Kwenye mkutano wa 31 wa kimataifa kuhusu urithi wa dunia uliofanyika huko Christchurch, New Zealand, ombi kuhusu "ardhi ya chokaa ya sehemu ya kusini mwa China" ikiwa ni pamoja na msitu wa mawe wa mkoani Yunnan, tunda la Litch pamoja na Wulong ya mji wa Chongqing, zilipita kwenye ukaguzi na upigaji kura, na zimeorodheshwa kuwa urithi wa dunia, na kuwa sehemu ya 34 ya urithi wa duni wa nchini China.
Msitu wa mawe uko kwenye wilaya inayojiendesha wa kabila la wa-yi, mkoani Yunnan, sehemu ya kusini magharibi mwa China, ukiwa umbali wa kilomita 78 kutoka Kunming, mji mkuu wa mkoa wa Yunnan. Mawe makubwa na madogo yaliyosimama kwenye miteremko, mabonde na sehemu zilizoinama ziko katika eneo lenye kilomita za mraba mia kadhaa. Mwongoza watalii Bi Yunhua alisema,
"Eneo la msitu wa mawe lenye kilomita za mraba 12, ni sehemu yenye sura ya ardhi ya chokaa inayochukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa nchini China na hata duniani. Kwa kawaida tunaangalia mandhari ya eneo hilo kwa kutembea kwa miguu, ndani ya msitu wa mawe, kuna njia panda zaidi ya 400 na sehemu zenye mandhari nzuri zaidi ya 200, hivyo inajulikana kama ni kasri lenye sehemu ambayo si rahisi kufikika."
Sehemu inayojulikana kama 'Msitu mkubwa wa mawe' iko katikati ya eneo zima la msitu wa mawe, na ni sehemu yenye mandhari nzuri zaidi ya mawe marefu yaliyochongoka na iliyogunduliwa mapema zaidi. Mawe yaliyoko katika sehemu hiyo yana rangi ya kijivu kizito, ambayo ni aina halisi ya mawe yaliyoko kwenye ardhi ya Chokaa. Mbali na hayo, huko pia kuna sehemu nyingine zenye mandhari nzuri zikiwa ni pamoja na "Vilele vyenye umbo la ua la yungiyungi" na "Bwawa la upanga". Kutokana na kuongozwa na Bi Yunhua, tulisimama kwenye mawe marefu yanayojulikana kama "Mlima wa panda na bahari ya moto".
"Mawe hayo yanajulikana kama "Mlima wa panga na bahari ya moto", kutokana na kuwa, mawe ya juu yanaonekana kama panga nyingi zinazoelekea mbinguni kutokana na kuliwa na maji ya mvua, mawe yaliyoko chini ambayo yaliwahi kufukiwa ardhini ni yenye dalili ya kuwa maji yaliwahi kuyapita"
"Kibanda cha kuangalia vilele vya mawe" ni mahali pazuri pa kujiburudisha kwa "msitu wa mawe". Bibi Ni Ni kutoka Shanghai alisema, matembezi kwenye msitu wa mawe yanamfanya ashangae kuhusu maajabu ya dunia.
"Mandhari nzuri, safi sana! Nikisimama kwenye kibanda hicho, ninaona mawe mengi sana yaliyoko hapa chini, nimeshangazwa sana na maajabu ya dunia, maumbile yametupatia binadamu vitu vingi vizuri."
'Msitu mkubwa wa mawe' una mawe mengi yanayokaribiana sana, mtu akipiga kila hatua chache anazuiliwa na jiwe moja kubwa. Mawe ya sehemu hiyo yana maumbo mengi, ambayo baadhi yake yanafanana sana na watu. Jiwe moja linalojulikana "Mama amemshika mkono mtoto" linaonekana kama mama anatembea akiwa amemshika mkono mtoto wake, na jiwe lingine linalojulikana kama "Tembo aliyesimama kwenye kilele cha jiwe" linaonekana kama kweli kuna Tembo mmoja aliyesimama kwenye sehemu ya juu ya jiwe kubwa. Kuna mawe karibu mia moja kama hayo yanayofanana na maumbo ya watu au vitu vingine. Dada aliyeongoza watalii alituambia kuwa, mawe yaliyoko kwenye msitu wa mawe, licha ya watu kujiburudisha kwa kuyaangalia, pia wanaweza kuyapapasa, tena baadhi ya mawe yakigongwa taratibu yanatoa sauti nzuri.
"Jiwe hilo linajulikana kwa jina la 'Jiwe la kengele', likipigwa kwa mkono linatoa sauti kama ya kengele."
Ikilinganishwa na "Msitu mkubwa wa mawe", "Msitu mdogo wa mawe" una mawe yasiyo marefu sana, lakini mawe hayo yanafanana zaidi na watu na vitu halisi. Baadhi ya mawe marefu yanatenganisha msitu mdogo wa mawe katika maeneo kadhaa. Jiwe linalovuma zaidi katika msitu mdogo wa mawe ni "Ashima", kwa sababu jiwe lile kubwa linalosimama kama nguzo linafanana na msichana mzuri wa kwenye hadithi ya kabila la Wa-yi anayeitwa Ashima: aliyefunga kilemba cha kitambaa, kubeba kikapu mgongoni, akisimama kule na kuangalia mbali. Hivi sasa zimewekwa taa kwenye sehemu ya "Msitu mdogo wa mawe", katika wakati wa usiku taa hizo zinawaka, mawe ya sehemu hiyo yanaonekana yanapendeza zaidi.
Kwenye upande wa kaskazini mwa eneo la msitu wa mawe, kuna sehemu yenye mawe mengi inayojulikana kwa "Neigu". Katika lugha ya Kisani ya kabila la wayi, "Neigu" ni neno lenye maana ya kale na rangi nyeusi. Mawe yaliyoko katika msitu wa mawe wa "Neigu" ni makubwa, ukitazama kutoka mbali, mawe hayo yanafanana na majengo makubwa yenye ngome, watu wakisimama juu ya mawe hayo makubwa wanaweza kuona mawe mengi yanayokaribiana sana, na kuonekana kama bahari yenye maji meusi. Mbali na mawe makubwa, chini ya msitu wa mawe wa "Neigu" kuna mapango ya ajabu. Bibi Briana Lopez kutoka Australia baada ya kutembelea msitu wa mawe wa "Neigu", alisema, uzuri wa msitu wa mawe unanishangaza sana. Alisema,
"Maumbo ya mawe hayo ni mazuri sana na ya kushangaza."
Rangi ya mawe ya huko inabadilika kwa kufuata mabadiliko ya hali ya hewa. Mvua ikinyesha, mawe yenye rangi ya kijivu chepesi yanabadilika kuwa na rangi nyeusi. Jua linachomoza baada ya mvua, baada ya dakika kumi kadhaa, mawe yale ya rangi nyeusi yanabadilika kuwa na rangi mbalimbali, na hatimaye yanabadilika kuwa na rangi ya kijivu nyepesi, kweli yanashangaza watu. Mtaalamu wa mabaki ya dunia profesa Liang Yongning alisema, msitu wa mawe wa mkoa wa Yunnan unastahili kuitwa jumba la makumbusho la ardhi yenye sura ya msitu wa mawe duniani.
"Msitu wa kila aina duniani unaweza kupatikana hapa, mawe makubwa yaliyoko mbele yetu ni yenye umbo la upanga, tukienda sehemu nyingine, tunaweza kuona mawe yenye umbo la mnara, katika sehemu nyingine tunaweza kuona mawe yenye umbo la uyoga, yenye rangi nyeusi, manjano na maumbo mengine na rangi nyingine mbalimbali. Mtaalamu mmoja wa nchi ya kigeni alisema, baada ya kufika kwenye msitu wa mawe wa hapa, wakati fulani aliona kama amefika Cuba, baada ya dakika chache aliona kama yuko nchini Hispania, alisema mbona misitu yote ya mawe kama imehamishiwa hapa kuja kushiriki maonesho. Eneo hilo ni jumba la makumbusho ya sura ya ardhi ya msitu wa mawe, ni lenye thamani kubwa sana."
Wasikilizaji wapendwa, kivutio cha msitu wa mawe ni kuwa watu kamwe hawawezi kufahamu uzuri wake, kinafanya watu kushindwa kueleza vizuri uzuri wake kwa lugha ya binadamu. Kilele kile kile cha jiwe kubwa, katika majira tofauti, hali ya hewa tofauti, hata katika nyakati tofauti za siku moja, kinaonekana kwa sura tofauti na kumpa mtu hisia tofauti.
Idhaa ya kiswahili 2007-07-16
|