Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-20 15:29:29    
China na Kenya zana fursa nyingi za ushirikiano katik sekta ya nishati ya jua

cri

Suala la nishati ni suala linalozingatiwa duniani siku zote. Hivi sasa soko la kimataifa la nishati lina mabadiliko makubwa, mapambano ya kugombea nishati yanazidi kuwa makali, na tatizo la usalama wa nishati limetokea, hivyo kuendeleza matumizi ya nishati endelevu kumekuwa ni sehemu muhimu ya mkakati wa maendeleo kwa nchi nyingi. Baada ya kufanya uchunguzi kwa siku nne nchini Kenya, mkurugenzi wa kituo cha nishati ya jua cha shirika la maendeleo ya viwanda la Umoja wa Mataifa, ambaye pia ni mkuu wa taasisi ya nishati ya viumbe mkoani Gansu Bw. Xi Wenhua alisema, zikiwa nchi zinazoendelea, China na Kenya zina fursa nyingi za ushirikiano katika kueneza na kutumia teknolojia na bidhaa za nishati ya mwangaza wa jua.

Kenya iko kwenye ukanda wa Ikweta. Nchi hiyo iko kwenye mwinuko wa kati ya mita 1,500 hadi 2,000 kutoka usawa wa bahari, na ni nchi yenye raslimali nyingi ya nishati ya jua. Mhandisi mkuu wa wizara ya nishati ya Kenya Bw. Issac Kiva alijulisha kuwa

"Mionzi ya jua inayopata Kenya kwa siku inafikia Megawati/saa bilioni 2.95, na ni kama asilimia 10% tu kati ya hizo ndio zikitumika, kiasi cha umeme unaozalishwa nchini Kenya kwa nishati ya jua utafikia Megawati/saa milioni 295."

Hivi sasa mahitaji ya umeme nchini Kenya ni Megawati/saa bilioni 13, hii ina maana kuwa mionzi ya jua moja kwa 230 ikitumika na kuwa umeme, itatosheleza mahitaji ya umeme kote nchini Kenya.

Baada ya kufanya uchunguzi kwa siku kadhaa nchini Kenya, mkurugenzi wa kituo cha nishati ya jua cha shirika la maendeleo ya viwanda la Umoja wa Mataifa ambaye pia ni mkuu wa taasisi ya nishati ya viumbe mkoani Gansu Bw. Xi Wenhua alisema, kuna uwezekano mkubwa wa kuanzisha soko kubwa kabisa barani Afrika au sehemu ya viwanda ya nishati ya jua nchini Kenya. Alisema,

"Kenya ni nchi inayoendelea kama China, katika sehemu za milimani au mipakani, pia hakuna umeme. Hivyo kuna mustakabali mzuri wa kueneza matumizi ya umeme unaozalishwa kwa nishati ya jua nchini Kenya. Nafikiri ni vizuri kueneza matumizi ya umeme unaozalishwa kwa nishati ya jua na jiko la nishati ya jua vijijini nchini Kenya. Hoteli na majengo makubwa mijini yanaweza kutumia mitambo ya kupasha moto maji kwa nishati ya jua. Kwa mfano huko Mombasa kuna joto kali, mkoa huo unaweza kutumia nishati ya jua ili kupunguza halijoto. Nina matumaini kuwa sehemu ya viwanda vya bidhaa zinazotumia nishati ya jua barani Afrika itaanzishwa hapa Mombasa, na soko kubwa kabisa la nishati ya jua litaanzishwa hapa pia. Nataka kuhimiza kueneza na kutumia teknolojia ya nishati ya jua barani Afrika kwa kupitia Kenya."

Bw. Kiva alisema wizara ya nishati ya Kenya ilifanya juhudi nyingi katika kueneza na kutumia teknolojia na bidhaa za nishati ya jua, kwa mfano kutunga waraka wa teknolojia ya mwangaza na umeme wa nishati ya jua, kueneza matumizi ya mashine ya kupasha maji moto kwa kutumia nishati ya jua kwenye hoteli kubwa, kuanzisha vituo vya nishati ya jua ili kuonesha teknolojia ya kisasa ya nishati ya jua, na kuwaelekeza watu namna ya kutumia bidhaa za nishati ya jua.

Bw. Kiva alisema wizara ya nishati ya Kenya inaelekea kwenye lengo la kuendeleza kwa ufanisi matumizi ya nishati ya jua. Lakini maendeleo ya kueneza teknolojia na bidhaa hizo yanakabiliwa na tatizo kubwa, yaani uwezo wa wakazi wa huko kununua bidhaa hizo ni mdogo sana, na bei ya bidhaa zinazotumia nishati ya jua ni kubwa. Alisema kutatua suala hilo kunahitaji kushiriki kwa wenzi wa ushirikiano wa nchi za nje ikiwemo China. Alisema, (??????)

"Tatizo tunalokabiliana nalo ni bei kubwa ya bidhaa zenye teknolojia ya kutumia nishati ya jua, hivi sasa tumekuwa tunaandaa sera, sheria na kanuni husika, tunataka kuwahimiza washirika wengi zaidi washiriki kwenye sekta ya matumizi nishati ya jua nchini Kenya, ili bei ya bidhaa iweze kupungua, na watu wengi waweze kunufaika na teknolojia hiyo. Tunawakaribisha washirika wa nchi zinazoendelea kama China. China na Kenya zina fursa nyingi za ushirikiano."

Bw. Kiva alisema, hivi sasa China ina maendeleo ya kasi, nchini China teknolojia nyingi za nishati endelevu zikiwemo teknolojia ya nishati ya jua zinatumika. Kenya inataka kufanya ushirikiano na China katika kupata teknolojia, na inaitaka China iisaidie katika kujenga uwezo wa kupata teknolojia hiyo. Alisema Kenya inavihamasisha viwanda vya China viwekeze nchini Kenya ili kupunguza bei ya bidhaa zinazotumia teknolojia ya nishati ya jua. Bw. Kiva alisema serikali za China na Kenya zina uhusiano wa kirafiki, na Kenya inafurahia sana kushirikiana na China katika sekta ya nishati ya jua.

Kenya ilianza kutumia nishati ya jua mwaka 1977, lakini baadaye miradi ya nishati ya jua haikudumu, kwa sababu miradi hiyo ilitegemea kununua bidhaa za nishati ya jua kutoka nchi za nje tu. Katika miaka 30 iliyopita, uzoefu na mafunzo uliwafundisha wakenya kuwa, maendeleo endelevu yanaweza tu kupatikana kwa kuwa na teknolojia, bidhaa na mafunzo. Bw. Xi Wenhua alisema,

"China ina teknolojia na bidhaa nyingi zinazohitajiwa na nchi zinazoendelea, kila mwaka China inatoa mara mbili mafunzo kuhusu teknolojia ya nishati ya jua, mafunzo hayo yanatolewa kwa nchi zinazoendelea. Kenya imewahi kutuma wanafunzi tisa nchini China na kushiriki kwenye mafunzo hayo, hivyo Kenya inazoea teknolojia na bidhaa za nishati ya jua za China."

Bw. Michael Munyao ni mfanyabiashara wa Kenya ambaye anajishughulisha na biashara ya kimataifa kwa miaka mingi. Aliona kuwa ushirikiano kati ya China na Kenya katika sekta ya nishati ya jua utamnufaisha kihalisi yeye na wananchi wa nchi hizo mbili. Alisema

"Kuna faida kubwa katika soko la nishati ya jua, hivi sasa soko hilo linaendelezwa kwa utulivu, nafikri nitapata pesa nyingi katika soko hilo. Nina matumaini kuwa wenzetu wa China wataleta teknolojia nchini Kenya, na kuanzisha viwanda hapa, hatua hizo zitaongeza nafasi za ajira, na kuinufaisha Kenya. Hivyo si kama tu tunanunua na kuuza bidhaa, bali ni muhimu zaidi kuanzisha viwanda vya pamoja vya China na Kenya, ili Kenya iwe na uwezo wa kutengeneza bidhaa zinazotumia nishati ya jua. "

Idhaa ya kiswahili 2007-07-20