Bi. Zheng Xiuzhen mwenye umri wa miaka 23, ni mkulima wa kijiji kimoja cha mkoa wa Henan. Mwezi Agosti mwaka 2005, Bi. Zheng Xiuzhen alipokuwa anarudi nyumbani pamoja na mchumba wake baada ya kufanya kazi shambani alimkuta mzee Guo Xiuqin akilala chini mahututi, yeye na mume wake walimchukua bibi huyo na kwenda naye nyumbani.
Baada ya kumtunza kwa makini kwa siku kadhaa, mzee Guo Xiuqin alianza kupata fahamu hatua kwa hatua, lakini aligunduliwa kuwa na mtindio wa ubongo, hakukumbuka alikotoka na wala hakutaja majina yoyote ya jamaa zake. Bi. Zheng Xiuzhen mwenye matatizo ya kiuchumi alishauriwa kumpeleka Bibi huyo Guo kwenye nyumba ya kuwapokea watu wanaorandaranda mitaani ya idara ya mambo ya kiraia, lakini hakufanya hivyo, bali aliamua kumtunza mzee Guo kwa upendo na kwa moyo mkunjufu kama mama yake mzazi.
Bi. Zheng Xiuzhen aliishi maisha magumu sana alipokuwa mtoto. Aliwahi kukumbwa na misiba mingi. Alipokuwa na umri wa miaka minne, kaka yake mkubwa alifariki dunia ghafla kutokana na kuugua ugonjwa wa dharura, mama yake alisononeka sana na kupoteza akili kama alivyo Bibi Guo na alifariki dunia mwaka 2003, baba yake pia alipoteza maisha katika ajali. Hivyo Bi. Zheng Xiuzhen anafahamu sana hisia za watoto wa bibi Guo. Alijua kuwa watoto wa bibi Guo hakika walikuwa wanahangaika sana kumtafuta, hivyo alijitahidi kuwatafuta, na aliwahi kuweka habari za mzee Guo kwenye tovuti ya Internet, lakini hakupata jibu. Hivyo Bi. Zheng Xiuzhen aliamua kumtunza bibi Guo yeye mwenyewe, na kumsihi mume wake wamtunze bibi Guo kwa pamoja.
Kwa bahati nzuri siku moja ya mwezi Aprili mwaka huu, Bibi Guo Xiuqin aliyekuwa ameishi pamoja na Bi. Zheng Xiuzhen kwa miaka miwili hivi alikumbuka ghafla anuani ya maskani yake na jina la mtoto wake. Bi. Zheng Xiuzhen aliwasiliana na mtoto wa bibi Guo mara moja. Jamaa wa bibi Guo walipofika nyumbani kwa Bi. Zheng Xiuzhen na kumkuta Bibi Guo akionekana msafi na afya nzuri walifurahi sana, walitaka kumshukuru kwa kumpa fedha, lakini Bi. Zheng Xiuzhen na mumewe walikataa. Alisema:
"Kama ningeshindwa kuwapata watoto wa Bibi Guo ningemtunza daima kama mama yangu mwenyewe. Sitaki fidia yoyote, nafurahi kufanya hivyo."
Mkwe wa kwanza wa Bibi Guo Bi. Hu Meihua alimwambia mwandishi wa habari kuwa:
"Baada ya mama kupotea, tulimtafuta sana mpaka tulikata tamaa. Tulipoambiwa kuwa labda mama ameshafariki dunia, tulihuzunika sana. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa bado yuko hai na anaishi kwa afya namna hii. Hatuna njia nyingine ya kumshukuru Bi. Zheng Xiuzhen, ila tu kumtendea kama jamaa asiyekuwa na uhusiano wa damu, tutamsaidia wakati wowote akituhitaji."
Hivi sasa Bi. Zheng Xiuzhen ni mja mzito, Bi. Hu Meihua alisema atamtunza dada yake atakapojifungua. Kama watu wote wanaweza kutoa msaada kwa watu wanaohitaji misaada, dunia hii itajaa upendo na furaha.
Idhaa ya kiswahili 2007-08-16
|