Michezo ya Olimpiki inayovutia kote duniani itafanyika mwezi Agosti mwaka kesho. Upigaji wa filamu ya kiserikali ya michezo hiyo umezinduliwa? na kuanzia mwezi Machi mwaka kesho filamu hiyo itaingia katika kipindi halisi cha upigaji wake.
Mliosikia ni sauti ya filamu ya kiserikali ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 1992 ya Barcelona, Hispania wakati mashindano ya mbio za Marathon yakifanyika.
Tokea mwaka 1912 filamu ya kwanza ya michezo ya Olimpiki ya Stockholm ilipopigwa na serikali ya Sweden, kila michezo ya Olimpiki inapofanyika huwa kunakuwa na filamu yake ya kiserikali, na hii imekuwa sehemu muhimu ya kazi za kamati ya maandalizi ya michezo hiyo. Jukumu la filamu ya kiserikali ni kurekodi hali ilivyo ya michezo ya Olimpiki kwa pande zote, kuonesha mashindano yanayosisimua na kutoa maelezo kuhusu wachezaji, filamu hiyo itakuwa kumbukumbu adimu katika historia ya michezo ya Olimpiki.
Filamu ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 Beijing ni filamu ya 22 ya kiserikali. Hivi sasa kikundi cha kupiga filamu hiyo kimeundwa, mwongozaji wa filamu hiyo ni Bi. Gu Jun, ambaye pia ni mwongozaji wa Kiwanda cha serikali kuu cha kutengeneza filamu za habari. Alipozungumzia filamu ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008, Bi. Gu Ju aliasema,
"Filamu hiyo ni tofauti na filamu nyingine za nyaraka, kwanza inawakilisha Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki, pili inawakilisha Kamati ya Maandalizi ya Michezo ya Olimpiki ya mji unaoandaa michezo hiyo, na tatu inawakilisha mji wenyewe. kwa hiyo nafasi iliyobaki ya kumruhusu mwongozaji apige kwa mtazamo wake ni ndogo sana. Tofauti kubwa na filamu nyingine ni kuwa filamu ya kiserikali inaonesha msimamo wa serikali."
Bi. Gu Jun alisema filamu hiyo ya kiserikali itachanganya utamaduni wa Kimashariki, na itakuwa na maandalizi ya makini kuhusu mtindo wa filamu hiyo na uchaguzi wa hadithi. Imefahamika kuwa filamu ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 itaonesha mada ya michezo hiyo ya "dunia moja na ndoto moja" kwa kupitia harakati za kukimbiza mwenge, ufunguzi, hali ya maandalizi ya wachezaji wa nchi mbalimbali na rekodi zao kwenye mashindano ya michezo hiyo, ili kuenzi moyo wa michezo ya Olimpiki na kuonesha jinsi watu wote duniani wanavyotamani amani.
Kutokana na mpango, mwezi Machi mwaka kesho kikundi cha kupiga filamu hiyo kitagawanyika na kwenda kwenye mabara matano kupiga filamu kuhusu wachezaji wa michezo ya aina sita kwa lengo la kuonesha jinsi wachezaji wa nchi mbalimbli wanavyojianda na maelezo yao kuhusu kushiriki kwenye michezo hiyo. Mtengenezaji wa filamu hiyo Bw. Wu Qi alisema, filamu hiyo itasisitiza kuonesha tumaini kubwa la watu kuhusu dunia yenye masikilizano. Alisema,
"Masikilizano sio neno tupu bali linamaanisha uvumilivu kwa vitu tofauti, moyo wa michezo ya Olimpiki unamaanisha uvumilivu mkubwa, pengine baada ya kurudi nyumbani wachezaji wanaendelea kuvaa mavazi yao na kukabiliwa na mapambano ya kisilaha, lakini kwenye viwanja wachezaji hao wako katika hali ya amani na kushindana. Hatutaficha tofauti ya kisiasa na kiutamaduni katika maisha yao, badala yake kwa kiasi fulani tutaonesha tofauti hiyo, kwa hiyo tutakwenda Mashariki ya Kati kupiga filamu ingawa huko sio salama ili kuwafanya watu watafakari kwamba ingawa michezo ya Olimpiki imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 100 lakini leo hii bado inakabiliwa na jukumu lake."
Kuhusu filamu hiyo namna ya kuonesha utamaduni wa mwenyeji China, Bw. Wu Qi alisema, kutokana na kuwa filamu hiyo ni ya kiserikali, haiwezi kuachana na mashindano ya michezo, utamaduni wa China utaoneshwa kwa muziki, na sehemu za mwanzo wa filamu hiyo na ufundi wa upigaji. Pamoja na hayo alisema filamu hiyo haitaonesha zaidi wachezaji wa China kuliko wachezaji wa nchi nyingine kwa sababu tu China ni mwenyeji wa kufanya michezo hiyo.
Kamati ya Kimataifa ya Michezo ya Olimpiki na Kamati ya Maandalizi ya michezo hiyo ya Beijing zimeweka matumaini makubwa kwa filamu hiyo. Mwongozaji mashuhuri wa filamu za michezo Bw. Bud Greenspan ni mshauri wa upigaji wa filamu hiyo.
Baada ya Beijing kupata nafasi ya kuwa mwenyeji wa kuandaa michezo ya Olimpiki mwaka 2001, Kiwanda cha serikali kuu cha kutengeneza filamu na habari kimeanza kupiga filamu iitwayo "Miaka Saba baada ya Mwaka 2001". Filamu hiyo imerekodi hali yote ya maandalizi ya michezo hiyo, na hivi sasa iko katika kipindi chake cha mwisho, filamu hiyo itaoneshwa kote nchini China mwezi Julai mwaka 2008.
Filamu hiyo imerekodi hali inavyokuwa ya ujenzi wa majumba na viwanja vya michezo, maandalizi ya wachezaji, watu wanaojitolea kutoa huduma na kazi ya ulinzi. Mwongozaji wa filamu hiyo Bi. Gu Jun alisema,
"Kuandaa michezo ya Olimpiki kunahitaji mambo matatu muhimu: majumba na viwanja, wachezaji na usalama. Kwa hiyo filamu yetu ya "Miaka Saba baada ya Mwaka 2001" inapigwa kwa kufuata mtizamo huo." Filamu hiyo imeonesha mada ya "dunia moja na ndoto moja" kupitia ujenzi wa jengo moja, familia moja, njia moja ya mbio uwanjani, kundi moja la wachezaji na kundi moja la walinzi."
Idhaa ya kiswahili 2007-08-20
|