Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-22 16:24:56    
Wachangjiao ambao ni tawi moja la kabila la wamiao waishio mkoani Guizhou nchini China

cri

Katika kitongoji cha Suoga cha mkoa wa Guizhou, kusini magharibi mwa China, wanaishi wachangjiao, ambao ni tawi moja ya kabila la wamiao. Tawi hilo lina idadi ya watu zaidi ya 4000, ambao wanaishi kwenye milima mirefu na yenye hali ya hewa ya baridi. Watu hao wanasemekana bado wanaishi maisha ya kiasili.

Waandishi wetu wa habari walipofika katika kijiji cha Longga katika kitongoji cha Suoga walikaribishwa kwa ukarimu mkubwa na wasichana na wavulana wa huko waliovaa mavazi maridadi wakishika vikombe vya pembe za ng'ombe mkononi, huku wakiimba wimbo wa kutakiana heri na baraka. Kwa mujibu wa desturi za huko, wageni wanapaswa kunywa vikombe vitatu vya pombe kabla ya kuingia kijijini.

Umaalumu wa kipekee wa wachangjiao ni kwamba, wanawake wanafunga nywele zao ndefu kwenye pembe ndefu za mbao na kuliweka fundo kubwa la nywele utosini wakaonekana kama wana pembe kichwani. Hivyo ndivyo watu hao wamiao walivyojulikana kwa jina la "Changjiao", maana yake ya kichina ni "pembe ndefu." Bwana Mou Huixu ambaye alikuwa amefanya utafiti mwingi kuhusu historia na utamaduni wa tawi la "Changjiao" la kabila la wamiao alisema:

"Kuna usemi wa aina mbili kuhusu historia ya wachangjiao. Usemi mmoja ni kuwa, watu hao walitegemea sana ng'ombe katika uzalishaji wa kilimo, pembe ya ng'ombe ni kama ishara ya mungu kwao. Na usemi mwingine ni kuwa, siku zamani wachangjiao waliishi kwa kutegemea kuwinda wanyama wenye pembe kama vile paa. Walifunga pembe kichwani kwa umaalumu ili kuchafusha akili za wanyama."

Bi. Xiong Jizai alisema, wanawake wanapofunga nywele zao, huzikusanya nywele katika wakati wa kuchana na huzisuka kwa nyuzi za katani, na huzichukua kama zawadi kwa mabinti zao wanapoolewa. Kurithi kizazi hadi kizazi, nywele za wanawake wa kabila la wamiao huzidi kuongezeka.

"Fundo la nywele ni umaalumu wetu, wanawake wazee huvaa nywele zao hata wanapofanya kazi shambani."

Katika kijiji cha Longga nyumba zote zinaezekwa na majani?na paa lenye mwinuko mkali linafaa kwa mvua kutiririka chini ili kufanya majani yasiozwe haraka. Chini ya upenu wa paa la nyumba zao, wasichana waliovaa mavazi maridadi ya kabila wachangjiao wanajishughulisha na kuweka michoro ya aina mbalimbali kwenye vitambaa vya pamba kwa kutumia rangi za mimea. Msichana Wang Jiaying alisema, wanawake wote wachangjiao wa kabila la wamiao ni hodari kuweka michoro kwenye vitambaa, hawana haja ya kufuata mifano maalum, wanabuni michoro kwa wanavyopenda. Alisema:

"Nilipokuwa mtoto mdogo nilifundishwa namna ya kuweka michoro kwenye vitambaa vya nguo. Hii ni hatua ya kwanza ya kushona nguo. Pia nimejifunza kutarizi. Inachukua muda wa mwezi mzima kwa sisi kushona nguo moja."

Ufumaji na utarizi ni masomo ya lazima kwa wanawake wachangjiao wa kabila la wamiao. Mliosikia sasa hivi ni milio ya kufuma vitambaa katika kijiji cha Longga.

Mwaka 1998 ili kuhifadhi na kurithisha vizuri zaidi utamaduni wenye umaalum wa wachangjiao wa kabila la wamiao, China na Norway zilishirikiana kujenga jumba la maonesho ya hali halisi ya maisha ya wachangjiao wa kijiji cha Longga. Mkuu wa jumba hilo Bwana Mou Huixu alieleza kuwa, jumba hilo lina eneo la kilomita za mraba 120, licha ya kuonesha na kuhifadhi maskani, mavazi, ala za muziki na vifaa vya uzalishaji vya wachangjiao wa kabila la wamiao, jumba hilo pia limehifadhi mila na utamaduni wa kabila hilo kama vile sherehe za ndoa, mazishi na matandiko ya kidini kwa njia ya kunasa sauti, kupiga video na kuandika maandishi.

"Kutokana na maendeleo ya binadamu na jamii, utamaduni wa makabila mbalimbali unaingilizana na kuathiriana, baadhi ya vitu vya utamaduni fulani vitatoweka katika mchakato huo, kama vile lugha, mila na desturi. Hivyo jumba hilo la maonesho linaweka mkazo katika kuhifadhi utamaduni wa asili wa kikabila, ili kuokoa vitu vinavyokaribu kutoweka."

Jua lilipotua magharibi, kusindikizwa kwa wimbo wa kabila la wamiao wa "Changjiao", waandishi wetu wa habari walipanda gari katika kijiji cha Longga kilichowavutia sana.

Idhaa ya kiswahili 2007-08-22