Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-17 10:01:23    
Kuendeleza kilimo kinachobana matumizi ya maji kuna manufaa mengi

cri

Kilimo ni sekta inayotumia maji mengi zaidi nchini China. Matumizi ya maji kwenye sekta hiyo yanachukua asilimia 64 ya matumizi yote ya maji nchini kote, lakini kwenye uzalishaji wa kilimo nusu ya maji yanapotea. Kutokana na kuwa na upungufu mkubwa wa maji, sehemu nyingi za China zimeanza kuendeleza kilimo kinachobana matumizi ya maji, ili kupata faida nyingi zaidi kwa matumizi kidogo ya maji. Sehemu ya kaskazini mwa China ni sehemu iliyo kavu zaidi.

Katika kijiji cha Dongliang cha mji mdogo wa Xinzhuang mjini Zhaoyuan mkoani Shandong, Bw. Liu Xingliang mwenye umri wa miaka 65 ana mashamba ya mizabibu zaidi ya hekta 30. Katika mashamba yake ya mizabibu kuna mabomba ya maji ambayo yanadondosha maji. Bw. Liu alimwambia mwandishi wa habari kuwa, teknolojia hiyo ya umwagiliaji maji kwa njia ya matone ni ya kisasa zaidi duniani, alisema,

"Haifai kutumia maji mengi wakati wa kumwagilia mashamba ya mizabibu. Mizizi ya mizabibu iko sentimita 20 chini ya ardhi. Ni bora mbolea ziwekwe kwenye sehemu hiyo. Umwagiliaji maji kwa njia ya matone hautasababisha mbolea ivuje chini zaidi."

Bw. Liu Xingliang alisema alianza kupanda zabibu mwaka 2000, na baada ya miaka miwili alianza kutumia vifaa vya umwagiliaji maji kwa matone. Zamani mavuno ya zabibu kwa hekta yalikuwa kilo 60, hivi sasa yamefikia kilo 120. Umwagiliaji maji kwa matone ni njia ya kisasa ya umwagiliaji maji ambayo inasaidia kubana matumizi ya maji. Lakini bei za vifaa vya umwagiliaji maji kwa matone ni ghali, wakulima wengi hawawezi kumudu. Hivi sasa makampuni ya mazao ya kilimo kushirikiana na vijiji imekuwa njia ya kawaida ya kueneza matumizi ya teknolojia hiyo. Kwa mfano vifaa vinavyotumiwa kwenye mashamba ya mizabibu ya Bw. Liu vilinunuliwa na kijiji cha Dongliang na kampuni ya Fufazhongji ya Singapore, na zabibu zinazozalishwa katika mashamba hayo zinanunuliwa na kampuni hiyo na kuuzwa katika nchi za nje. Hivyo makampuni ya mazao ya kilimo na wakulima wote wanapata faida. Kutokana na takwimu zisizokamilika, mashamba yanayotumia teknolojia ya umwagiliaji maji kwa njia ya matone yamekuwa zaidi ya hekta laki 8.

   

Kadi za IC ni vitu vya kawaida katika maisha ya watu. Katika kijiji cha Xiaowu wilayani Qingxu mkoani Shanxi, Kadi za IC zinatumiwa katika umwagiliaji maji. Katika kijiji cha Xiaowu chenye mashamba zaidi ya hekta 370, jambo linalomsumbua zaidi naibu mkurugenzi wa kamati ya kijiji hicho Bw. Hou Zhongxi ni kazi ya kutoza matumizi ya maji. Hivi sasa Bw. Hou Zhongxi hasumbuliwi na jambo hilo. Katika kijiji hicho maji yanayotumiwa mashambani yanatoka visimani. Zamani maji hayo yalipelekwa mashambani kwa mifereji, lakini wakati yalipopelekwa sehemu kubwa ya maji hayo ilifyonzwa na ardhi. Mwaka 2003 mfumo wa kutoza gharama za matumizi ya maji kwa kutumia kadi ya IC ulianza kutumiwa katika kijiji hicho, kila familia ilipata kadi ya IC, hivyo matatizo ya kutoza gharama za matumizi ya maji yalitatuliwa. Na hivi sasa njia ya kusafirisha maji imebadilishwa, maji yanapelekwa kwa mabomba chini ya ardhi badala ya mifereji ili kuzuia maji yasifyonzwe na ardhi; tena kijiji hicho kinachukua hatua kuwafundisha wakulima njia za kubana matumizi ya maji. Zamani wastani wa mapato kwa familia ulikuwa Yuan elfu kadhaa tu, hivi sasa kutokana na teknolojia ya kubana matumizi ya maji, wanakijiji wanapanda mboga katika mashamba mengi zaidi, katika miaka miwili iliyopita wastani wa mapato kwa familia ulikuwa zaidi ya yuan elfu 10.

Kutokana na kutumia teknolojia ya umwagiliaji maji inayobana matumizi ya maji, wakulima wa sehemu nyingi wamebadilisha aina za mimea wanazopanda. Katika kijiji cha Dongnanfang wilayani Qingxu mkoani Shanxi, mkurugenzi wa kamati ya kijiji hicho Bw. Yang Shengli alitambua kuwa wakulima hawawezi kupata mavuno makubwa kwa kupanda nafaka kwenye ardhi kavu, hivyo aliwaongoza wanakijiji kupanda alfalfa ambayo ni malisho ya mifugo kwa kutumia vifaa vya umwagiliaji maji vinavyobana matumizi ya maji, alisema,

"Hatua hiyo imeongeza mapato ya wakulima, zamani wakulima waliweza kupata yuan elfu 3 kwa hekta, baada ya kupanda alfalfa na miti ya matunda wanaweza kupata yuan elfu 7.5 kwa hekta. Sasa tunapanda alfalfa kwenye hekta 130."

Licha ya kueneza teknolojia ya umwagiliaji inayobana matumizi ya maji, sehemu nyingi za China zinajaribu kuanzisha utaratibu mpya wa usimamizi wa maliasili ya maji. Mradi wa "mwangaza ya jua" unatekelezwa katika sehemu ya Jiamakou mkoani Shanxi. Wanavijiji waliunda shirikisho la matumizi ya maji kwa upigaji kura, na shirikisho hilo linagawa maji, kuwahudumia wakulima, kutangaza bei na kiasi cha maji na wakati wa kutoa maji.

Wakulima wanaridhika na kufurahia mradi huo. Bw. Ren Dezhang anayeishi katika kijiji cha Jingjiazhuo cha sehemu ya Jiamakou amepanda miti ya matunda kwa miaka kumi kadhaa. Zamani hakujua alikuwa hajui anamwagilia maji mimea yake kwa mara ngapi, na alipokuwa analipia gharama za matumizi ya maji alisikitika sana, hivi sasa hali hiyo imebadilika, alisema,

"Ninapotaka kumwagilia maji nitamwambia mkuu wa shirikisho la matumizi ya maji, na atanipatia maji, baadaye nitalipia gharama za matumizi ya maji. Ni rahisi kupima kiasi cha maji ninachotumia, na bei ya tani moja ya maji ni Yuan 0.44."

Maeneo ya mashamba yanayotumia teknolojia ya umwagiliaji maji inayobana matumizi ya maji yameongezeka kwa kiasi kubwa, lakini ukosefu wa fedha bado ni suala kubwa linalozuia uenezi wa teknolojia hiyo. Naibu mkurugenzi wa idara ya majengo ya maji vijijini ya wizara ya maji ya China Bw. Li Yuanhua alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,

"Nchini China wastani wa eneo la mashamba kwa mkulima ni mdogo, na miradi ya kubana matumizi ya maji kwenye sekta ya kilimo haiwezi kujengwa kwa nguvu ya familia moja au kijiji kimoja, hivyo wakulima hawawezi kutenga fedha nyingi ili waweze kutumia teknolojia ya umwagiliaji inayobana matumizi ya maji."

Bw. Li Yuanhua alisema wizara ya maji ya China itafanya juhudi kutunga mipango, kuongoza jamii itenge fedha nyingi, kutilia mkazo kutatua suala la matumizi ya maji katika sehemu zinazozalisha nafaka kwa wingi, sehemu zinazokabiliwa na upungufu mkubwa wa maji na sehemu ambazo uchumi ulio nyuma, na kuwaongoza na kuwahimiza wakulima kutumia teknolojia ya umwagiliaji inayobana matumizi ya maji, ili kuongeza mapato ya wakulima.