoa wa Hunan kiliwavutia watu wengi nchini China, na mwanachuo Li Yuchun aliyeshinda kwenye mashindano hayo akapendwa na vijana wengi wa kike na wa kiume nchini China.

Miaka miwili iliyopita, Li Yuchun mwenye umri wa miaka 23, alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Muziki cha Mkoa wa Sichuan. Tokea mwezi Julai hadi Septemba mwaka 2005, alipita kwenye mashindano ya kwanza na ya pili, na mwishowe akiwa pamoja na wengine 10 alishiriki kwenye fainali. Mashindano hayo yote matatu yalitangazwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha mkoa wa Hunan. Mashindano yalikuwa magumu na ya kuvutia sana. Mpaka sasa Li Yuchun bado anakumbuka wazi hali ilivyokuwa kwenye mashindano. Alisema,

"Niliposhiriki kwenye fainali sikujali sana matokeo yangu kama ilivyokuwa kwenye mashindano ya kwanza, ambapo nilitamani sana kupata ushindi, kwani nilikuwa hoi sana, kwa hiyo nilipopata nafasi ya kwanza sikuwa na furaha kubwa bali nilishukuru kumalizika kwa mashindano."

Li Yuchun alizaliwa katika mji wa Chengdu, mkoani Sichuan. Alipokuwa mtoto alikuwa kama watoto wengine, alijifunza kuchora, kuandika insha na kucheza dansi, lakini hakufundishwa kuimba. Lakini Li Yuchun alikuwa na kipaji cha kuimba. Alipokuwa katika shule ya sekondari alikuwa nyota wa kuimba baada ya kushiriki mashindano ya kuimba shuleni, na alifanya maonesho yake ya kuimba alipohitimu masomo yake. Alisema,

"Nilikuwa sawa na wanafunzi wengine, nilikuwa sijulikani katika shule yangu, siku moja nilishiriki kwenye mashindano ya kuimba, mara moja nikaanza kujulikana. Nilipohitimu masomo nilifanya maonesho na niliimba nyimbo zaidi ya 20."

Baada ya kuwa mashuhuri, kila siku Li Yuchun ana pilika nyingi, alisaini mkataba wa kutoa albamu tano na kampuni moja ya muziki katika muda wa miaka mitano. Maisha yake yamejaa shughuli za kibiashara, kwamba licha ya kufanya matangazo ya biashara kwa sura yake kwa ajili ya bidhaa za kompyuta, simu za mkononi, saa za mkononi, pia anashiriki kwenye uigizaji wa filamu. Li Yuchun hawezi tena kurudi kwenye maisha yake ya zamani alipokuwa mtoto wa kawaida, shughuli nyingi na kusafiri mara kwa mara zinamfanya asikie mchovu sana. Shughuli hizo zilimpokosesha furaha, alisema,

"Mwanzoni sikuzoea sana shughuli nyingi kama hizi, nilitamani kuishi tena maisha kama ya utotoni, lakini hali ilivyo ni tofauti kabisa, ninaona usumbufu rohoni, Nilifikiri, kama nisingeshiriki kwenye mashindano ya kuchagua wanafunzi hodari sasa ningekuwa huru kabisa, ningeweza kukaa na kuongea na marafiki zangu, lakini sasa siwezi. Mara nyingi nilipokuwa safarini marafiki zangu walinipigia simu wakisema, 'sote tuko pamoja, ila wewe tu haupo,' niliposikia maneno hayo nilisikia uchungu."

Li Yuchun hakutegemea kama angekuwa nyota kutoka mwanachuo wa kawaida, lakini hayo ni kweli na amepata mafanikio. Albamu yake ya kwanza kwa jina la "Mke wa Mfalme na Ndoto Yake" iliuzwa nakala laki 4.3 katika muda wa mwezi mmoja tu. Jarida la Marekani "Times", chapa ya Asia, liliwachagua mashujaa wa Asia wa mwaka 2005, yeye alikuwa mmoja wa mashuja sita wa China. Hata hivyo, yeye anaendelea kuwa kama zamani. Yeye ni msichana mrefu na mwembamba, ana nywele fupi na mwenye sauti nene. Ana mashabiki wake wengi, anapoimba jukwaani mashabiki wake wanamshangilia kwa kusema "Li Yuchun, tunakupenda!" Naye akawajibu "Niwapenda vile vile!" Upendo wa mashabiki zake unamtia sana wasiwasi, alisema,

"Kila nilipoona jinsi mashabiki zangu wanavyonipenda huwa nasikia uchungu, hasa ninapofanya maonesho ya mzunguko katika sehemu mbalimbali mashabiki wanasubiri maonesho yamalizike ili wanione kwa karibu, lakini gari mara linaondoka, nao wanakimbilia gari ili wanione zaidi, wakati huo ninasikia sana uchungu kwa sababu ninachoweza kufanya ni kuwaona tu wakikimbia nyuma ya gari yangu."

Li Yuchun ni mkimya na mwenye haya, lakini anapokuwa jukwaani anaonekana mchangamfu, sauti yake inavutia kama sumaku na dansi zake zinawafanya mashabiki wake wawe na furaha tele. Sasa tuburudike na wimbo wake uitwao "Love will keep us alive".

Idhaa ya kiswahili 2007-07-09