Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-23 17:32:41    
Chongqing: Mji uliojengwa mlimani

cri

Chongqing ni mji unaowavutia watu kati ya miji iliyopo kusini magharibi mwa China. Mji huo unajulikana kama mji wa mlima au mji wa mito kutokana na kwamba ulijengwa mlimani na kuzungukwa na mito miwili.

Mliosikia ni wimbo ulioimbwa na watu waliokuwa wanavuta meli kwa kutumia kamba kwenye kando ya mto Changjiang. Sauti hizo zilirekodiwa mwaka 1911 na balozi mdogo wa Ujerumani mjini Chongqing Bw. Fritz Wyss, alipokwenda Chongqing kutoka Wuhan, akipanda meli na kupita kwenye sehemu ambayo inajulikana kama magenge matatu ya mto Changjiang. Katika sehemu hiyo, maji ya mto yanakwenda kwa kasi kwenye mabonde membamba, kutokana na kuwepo kwa miamba mingi mtoni, wakati huo katika sehemu fulani walikuwepo watu waliofanya kazi ya kuvuta meli kwa kutumia kamba. Hiyo ilikuwa kazi ngumu sana, ili kupiga hatua kwa wakati mmoja na kujitia moyo, watu hao waliimba wimbo maalumu kazini.

Mto Changjiang wenye urefu wa kilomita 6,300 unapita China kutoka sehemu ya magharibi kwenda sehemu ya mashariki, unajulikana kuwa ni njia ya maji yenye dhahabu. Mji wa Chongqing upo katika mtiririko wa juu wa mto huo, ni kituo kikubwa kabisa cha biashara katika sehemu ya kusini magharibi mwa China.

Lakini mji huo ulianza kufuatiliwa na walimwengu tangu vita vya pili vya dunia. Mwaka 1937 mji wa Nanjing ambao ulikuwa mji mkuu wa China wakati huo ulitekwa na jeshi la Japani, serikali ya China ilihamia kwenye mji wa Chongqing, katika miaka minane iliyofuata Chongqing ulikuwa ni mji mkuu wa kipindi cha vita hadi kufikia mwaka 1945 China ilipopata ushindi kwenye vita dhidi ya uvamizi wa Japan.

Kutokana na uhamiaji huo, viwanda vingi, mashirika, shule na wanautamaduni mashuhuri wa China pia walihamia Chongqing. Meya wa sasa wa mji wa Chongqing Bw. Wang Hongju aliona kuwa uhamiaji huo uliiletea Chongqing fursa ya maendeleo kwa mara ya kwanza.

Anasema "Katika kipindi cha kupambana na uvamizi wa Japan, viwanda vilivyotangulia kuanzishwa nchini China vilihamishwa huko Chongqing vikiambatana na serikali ya wakati huo. Viwanda hivyo vilikuwa zaidi ya 2,500."

Mwaka 1949 Jamhuri ya watu wa China iliasisiwa, ambapo Chongqing iliamuliwa kuwa moja ya vituo vya viwanda, kwa hiyo viwanda vingi zaidi vilihamishwa huko. Mwaka 1997 serikali ya China iliufanya mji wa Chongqing kuwa mji unaosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu, hadhi ya mji huo inalingana na mkoa. Hivi sasa nchini China kuna miji minne inayosimamiwa moja kwa moja na serikali kuu. Pamoja na Chongqing, ni Beijing, Shanghai na Tianjin. Na Chongqing ni mji pekee uliopo sehemu ya magharibi mwa China kati yao.

Mkurugenzi wa kamati ya maendeleo na mageuzi ya Chongqing Bw. Yang Qingyu alisema, serikali ya China iliupa mji wa Chongqing kazi muhimu katika mambo manne, yaani kuhamisha watu, kuwasaidia watu wenye matatizo ya kiuchumi kujiendeleza, kuboresha kituo kikongwe cha viwanda, na kuhifadhi mazingira.

Anasema "Ni dhahiri kuwa, sababu ya moja kwa moja ni ujenzi wa mradi wa magenge matatu, na watu zaidi ya milioni moja walihamishwa kutokana na mradi huo. Tukiangalia ujenzi wa miradi mikubwa ya maboma nchini China na nje ya China katika miaka mia kadhaa iliyopita, suala kubwa si ujenzi wenyewe, bali ni suala la kuwahamisha watu. Serikali ya China inatilia maanani sana watu wanaohamishwa, kwa hiyo iliamua kuinua hadhi ya mji wa Chongqing ili ushughulikie moja kwa moja uhamiaji wa watu zaidi ya milioni moja."

Hadi hivi sasa mradi wa magenge matatu ni mradi mkubwa kabisa wa maji duniani. Maboma ya mradi huo yapo mjini Yichang, mkoani Hubei, lakini bwawa lake lipo ndani ya mji wa Chongqing. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana, kwa jumla watu wapatao milioni 1.03 walikuwa wamehamishwa kutoka kwenye eneo la bwawa la mradi huo na kupata nyumba mpya. Kiwango cha maji kwenye bwawa hilo kilifikia mita 156 mwezi Oktoba mwaka jana, na meli kubwa sasa zinaweza kusafiri mpaka kwenye bandari ya Chongqing.

Hivi sasa mji wa Chongqing una eneo la kilomita elfu 82.4 za mraba na watu milioni 32. Meya wa mji huo Bw. Wang Hongju aliona, pamoja na msingi wa viwanda uliokuwepo, mji huo una sifa nzuri ya kijiogrofia inayowavutia wawekezaji wengi. Kwani nchini China mji wa Chongqing upo kwenye makutano ya sehemu ya magharibi yenye maliasili nyingi na sehemu ya mashariki iliyoendelezwa kiuchumi. Mbali na hayo sekta ya mawasiliano ya Chongqing imeendelezwa sana. Pamoja na kuwa na mawasiliano reli, barabara za mwendo kasi na ndege, Chongqing iko kando ya mto Changjiang, ambao unajulikana kama njia ya maji yenye dhahabu kutokana na gharama nafuu za mawasiliano ya meli.

Watu wanasema Chongqing wa miaka 10 au 20 iliyopita, ulikuwa mji wa wilaya, lakini hivi sasa umekuwa mji mkubwa wenye mvutano. Mji huo unavutia uwekezaji na kuwavutia watu wenye ujuzi. Bw. Liu Lang ni msanii aliyehamia Chongqing miaka kadhaa iliyopita. Amewahi kutembelea miji mbalimbali ya China, na hatimaye akaamua kuishi huko Chongqing.

Bwana huyo anasema, "Nilitembelea sehemu mbalimbali, napenda kabisa mji wa Chongqing. Huu ni mji wenye umaalumu, naona uko tofauti na miji mingine. Hapa kuna mazingira yanayofaa kuishi, kuna milima na maji. Wageni wengi wanaofika Chongqing, wanaupenda mji huo, ambao una maendeleo ya kasi, vitega uchumi vingi, wafanyabiashara wanaweza kupata faida hapa, na wasanii pia wanaweza kupata mazingira mazuri ya kufanya shughuli za usanii. Kila mmoja anaweza kupata anachotaka hapa Chongqing."

Idhaa ya kiswahili 2007-08-23