Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-14 16:15:08    
Umaalumu wa utamaduni wa kabila la wamongolia

cri

Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani uko kwenye sehemu ya mpakani, kaskazini mwa China. Huko kuna jangwa kubwa, maziwa na mabaki mengi ya kiutamaduni. Mkoa huo wa Mongolia ya ndani una makabila 49 yakiwemo ya wamongolia, wahan, wahui na waman, kati yake kabila la wamongolia lina idadi ya watu zaidi ya milioni 4. Watalii wanaotaka kushuhudia umaalumu wa utamaduni wa kabila la wamongolia, wasisahau kwenda kuangalia mbuga za majani, hususan mbuga maarufu za Xilinguole, Hulunbeier na Keerxin. Bw. Wang Yi kutoka Beijing alielezea matembezi yake kwenye mbuga ya majani.

"Mbuga ya majani ya Mongolia ya ndani ni nzuri ajabu, mazingira bora ya kimaumbile, nimepata kumbukumbu nyingi kuhusu wafugaji pamoja na maisha yao."

Kumbukumbu kubwa zaidi aliyoipata Bw. Wang Yi kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ni uzuri na ukarimu wa watu wa kabila la wamongolia. Ukiingia nyumbani kwa wafugaji, mama hufanya haraka kupika chai ya maziwa na nyama ya kondoo. Wakati wa kula chakula, mwenyeji huchukua bakuli ya fedha iliyojaa pombe ya maziwa kwa mikono miwili na kuwakaribisha wageni kwa pombe waliyoitengeneza wao wenyewe, huku akiimba wimbo wa kuwakaribisha wageni pombe, ambayo ni heshima kubwa ya watu wa kabila hilo kwa wageni.

Makundi makubwa ya kondoo wa rangi nyeupe, ng'ombe wa rangi manjano na ngamia wa rangi ya dhahabu wanakula majani kwenye mbuga kubwa isiyo upeo, kati yao yanaonekana mahema ya rangi nyeupe, hii ni picha halisi ya mbuga ya majani ya Mongolia ya ndani. Kwa wakazi wanaoishi mijini wanaona raha kubwa kuhusu mazingira na utamaduni wa kabila la Mongolia. Naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya mkoa wa Mongolia ya ndani Bw. Yun Taiping alisema,

"Kusafiri kutoka Beijing hadi mji wa Huhehaote ni dakika 45 kwa ndege, saa nne na nusu kwa gari kwenye barabara ya mwendo kasi na saa 11 kwa treni. Sasa hakuna matatizo kwenda kwenye mbuga ya majani, kule kuna mandhari nzuri sana, barabara zetu zinafikia kila mahali, tena mawasiliano ni rahisi sana."

Mbuga ya majani ya Gombaolage ya wilaya ya Xinlingele iko kwenye umbali wa saa tatu na kidogo kusafiri kwa gari kutoka Beijing, ambayo ni mbuga iliyo karibu zaidi na mji wa Beijing. Kabla ya miaka mia kadhaa iliyopita, mbuga ya majani ya Gombaolage ilikuwa mbuga ya kulisha farasi wa wafalme katika vizazi kadhaa vya enzi ya Qing, na pakuwa ni mahali pa kutoa farasi na nyama za ng'ombe na kondoo kwa wafalme pamoja na jamaa zao. Katika miaka ya hivi karibuni, utalii kwenye familia za wafugaji ulianza kwenye mbuga za Mongolia ya ndani, watalii wanaweza kulala kwenye nyumba za wafugaji. Mfugaji Qilindaoerji alijenga mahema matano ya kimongolia kwenye mbuga ya majani ya Gombaolage kwa ajili ya kupokea watalii. Bw. Qilindaoerji alisema, kila ifikapo majira ya joto, kunakuwa na watalii wengi wanaokwenda kutembelea mbuga za majani.

"Sehemu yetu hii ni mbuga nzuri, wageni wanaofika hapa wanaweza kwenda kukamua maziwa mbugani, au kutengeneza mtindi na chakula kinachotengenezwa kutokana na samli, licha ya hayo kuna nyama inayopikwa na kukaushwa kwa kuanikwa, vyakula hivyo ni vitamu vyenye lishe nyingi na havina vitu vyenye madhara kwa afya ya watu."

Wamongolia ni wakarimu sana. Kila wanapofika wageni nyumbani mwao, wenyeji huchinja kondoo, kupika nyama na kuwakaribisha pombe ya maziwa. Wafugaji wa Mongolia ya ndani wanapenda sana chakula kilichotengenezwa kwa maziwa, kama maziwa yaliyoganda, samli, mtindi na siagi pamoja na ndafu, ambayo ni chakula kizuri cha kuwakaribisha wageni wa heshima. Wageni hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa kutokuwa na uwezo wa kunywa pombe, kwani wanaweza kufanya kama wanavyofanya wamongolia, yaani kuchovya kidole cha pete kwenye pombe kisha kuirusha juu na chini, hii ina maana ya kutoa heshima kwa mbingu na ardhi, baada ya hapo wanaweza kunywa kidogo tu, basi inakuwa imetosha.

Anga la buluu, mawingu meupe, mbuga ya majani na makundi ya farasi, vitu hivyo siyo sura kamili ya umaalumu wa utamaduni wa kabila la wamongolia wanaoishi katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China.

Kwenye sehemu ya magharibi mwa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kuna mahali panapojulikana kwa jina la Alashan, mahali hapo ni sehemu ambayo Ngamia wanazaliwa kwa wingi, mbali na hayo kuna uwanda wa juu wa Eerduosi wenye jangwa kubwa lisilo na upeo. Kupanda kwenye ngamia na kutembea kwenye jangwa pia ni jambo la kufurahisha.

Kwa watu wanaotaka kufahamu vizuri utamaduni wa kabila la wamongolia wanaoishi kwenye mbuga ya majani, wasisahau kwenda kuangalia mila ya kutambika ya kabila la wamongolia. Kaburi la mfalme wa Chengjisi (neno hilo lina maana ya bahari kubwa katika lugha ya Kimongolia), ambaye ni shujaa wa kabila la wamongolia linalindwa vizazi vya watu wa tawi la Daerhute la kabila la wamongolia. Sherehe kubwa ya matambiko hufanyika katika majira ya mchipuko, majira ya joto, majira ya mpukutiko na majira ya baridi ya kila mwaka, na matambiko ya kawaida yanafanyika kila siku.

Tamasha kubwa la Nadamu linalofanyika kila mwaka kote mkoani humo, ni maonesho ya shughuli za utamaduni wa kijadi wa kabila la wamongolia. Neno la "nadamu" katika lugha ya Kimongolia ni "burudani", shughuli za tamasha hufanyika kila mwaka kwenye mbuga kubwa katika majira ya joto na majira ya mpukutiko. Wafugaji wa mbugani hukutana pamoja, kufanya michezo ya mbio za farasi, mieleka na kulenga shabaha kwa mishale, ambayo inahusika moja kwa moja na mila ya utamaduni wa mbugani wa kabila la wamongolia toka miaka mingi iliyopita.

Katika majira ya joto ya mwaka huu, sherehe kubwa itafanyika kuadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwa mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ambapo shughuli zaidi ya 70 kuhusu mila za utamaduni wa kikabila zitafanyika katika sehemu mbalimbali za mkoa huo kwa kuhusishwa na mapumziko ya likizo. Kuhusu shughuli hizo za sherehe, naibu mkurugenzi wa idara ya utalii ya mkoa wa Mongolia ya ndani Bw. Yun Daping alisema,

"Wakati huo kutakuwa na tamasha la nne la kimataifa la utamaduni wa mbuga ya Mongolia ya ndani, mashindano ya kwanza ya kwaya ya nyimbo za wafugaji wa mbugani nchini China, tamasha la 18 la Nadamu, maonesho ya mavazi ya kabila la wamongolia wa nchini China, siku ya sherehe ya maji matakatifu ya mlima wa Aer na maonesho ya mabaki ya kiutamaduni ya mlima mwekundu.