Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-01 15:23:23    
Serikali ya China yachukua hatua kulinda haki na maslahi ya watoto wa vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi nchini China, katika miaka ya hivi karibuni idadi ya wakulima wanaomiminikia mijini kutafuta kazi za vibarua imeongezeka kwa haraka, na watoto wao wanaoachwa vijijini wamekuwa wanakabiliwa na matatizo mengi kama vile kukosa matunzo, utapiamlo, elimu na afya. Takwimu zinaonesha kuwa hivi sasa China ina watoto zaidi ya milioni 20 wa vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini.

Ili kutatua matatizo hayo ambayo yameathiri maendeleo ya watoto husika na ujenzi wa vijiji vya aina mpya na utulivu wa jamii yenye masikilizano, shirikisho kuu la wanawake la China hivi karibuni lilifanya kongamano la kuimarisha kazi ya kuwashughulikia watoto wa aina hiyo. Kongamano hilo liliwashirikisha maofisa kutoka idara husika, kama vile wizara ya afya, wizara ya elimu na wizara ya mambo ya kiraia.

Katibu wa sekretarieti ya shirikisho kuu la wanawake la China Bw. Zhang Shiping alisema, kutatua masuala yanayowakabili watoto wa aina hiyo kwanza kunatakiwa kuweka mazingira mazuri ya kuishi kwa watoto na wazazi wao, ili kuwawezesha watoto hao wapate ulinzi na usimamizi mzuri wa kifamilia, kuchukua hatua kuwaelimisha wazazi na wasimamizi wa watoto wa aina hiyo namna ya kuwatunza watoto ipasavyo, kuenzi ujuzi wa kisheria wa kuwalinda watoto, kuwaelekeza wazazi kufuatilia elimu na maendeleo ya watoto wao.

Ofisa husika wa wizara ya afya ya China Bwana Sun Jiahai alisema, idara za afya katika ngazi tofauti nchini China zinatakiwa kuhakikisha watoto wa vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini wapate huduma za afya za kimsingi. Alidhihirisha kuwa idara husika za afya zitaimarisha uchunguzi kuhusu hali ya afya ya watoto wa aina hiyo, ili kuchukua hatua mwafaka kama vile kupima hali ya ukuaji wa watoto hao, kutoa maelekezo ya kuwapa watoto hao vyakula vyenye virutubisho vya kutosha, na kuwapa kinga ya maradhi kwa wakati.

Na ofisa husika wa wizara ya elimu ya China amesema idara za elimu katika ngazi tofauti nchini China zimeagizwa kutunga hatua na utaratibu husika wa kuhakikisha watoto wa aina hiyo ambao wanabaki vijijini au kufuatana na wazazi wao mijini wanapewa fursa sawa ya kupata elimu ya lazima, na hawataongezewa gharama za kwenda shule mijini.

Ofisa huyo alisema idara za elimu katika sehemu vijijini ambazo wakazi wake wengi wanakwenda mijini kufanya kazi za vibarua, zinatakiwa kushirikiana na serikali za huko kuimarisha ujenzi wa shule za bweni vijijini, kutoa kipaumbele kwa watoto wa aina hiyo kusoma katika shule za bweni na kuwawekea mazingira mazuri ya kusoma na kuishi.

Ofisa husika wa wizara ya mambo ya kiraia Bwana Li Quanmao alisema, idara husika za mambo ya kiraia katika ngazi tofauti nchini China zinatakiwa kuimarisha uchunguzi kuhusu hali ya umaskini ya familia za watoto wa vijijini, ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini, ili kutunga sera husika kuhakikisha watoto wa aina hiyo wenye matatizo ya kiuchumi wapate misaada ya kijamii. Idara husika pia zinapaswa kuchukua hatua kuwazuia watoto wa vijijini wasiende kurandaranda mijini, na kwa wale ambao tayari wametoka nje na kurandaranda mijini wanatakiwa kurejeshwa vijijini na watunzwe kwa pamoja kwa kushirikiana na walezi wao.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-01