Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-18 11:11:28    
Bi. Zhai Zhaoxiu na picha alizochora kwenye kuta za nyumba za kijijini

cri

Mwandishi wetu wa habari alipoingia kwenye kijiji cha Loujiashan cha wilaya ya Zhanyi mkoani Yunnan, kusini magharibi mwa China aliona picha nyingi nzuri zilizochorwa kwenye kuta za nyumba za wanakijiji. Picha hizo zinaonesha mandhari ya kimaumbile na maisha ya wanavijiji kama vile shughuli za kilimo na hali ya wakulima kucheza michezo ya kisanaa. Michoro hiyo ya ukutani imekipamba kijiji hicho kiwe kizuri sana. Mwandishi wa habari aliambiwa kuwa, michoro hiyo yote ilichorwa na Bi. Zhai Zhaoxiu. Bi. Zhai Zhaoxiu ana umri wa miaka 40 hivi, alipoulizwa ni kwa nini anapenda kuchora picha ukutani alisema:

"Kutokana na kuathiriwa na babu yangu nilipenda kuchora na kuandika tokea nilipokuwa mtoto. Ndoto yangu ilikuwa ni kuwa mwalimu wa uchoraji."

Mwaka 1985 Bi. Zhai Zhaoxiu alihitimu masomo ya sekondari ya juu na kutimiza ndoto yake, akawa mwalimu wa uchoraji katika shule moja ya nyumbani kwao. Baadaye alifaulu mtihani na kupata diploma katika somo la uchoraji wa kichina. Wakati huo kutokana na kuwa watu wachache wa vijijini walipata elimu ya juu, hivyo mwaka 1987 Bi. Zhai Zhaoxiu alitakiwa kurudi kijijini na kuteuliwa kuwa karani na kamati ya kijiji.

Mwaka 2005 katika ujenzi wa vijiji vya aina mpya nchini China, wilaya ya Zhanyi ilitenga fedha kukarabati barabara za vijiji, na kupaka rangi kwenye kuta za nyumba za wanavijiji. Bi Zhai Zhaoxiu alipoona kuwa ukuta uliopambwa ni mweupe na safi, alishikwa na wazo la kuonesha sanaa za kiutamaduni ikiwa ni pamoja na kuchora picha na kuandika maandiko kwenye ukuta mweupe. Wazo lake liliungwa mkono na viongozi na wanakijiji. Mwezi Septemba mwaka 2005, Bi. Zhai Zhaoxiu alianza kazi yake ya kuchora picha kwenye kuta za nyumba za wanakijiji. Na katika muda wa mwezi mmoja alimaliza picha zaidi ya 30. Kila siku alianza kazi saa moja ya asubuhi, baada ya chakula cha mchana aliendelea na kazi yake bila kupumzika mpaka jioni. Michoro yake ilisifiwa sana na wanakijiji wenzake, na aliombwa na wanakijiji wengi zaidi kuwasaidia kuchora picha ukutani.

Juhudi za Bi. Zhai Zhaoxiu ziliungwa mkono na watu wengine waliofahamu kuchora, kama vile walimu wa shule ya msingi, makada waliostaafu, na ndugu zake. Katika muda wa miezi minne tu, picha 300 za ukutani zilichorwa, na zikakipamba kijiji hicho na kukifanya kionekane kinapendeza sana. Picha hizo zinaonesha mandhari, maua, ndege, picha za kuchekesha, maandiko ya kichina, hali mpya ya kistaarabu, utulivu na masikilizano na shughuli za kijamii, zimekuwa vitabu vizuri vya kiada vya kuwaelimisha wanakijiji mambo ya sheria, sera na ustaarabu. Mwanakijiji Zhao Dabao alisema:

"Zamani tulihusudu maisha ya wakazi waishio mijini, lakini hivi sasa sina wazo hilo, katika harakati ya ujenzi wa vijiji vya kistaarabu, na kuelekezwa na picha zilizochorwa kwenye ukuta, wanakijiji wengi wameinua ufahamu wao na sifa zao, vitendo visivyo kistaarabu vinatoweka hatua kwa hatua."

Mabadiliko ya kijiji cha Loujiashan yamevutia ufuatiliaji mkubwa wa watu wa vijiji vingine karibu. Watu hao wamekuwa wanakuja kwa nyakati tofauti kumwomba Bi. Zhai Zhaoxiu awasaidie kusanifu mpango wa kupamba vijiji vyao. Hivi sasa Bi. Zhai Zhaoxiu amekuwa na shughuli zaidi, tena anapanga kuanzisha chama cha kaligrafia na uchoraji, kuwaandaa bila malipo watoto wa wakulima waishio katika sehemu za karibu wanaopenda kujifunza maandiko na uchoraji.

Picha zilizochorwa kwenye ukuta zimekuwa na umaalum mkubwa wa utamaduni wa vijijini vya wilaya ya Zhanyi. Picha hizo si kama tu zimepamba maisha ya wakulima, bali pia zimekabidhi ujuzi na ustaarabu kwa wakulima hao. Picha za ukutani zimeonesha matakwa makubwa ya wakulima ya kupamba maskani yao na mtizamo wao wa kimaisha wa kufanya juhudi zaidi.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-18