Maji taka yanayotolewa mijini yanaweza kutumiwa katika kuzalisha umeme baada ya kushughulikiwa, majivu yanaweza kutumiwa katika kutengeneza zege, utararibu kama huo wa kubana matumizi ya nishati na raslimali unatekelezwa katika shughuli mbalimbali katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, China. Mbali na hayo, mkoa huo pia umeeneza matumizi ya nishati isiyochafua mazingira kama vile gesi ya kinyesi na nishati ya upepo.
Katika mji wa Wuhai ulioko katikati mkoani Mongolia ya ndani kuna kampuni moja ya kuyashughulikia makaa ya mawe inayoitwa Shenhuawuhai. Zamani ushughulikiaji wa makaa ya mawe ulikuwa ni moja ya shughuli zinazoleta uchafuzi mwingi sana kwa mazingira, lakini hivi karibuni mwandishi wetu wa habari alipoingia kwenye eneo la kiwanda hicho, hakuona hali ya kujaa kwa moshi hewani kama ilivyokuwa kwenye viwanda hivyo hapo zamani. Mkurugenzi wa bodi ya kampuni hiyo Bw. Li Huaiguo alieleza kuwa, kampuni hiyo inatilia maanani hifadhi ya mazingira, na imeendelea kufanya utafiti kuhusu teknolojia ya kushughulikia takataka za makaa ya mawe na kuzitumia tena. Hivi sasa kampuni hiyo imepata njia yake ya kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira katika uzalishaji. Bw. Li Huaiguo alisema:
"zamani tulikuwa tunatupa takataka za makaa ya mawe, kitendo hicho kilikuwa kinaleta uchafuzi kwa mazingira. Hivi sasa tumejenga kiwanda cha kuzalisha umeme kwa kutumia takataka hizo, hata unga wa takataka hizo baada ya kuwaka zinatumiwa katika kutengeneza zege na matofali. Kwa maji taka yanayotolewa, tumejenga mfumo kamili wa kushughulikia maji hayo ili yaweze kutumiwa tena kwenye mzunguko wa uzalishaji, hivi sasa kiwanda chetu hakitoi maji taka hata kidogo."
Kutokana na kufuata utaratibu huo, kampuni ya Shenhuawuhai si kama tu imetimiza lengo la kubana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira, bali pia imehimiza ongezeko la kasi la kiuchumi.
Kutokana na kuwa na raslimali nyingi za nishati, mkoa wa Mongolia ya ndani umeanzisha shughuli mbalimbali zinazotegemea makaa ya mawe, chuma na chuma cha pua na umeme. Ingawa shughuli hizo zimesukuma mbele maendeleo ya mkoa huo, lakini pia zimekuwa shughuli zinazotumia nishati nyingi zaidi na zinazochafua mazingira vibaya zaidi mkoani humo. Katika miaka ya hivi karibuni, mkoa huo umeweka mkazo katika usimamizi wa viwanda hivyo ili kutimiza lengo la 'uzalishaji safi' wenye kubana matumizi ya nishati, kupunguza utoaji wa uchafuzi na kuongeza ufanisi wa uzalishaji. Hivi sasa makampuni yanayofuata njia hiyo kama kampuni ya Shenhuawuhai mkoani humo yamezidi mia moja.
Mbali na viwanda kutilia maanani shughuli hizo, wakazi wa kawaida wa mkoa huo pia wanazingatia kubana matumizi ya nishati na kupunguza uchafuzi wa mazingira katika maisha ya kila siku. Katika kijiji cha Lianfeng mjini Baotou, kila familia imechimba shimo la gesi ya kinyesi kwenye banda la nguruwe, kinyesi cha wanyama hakitupiliwi ovyo tena, bali kinatumiwa kwa kuzalisha gesi ya kinyesi na maji kwa ajili ya kupikia na kumwagilia shamba. Kutokana na kueneza matumizi ya gesi ya kinyesi, wanakijiji wa kijiji hicho hata wamebuni bidhaa mpya zinazotumia gesi hiyo. Mwanakijiji Bw. Zhang Jieping alifafanua kwa furaha vyombo alivyotenegeza, akisema:
"hili ni sufuria la kupikia wali linalotumia gesi ya kinyesi, lina uwezo unaofanana na lile la kawaida linalotumia umeme. Licha ya hilo, pia tuna tauri linalotumia gesi ya kinyesi, ambalo linasaidia kuongeza joto nyumbani katika majira ya baridi."
Mkoa wa Mongolia ya ndani ulioko kaskazini mwa China una raslimali nyingi za kimaumbile. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya sehemu zimeanza kutumia raslimali hizo kuendeleza nishati isiyoleta uchafuzi kwa mazingira. Shughuli za kuzalisha umeme kwa nguvu ya upepo zimeanza kuendelea kwenye sehemu za katikati mkoani humo. Mji wa Wulanchabu ni mmoja kati ya miji ya sehemu hiyo, na raslimali ya upepo kwenye mji huo inachukua asilimia 30 ya ile ya mkoa mzima. Katika miaka miwili iliyopita, mji huo umetunga mpango wa kwanza wa kisehemu wa kuendeleza nishati ya upepo nchini China, na kujenga kiwanda cha kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo chenye eneo la kilomita za mraba 6,828 mjini humo. Kwa kuwa mji wa Wulanchabu uko kilomita 336 tu kutoka Beijing, hivyo kiasi cha umeme uliozalishwa kwenye kiwanda hicho kinapelekwa moja kwa moja mjini Beijing. Na kwa kuwa Kiwanda hicho kitashiriki kwenye shughuli za utoaji wa umeme kwa ajili ya michezo ya Olimpiki mwaka 2008, kimetoa uungaji mkono imara kwa mpango wa Beijing kuandaa michezo ya Olimpiki yenye kuhifadhi mazingira'.
Katibu wa kamati ya chama cha kikomunisti cha mji huo Bw. Wu Yongxin alisema, kituo cha kuzalisha umeme cha magenge matatu ni kituo kikubwa kabisa cha kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji nchini China, na mji wa Wulanchabu umepanga kujenga "magenge matatu ya hewani" na kujenga kituo kikubwa kabisa cha kuzalisha umeme kwa nguvu ya upepo nchini China katika siku za baadaye. Bw. Wu Yongxin alisema:
'sehemu yetu ina upepo kila mahali, hasa kwenye sehemu ya Wulanbacha. Tunaweza kukuza shughuli za kuzalisha umeme kwa nishati ya upepo, tena tuko karibu na soko kubwa, umeme unaozalishwa hapa unaweza kupelekwa nje moja kwa moja. Kwa hivyo nadhani kujenga 'magenge matatu ya hewani" si ndoto tu."
Mbali na kuendeleza nishati isiyochafua mazingira, mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani pia umeweka mkazo katika kufunga na kurekebisha viwanda vinavyotumia nishati nyingi na kuleta uchafuzi mkubwa. Mji wa Wuhai ni mji wa viwanda wenye raslimali nyingi, kutokana na kuwepo kwa viwanda vingi kama hivyo mjini humo, zamani hata hewa mjini humo ilikuwa inaonekana ni ya rangi ya kijivu. Meya ya mji huo Bw. Bai Xiangqun alisema, ili kurejesha anga ya kibuluu kwa wakazi ya Wuhai, katika miaka 10 hivi iliyopita, mji huo umefunga na kurekebisha viwanda vidogo na vya wastani zaidi ya 60, na kuvisaidia viwanda vikubwa kuboresha vifaa vyao vya kushughulikia hali ya uchafuzi. Kutokana na juhudi za miaka 10, hivi sasa Mongolia ya ndani imefuata njia ya maendeleo endelevu inayobana matumizi ya nishati na kutoleta uchafuzi kwa mazingira.
|