Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-07-23 16:19:23    
Ushirikiano katika sekta ya filamu kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong waimarika

cri

Tarehe mosi Julai ilikuwa ni siku ya kuadhimisha miaka 10 tokea Hong Kong irudishwe nchini China. Katika muda wa miaka 10 iliyopita maingiliano kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong yamekuwa yakiongezeka siku baada ya siku katika uchumi na utamaduni, na ushirikiano katika sekta ya filamu pia unazidi kuimarika, katika muda huo filamu zilizotengenezwa kwa ushirikiano zimekuwa zaidi ya 200.

Siku chache zilizopita, filamu ya "Hadithi ya Kweli ya Hong Kong" iliyotengenezwa na watu wa Hong Kong kwa ajili ya kuadhimisha mwaka wa 10 tokea Hong Kong irudishwe nchini China ilioneshwa nchini China. Filamu hiyo inaeleza mabadiliko makubwa ya maisha ya mwonesha filamu mmoja yaliyotokea katika muda wa miaka 40, na inaonesha wakazi wa Hong Kong wanavyoipenda nchi yao kwa kueleza matukio makubwa kama kurudishwa kwa Hong Kong kwa China kutoka kwa Uingereza, mgogoro wa mambo ya fedha barani Asia na mlipuko wa ugonjwa wa SARS. Tumaini kubwa alilokuwa nalo mwonesha filamu katika filamu hiyo lilikuwa ni kwenda Beijing kutazama uwanja wa Tian An Men.

Tokea Hong Kong irudishwe nchini China mwaka 1997, pande mbili, sehemu ya dani ya China na Hong Kong, zimefanya juhudi nyingi kushirikiana katika sekta ya filamu, na zilishirikiana vizuri kutengeneza filamu zaidi 200. Mwaka 2003 kati ya filamu 10 zilizoongoza katika mapato ya tikiti, filamu 7 ni filamu zilizotengenezwa kwa ushirikiano. Meneja wa Kampuni ya Maingiliano na Nje katika sekta ya filamu Bw. Yang Buting alieleza,

"Miongoni mwa filamu 10 zilizoongoza katika mapato ya tikiti, filamu 7 zilitengenezwa kwa ushirikiano kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong. Filamu kama "Shujaa", "Karamu ya Usiku", "Dunia isiyo na wezi", zote zinasifiwa sana na kupata mapato mazuri kwa kuuza tikiti."

Bw. Yang Buting alisema, filamu za gongfu za Hong Kong zinajulikana duniani, na katika sehemu ya ndani ya China kuna riwaya nyingi za gongfu, kuna mazingira mengi yanayolingana na riwaya hizo na waongoza filamu kama hizo pia ni wengi, kwa hiyo ushirikiano wa pande mbili unaweza kutengeneza filamu za gongfu zilizo nzuri zaidi. Kwa mfano, filamu ya "Shujaa" iliyoongozwa na mwongozaji mashuhuri wa filamu Zhang Yimou. Filamu hiyo ni tofauti na nyingine za gongfu, kwamba imechanganya utamaduni wa kale wa China, na kuchezwa na mwigizaji mashuhuri wa Hong Kong, filamu hiyo imepata mapato makubwa kutokana na kupata watazamaji wengi nchini China na nchi za nje.

Mwaka 2005 msanii wa Hong Kong Bw. Liu Dehua alimfadhili mwongozaji kijana wa filamu wa sehemu ya ndani ya China kwa ajili ya kutengeneza filamu ya "Hadithi ya Jade". Filamu hiyo ni ufanisi wa ushirikiano kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong. Filamu hiyo inaeleza jinsi genge la wezi lilivyojaribu kuiba jiwe kubwa la jade lenye thamani kubwa na kutokea vituko vingi vya kuchekesha. Gharama za kutengeneza filamu hiyo ilikuwa ndogo, lakini imepata mapato makubwa katika mwaka ilipooneshwa filamu hiyo 2005. Meneja mkuu wa Kundi la Vyombo vya Habari vya Hong Kong Bw. Feng Yong alipotathmini filamu hiyo alisema,

"Filamu hii ni kama mpaka kati ya filamu za kuchekesha za zamani na za leo za Hong Kong, hapo kabla filamu za kuchekesha huko Hong Kong zilikuwa chache, na pia hazikufanikiwa sana, lakini sasa filamu kama hizo zimetokea Hong Kong."

Katika muda wa miaka kumi iliyopita tokea Hong Kong irudishwe nchini China, ushirikiano katika sekta ya filamu kati ya sehemuu ya ndani ya China na Hong Kong umepata maendeleo makubwa. Bw. Xu Xiaoming ni mwongozaji wa filamu mashuhuri wa Hong Kong na ni mtu wa kwanza kujulisha filamu za Hong Kong katika sehemu ya ndani ya China. Alipozungumzia ushirikiano huo alisema,

"Ushirikiano katika sekta ya filamu kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong katika miaka kumi iliyopita umepata mafanikio makubwa, na katika mashindano ya filamu duniani filamu zetu pia zimepata tuzo ya Osca. Miaka kumi iliyopita sikutegemea kwamba filamu zetu za ushirikiano zingeweza kupata mapato ya tikiti Yuan milioni mia kadhaa, hii inadhihirisha kuwa filamu za China zimepata maendeleo makubwa."

Siku chache zilizopita, maonesho ya filamu zilizotengenezwa kwa ushirikiano kati ya sehemu ya ndani ya China na Hong Kong yalifanyika mjini Beijing. Kwa kuangalia filamu hizo, watu wana uhakika kuwa ushirikiano kati ya pande mbili utakuwa na mustakbali mzuri zaidi. Meneja mkuu wa Kundi la Vyombo vya Habari vya Hong Kong Bw. Feng Yong alisema,

"Mimi katika nafsi yangu naona kwamba Hong Kong ina sifa zaidi katika usimamizi, uchangishaji wa fedha na usambazaji wa filamu nje ya China, na sehemu ya ndani ya China ina sifa za utengenezaji, utungaji wa hadithi za filamu ambazo hasa zinahusiana na utamaduni wa kale, na kuwa gharama ndogo za utengenezaji wa filamu ikilinganishwa na Hong Kong."

Bw. Feng Yong alisema, soko la filamu la Hong Kong ni dogo, na soko hilo katika sehemu ya ndani ya China ni kubwa. Muda wa miaka kumi iliyopita tokea Hong Kong kurudishwa nchini China ulikuwa ni muda wa sehemu ya ndani ya China na Hong Kong kutafuta ushirikiano katika sekta ya filamu, na filamu kadhaa zilizotengenezwa kwa ushirikiano zimepata njia nzuri ya ushirikiano ambayo inakubaliwa na kukaribishwa na wanafilamu wa pande mbili. Huu ni ushirikiano wa kunufaisha pande zote mbili.

Idhaa ya kiswahili 2007-07-23