Katika mkoa unaojiendesha wa kabila la wauygur wa Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, kuna jangwa kubwa la Takelamagan. Kwenye jangwa hilo kuna Mto Talimu, na kwenye mtiririko wake kuna maziwa madogo madogo na maeneo yenye majani. Tawi moja la kabila la wauygur wanaoishi kwenye eneo karibu na Ziwa Luobu la jangwa la Takelamagan wanaitwa waluobu. Waluobu wanaishi kwa kutegemea kazi ya kuvua samaki kwenye ziwa Luobu, na kuwa wavuvi wanaoishi kwenye jangwa.
Karquga ni kijiji kimoja cha waluobu, ambacho kina familia zisizofikia 100. Mzee Sdike Elinyatz mwenye umri wa miaka 104 mwaka huu alisema:
"Sisi tunaishi hapa kwa kutegekea kazi ya kuvua samaki kizazi baada ya kizazi, tulipokuwa watoto tulikuwa tunasuka nyavu kwa kutumia magamba ya katani ya Luobu, waluobu wametumia njia hiyo kusuka nyavu na kuvua samaki kwa miaka elfu kadhaa."
Katika miaka ya hivi karibuni, hali ya jangwa katika sehemu ya Ziwa Luobu imezidi kuwa mbaya, maji ya Mto Talimu umekuwa unapungua mwaka hadi mwaka, na eneo la Ziwa Luobu yamekuwa yanapungua siku hadi siku, hivyo baadhi ya waluobu wanapaswa kuacha kazi ya uvuvi na kujifunza kulima nafaka. Mkulima Amudong anajishughulisha na kilimo, lakini anadumisha maisha ya jadi ya uvuvi. Akisema:
"Maji ya Ziwa Luobu yamepungua kwa zaidi ya nusu kuliko yale yaliyokuwepo wakati nilipokuwa mtoto, na samaki wanaishi kwenye ziwa hilo sasa ni wachache sana. Hivi sasa maziwa mengi yanayotegemea Mto Talimu yamekauka, na bila maji hakutakuwa na samaki."
Waluobu wanaoishi kwenye kijiji cha Karquga wanafahamu kuwa, shughuli za uvuvi na kilimo peke yake haziwezi kuboresha maisha yao, wanatumai kubadilisha sura ya sehemu yao na kuboresha maisha yao kwa kuendeleza shughuli za utalii. Mwaka 2000 wanakijiji wa Karquga walianza kuendeleza shughuli za utalii, na kufanya maonesho ya vitu vinavyoonesha maisha ya jadi ya waluobu ili kuwavutia watalii. Waluobu wameanza kunufaika kutokana na kuendeleza shughuli za utalii. Mkulima Amudong alisema:
"Jambo linalonifurahisha ni kwamba, hivi sasa naweza kuuza samaki ninaowavua papo hapo. Zamani nilipaswa kuwauza katika sehemu yenye umbali wa kilomita 12 kutoka nyumbani, nilitumia siku mbili kamili kwenda na kurudi. Lakini hivi sasa barabara imejengwa, ninakwenda na kurudi kwa saa moja tu."
Maendeleo ya shughuli za utalii pia zimehimiza kustawi kwa michezo ya sanaa ya jadi ya huko, kama vile ngoma ya simba. Ngoma ya simba imekuwepo katika kijiji cha Karquga kwa miaka elfu moja, mzee Ason Sepi mwenye umri wa miaka 88 ni mtu pekee anayeweza kucheza ngoma hiyo kamili katika kijiji hicho. Alisimulia chimbuko cha ngoma ya simba akisema:
"Hapo zamani za kale, walikuwepo wafalme wawili ambao waliona simba kwa wakati mmoja katika jangwa la Takelamagan, mfalme mmoja alibuni ngoma ya simba, na kuwafundisha watumishi wake kucheza ngoma hiyo. Hilo ndio chimbuko la ngoma ya simba wanayocheza waluobu. Na ngoma ya simba inayochezwa na watu wa kabila la wahan ilibuniwa na mfalme mwingine.
Jambo linalomtia wasiwasi mzee Sepi ni kuwa, huenda siku moja ngoma ya simba itatoweka, hivyo alimfundisha mjukuu wake acheze ngoma ya simba alipokuwa na umri wa miaka minne tu. Hivi sasa mjukuu wake amejifunza ngoma hiyo kwa miaka mitano, na kutokana na kustawi kwa soko la utalii, ikiwa ni pamoja na utamaduni wa jadi wa kijiji cha Karquga, ngoma ya simba inapendwa na watalii, hivyo wanakijiji wanaojifunza kucheza ngoma hiyo wanaongezeka. Kuendeleza shughuli za utalii si kama tu kumewafahamisha waluobu umuhimu wa kukuza utamaduni wao wa jadi, pia kumeboresha hali yao ya maisha. Mzee Elinyatz alisema:
"Katika miaka mia moja iliyopita mimi siku zote niliishi katika jangwa hilo, sikuwahi kwenda sehemu nyingine. Mwaka jana nilienda Urumqi na Beijing. Nilikaa mjini Beijing kwa siku 12, nilitembelea ukuta mkuu, kasri la kale la wafalme na Jumba la mikutano ya umma. Siku zijazo nitaendelea kwenda nje kufanya utalii ili nijionee kwa macho yangu mwenyewe mambo yanayotokea nje ya jangwa.
Utalii umemburudisha mzee Elinyatz. Maisha bora, na moyo mwepesi umemfanya mzee huyo mwenye umri wa miaka zaidi ya mia moja aonekane bado mkakamavu. Mto Talimu ambao umekuwa unatiririka kwa miaka elfu kadhaa, umeunda eneo lenye majani kwenye jangwa waluobu wanakoishi, na kila mtu wa Luobu alikuwa anaishi kwa kufuata njia yake mwenyewe. Lakini hivi sasa Mto Talimu unakabiliwa na tatizo la kukauka, matumaini makubwa kabisa ya waluobu wa kijiji cha Karquga ni kuona maeneo yenye majani yanazidi kuongezeka katika maskani yao yaliyopo kwenye jangwa.
Idhaa ya kiswahili 2007-08-15
|