Katika miaka 50 iliyopita, China imefanya ushirikiano wa aina mbalimbali na Afrika katika sekta nyingi, hasa sekta ya kilimo. Ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya kilimo umepitia vipindi vitatu. Kipindi cha kwanza kilikuwa ni kuanzia mwaka 1959 hadi mwisho wa miaka ya 70 ya karne iliyopita, ambapo China ilitoa misaada kwa nchi za Afrika bila malipo. Muda wa mageuzi na marekebisho ni kipindi cha pili. Katika kipindi hicho ingawa misaada mingi iliyotolewa na China kwa Afrika bado haikutakiwa kulipwa, lakini China na Afrika zilitilia maanani zaidi usimamizi wa miradi ya ushirikiano na ufanisi wa kiuchumi wa miradi hiyo, na kusisitiza ushirikiano wa kuzinufaisha pande hizo mbili. Kuanzia mwaka 1995, serikali ya China ilithibitisha wazi sera ya ushirikiano wa kunufaishana, ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya kilimo uliingia kwenye kipindi cha tatu, yaani ushirikiano chini ya mfumo wa uchumi wa soko huria.
Baada ya mageuzi ya mfumo wa ushirikiano huo, wataalamu husika walitoa mapendekezo mbalimbali kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya kilimo chini ya hali mpya. Naibu mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa mambo ya Afrika ya China ambaye pia ni profesa wa Chuo Kikuu cha Nanjing Bw. Jiang Zhongjin alitoa maoni yake kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta ya kilimo, akisema "Maoni yangu ni kuwa matokeo ya utafiti wa kisayansi katika miradi ya elimu inayotolewa na China kwa kuisaidia Afrika yanapaswa kutumika kihalisi katika uzalishaji wa mazao ya kilimo. Kampuni zinapaswa kushiriki kwenye utafiti wa miradi ya elimu. Kama kampuni zikipenda kuwekeza, zinaweza kununua hataza, na kutumia matokeo hayo ili kupata maendeleo".
Tangu China ianze kutoa miradi ya elimu kwa kuisaidia Afrika, miradi zaidi 360 imeanzishwa katika nchi 21 barani Afrika, ambapo zimejengwa maabara 23 zikiwemo za tekenolojia ya biolojia, kompyuta, kazi ya utengenezaji wa vyakula?kemikali na mafunzo ya lugha ya Kichina. Kati ya hizo maabara ya teknolojia ya biolojia na maabara ya tekenolojia ya usanii wa bustani nchini Kenya na kituo cha utengenezaji wa vyakula nchini Cote' d'ivoire vilipata mafanikio makubwa, na kusifiwa na nchi zilizopokea misaada hiyo. Kutegemea msingi wa vituo hivyo, kufanya shughuli za kutoa mafunzo, kufanya utafiti na kutoa vielelezo, huu ni utaratibu wa kuwaandaa pamoja wanafunzi kwa walimu wa China na Afrika, pia ni njia muhimu ya China kutoa misaada ya elimu kwa Afrika.
Lakini Profesa Jiang vilevile alisema, baada ya upande wa China kukabidhi miradi hiyo ya elimu kwa upande wa Afrika, kama upande wa China hauwezi kuendelea kutoa misaada ya fedha, walimu, na zana, miradi mingi haiwezi kuendelea vizuri. Profesa Jiang alishauri kuwa kampuni za China zinapaswa kuzingatia kwanza kutoa miradi ya elimu kwa kuzisaidia nchi za Afrika wakati zinapotafuta miradi ya uwekezaji barani Afrika, ili kuyafanya matokeo ya utafiti wa kisayansi wa miradi ya elimu yatumike katika shughuli za uzalishaji na uuzaji. Hivyo miradi ya elimu inaweza kuwaandaa watu wenye ujuzi wa nchi za Afrika, pia inaweza kuhudumia maendeleo ya uchumi.
Rais Hu Jintao wa China kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika hapa Beijing aliahidi kuchukua hatua nane za misaada kwa nchi za Afrika. Hatua moja ni kutuma wataalamu 100 wa ufundi wa kilimo barani Afrika na kuanzisha vituo 10 vya vielelezo vya sayansi na tekenolojia za kilimo. Profesa Jiang aliona kuwa inapaswa kuimarisha umuhimu wa vituo hivyo vya vielelezo. Alisema, "Vituo hivyo vinapaswa kutoa vielelezo vya ufundi wa kilimo cha kisasa, mashine za kilimo na mafanikio ya kilimo. Pia vinapaswa kuwa vituo vya kutoa mafunzo ya ufundi wa kilimo cha kisasa kwa wakulima barani Afrika".
Profesa Jiang alisema, ufundi duni wa kilimo kwa wakulima wa Afrika ni sababu mojawapo inayokwamisha maendeleo ya kilimo barani Afrika. Alishauri yaanzishwe semina za usimamizi wa kilimo na ufundi wa kilimo, na kutoa mafunzo ya ufundi husika kwa wakulima wa huko. Wakulima wa huko wanaweza kujifunza katika vituo vya vielelezo vya kilimo. Wakulima ni nguvu kubwa ya kuzalisha vyakula, hivyo ni muhimu sana kutilia maanani elimu kwa wakulima, na kuongeza elimu na uwezo wao wa kilimo. Maendeleo ya kilimo yanapaswa kutegemea maendeleo ya sayansi na teknolojia na kuinua sifa ya nguvu kazi.
Profesa Jiang alisema serikali ya China inapaswa kuwahimiza wakulima wa China waende kufanya shughuli za kilimo barani Afrika, ili kuwapatia wakulima wa Afrika waweze kuiga ufundi wa kilimo wa China. Hivi sasa wakulima wa Afrika wanafanya juhudi ili kukidhi mahitaji ya kimsingi ya maisha, na bado wako mbali na utengenezaji na uuzaji wa mazao ya kilimo. Lakini wakulima wa China wamefanikiwa kuleta uzalishaji wa mazao ya kilimo kwenye soko, na maendeleo ya kilimo cha jadi yamebadilika kuwa uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa ajili ya mahitaji ya soko.
Profesa Jiang alijulisha kuwa wakulima wa China walianza kwenda barani Afrika na kufanya shughuli za kilimo tangu miaka ya 90 ya karne iliyopita, walinunua mashamba mengi madogo, na kupata mafanikio makubwa. Alisema
"Wakulima wengi wa China waliokuwa na kiasi fulani cha fedha, walijitolea kwenda kuwekeza barani Afrika. Walinunua mashamba kadhaa, na kuajiri wakulima wenyeji kati ya 20 na 30, pia walikwenda na baadhi ya wakulima wenye ujuzi kutoka China. Wengi wao walijishugulisha na kilimo cha mboga, na kupata mafanikio."
Profesa Jiang alisema, Wakulima wa China wanapofanya shughuli za kilimo barani Afrika, wanawaajiri watu wa huko. Hivyo wanaweza kutoa mchango katika kutatua tatizo la ajira la huko.
Profesa Jiang alisema katika miaka 50 iliyopita, kulikuwa na mafaniko na matatizo katika ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika. Katika siku za mbele inapaswa kutunga mpango mwafaka kwa msingi wa kimkakati wa maendeleo ya kilimo, na kuzisaidia nchi za Afrika kuwaandaa wataalamu wa kilimo cha kisasa, ili kuanzisha mfumo wa maendeleo endelevu wa kilimo.
Idhaa ya kiswahili 2007-08-10
|