Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-16 16:26:20    
Motaboti zachangia kupunguza msongamano wa magari mjini Guangzhou, China

cri

Guangzhou ni mji mkuu wa jimbo la Guangdong, kusini mwa China. Mto Zhujiang unapita kwenye mji huo ambao unaugawa mji huo katika sehemu tatu. Ili kupunguza msongamano wa magari barabarani, usafiri wa motaboti ulianzishwa kwenye mto Zhujiang mwezi Aprili mwaka huu, kuchukua nafasi ya vivuko vikongwe. Hivi sasa motaboti, mabasi na subway zimekuwa ni mtandao wa kisasa wa mawasiliano ya mji wa Guangzhou.

Tarehe 10 Aprili asubuhi, motaboti ya kwanza iliyokuwa imebeba abiria makumi kadhaa iliondoka kutoka kituo kilichopo kando ya kusini mwa mto Zhujiang, na kufika kwenye kituo cha mwisho ndani ya dakika 30 baada ya kusimama kwenye vituo viwili njiani. Lakini safari hiyo hiyo inaweza kuchukua zaidi ya dakika 50 kwa mabasi.

Kuanzishwa kwa usafiri wa motaboti kulifuatiliwa na wakazi wa mji wa Guangzhou, na kuwafurahisha sana. Hivi sasa wakazi wengi wa huko wanasafiri kwa motaboti zinazojulikana kama "mabasi ya majini". Mkazi mmoja Bibi Li Li alisema (sauti 1), "Sasa inaokoa muda. Naona inasaidia sana, kwani hakuna msomganamo wa magari, hii ni njia rahisi ya kwenda kazini na kurudi nyumbani."

Hivi sasa motaboti zimechukua nafasi ya vivuko ambavyo vilikuwepo mjini Guangzhou kwa miaka zaidi ya 100. Mwanzoni mwa miaka ya 1980, mjini humo kulikuwa na madaraja kadhaa tu yaliyounganisha kando mbili za mto Zhujiang, kwa hiyo wakazi wa huko walipenda kupanda vivuko ili kuvuka mto huo.

Mama Lai Jianfen mwenye umri wa miaka 49 alikuwa kondakta kwenye kituo cha vivuko wakati huo. Yeye alielezea pilikapilika alizoshuhudia siku zilizopita. Alisema (sauti 2) "Nimefanya kazi katika kampuni hiyo kwa miaka 27. Zamani nilipoanza kazi, kulikuwa na pilikapilika nyingi, wakati huo ujenzi wa barabara iliyo chini ya mto Zhujiang ulikuwa haujaanza. Kazi yangu ilikuwa kuuza tiketi, ambapo watu wengi walikuwa wanapanga mistari wakisubiri kununua tiketi, hali ambayo ilinifanya nishindwe hata kupata nafasi ya kula chakula."

Wakati huo kampuni ya vivuko ilikuwa inawahudumia abiria laki moja hivi kwa siku, idadi ambayo ilichukua asilimia 14 ya abiria waliosafiri mjini Guangzhou. Mfanyakazi mwingine wa kampuni ya vivuko Bw. Deng Xianyao alikumbusha hali ya kustawi kwa huduma za vivuko kwa wakati huo, alisema (sauti 3) "Wakati huo kivuko kilikuwa ni chombo muhimu cha mawasiliano hapa Guangzhou. Nakumbuka kwenye njia moja yenye pilikapilika zaidi ya usafiri, meli kubwa 5 hadi 6 zilikuwa zinatoa huduma, na kila meli ilikuwa na uwezo wa kubeba abiria kati ya 800 na 1,000. Mwaka mmoja idadi ya abiria iliwahi kuzidi milioni 100."

Kwenye kumbukumbu za wakazi wa Guangzhou, vivuko vilikuwa muhimu sana kwenye maisha yao ya kila siku.

Lakini hali hii ilianza kubadilika. Tokea mwaka 1993, kutokana na ujenzi wa madaraja mengine, barabara iliyo chini ya mto Zhujiang na barabara mpya, idadi ya abiria waliokuwa wanapanda vivuko ilianza kupungua kwa wastani wa asilimia 10 hadi 20 kila mwaka. Hali hiyo iliwatia watu wasiwasi kwamba, je usafiri wa vivuko kwenye mto Zhujiang utaachwa kabisa huko Guangzhou?

Katika miaka ya hivi karibuni, ongezeko la kasi la magari limeleta tatizo la msongamano barabarani. Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali ya mji wa Guangzhou iliamua kuendeleza usafiri wa majini. Mpango wa serikali ulipata uungaji mkono wa wakazi wa mji huo. Mwaka 2006 wajumbe kadhaa wa bunge la umma la mji wa Guangzhou wakishirikiana walitoa pendekezo la kuanzisha usafiri wa motaboti kwenye mto Zhujiang, ili kupunguza shinikizo kubwa kwenye mawasiliano.

Bw. Sun Shisheng ni mmoja wa wabunge, alisema (sauti 4) "Naona hapa Guangzhou, kuna mtandao wa mito ambao tunatakiwa kuutumia ipasavyo na kuifanya iwe sehemu ya mawasiliano ya umma. Ndiyo maana inafaa kuanzisha usafiri wa motaboti mjini Guangzhou, ili kupunguza shinikizo kwenye mawasiliano ya umma."

Hivi sasa njia za usafiri wa motaboti bado ni chache, hata hivyo serikali ya mji wa Guangzhou ina mpango wake, kwamba hadi ifikapo mwaka 2020, vituo vya motaboti vitaongezeka na kufikia 65 kutoka 28 vya hivi sasa.

Pamoja na aina ya chombo cha mawasiliano ya umma, usafiri wa motaboti mjini Guangzhou pia unaweza kutumika kwa ajili ya shughuli za utalii, kwani abiria wanaweza kuburudishwa na mandhari ya kupendeza ya mji huo wakisafiri kwa motaboti.

Meneja mkuu wa kampuni ya mawasiliano ya meli za abiria ya mji wa Guangzhou Bw. Yu Haoran alitoa maoni yake, akisema, (sauti 5) "Ni jambo la kufurahisha watu tukisafiri kwa motaboti huku tukiburudishwa na mandhari nzuri ya kando mbili za mto. Pia kuna wakazi ambao wanataka kuanzisha motaboti za utalii. Katika siku za baadaye tutaweza kuweka maeneo mawili tofauti kwenye motaboti moja, yaani ghorofa ya juu kwa ajili ya watalii na ghorofa ya kwanza kwa ajili ya abiria wa kawaida, pia tutauza tiketi za aina mbili."

Kutokana na kustawi na kudidimia kwa usafiri wa vivuko pamoja na kuanzishwa kwa usafiri wa motaboti kwenye mto Zhujiang, tunaweza kujionea jinsi sekta ya mawasiliano ya umma mjini Guangzhou ilivyokua sambamba na maendeleo ya mji huo.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-16