Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-28 15:05:07    
Mazao ya kilimo ya Taiwan yaendelea kuingia kwenye soko la China bara

cri

Mwishoni mwa mwezi Julai, maonesho ya mazao ya kilimo ya Taiwan yenye sifa nzuri ya mwaka 2007 ambayo yaliandaliwa na shirikisho la mawasiliano ya kilimo kati ya China bara na Taiwan na shirikisho la kilimo la Taiwan yalifanyika kwenye miji mingi ya China bara. Maonesho hayo yameyasaidia mazao ya kilimo ya Taiwan yenye sifa nzuri yakubalike zaidi kwa wakazi wa China bara, na kusukuma mbele mawasiliano na ushirikiano kati ya pande mbili kwenye sekta ya kilimo.

Maonesho ya mazao ya kilimo ya Taiwan yenye sifa nzuri ya mwaka 2007 yalifanyika kuanzia tarehe 20 hadi tarehe 25 mwezi Julai kwenye miji ya Shanghai, Nanjing, Fuzhou, Wuhan, Guangzhou na Dalian. Shirikisho la kilimo la Taiwan, mashirikisho ya kilimo ya wilaya na vijiji mbalimbali na makampuni ya mazao ya Taiwan yalishiriki kwenye maonesho hayo.

Wengi wa washiriki kutoka Taiwan, hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuja China. Kupitia maonesho hayo walipata fursa ya kukutana na wateja wa China bara ana kwa ana, na walifahamu zaidi soko la China bara. Bw. Chen Zhiwei kutoka wilaya ya Nantou alimwambia mwandishi wa habari kuwa, sawa na wafanyakazi wengine wa makampuni ya mazao ya kilimo ya Taiwan waliokuja China bara kwa mara ya kwanza, anatumai pia ataweza kukutana na wafanyabiashara wengi zaidi wa China bara mjini Shanghai, na kupanua soko la mazao ya kampuni yake katika China bara. Alisema,

"Tumekuja hapa kutafuta fursa za kibiashara, ili tuweze kushirikiana na makampuni ya China bara."

Kwenye maonesho hayo mwandishi wa habari aliona aina mbalimbali za matunda na mboga, na zaidi ya aina 400 za mazao ya kilimo yaliyotengenezwa tena ukiwemo mchele, chai, mazao ya baharini na mazao yaliyotengenezwa kwa maharagwe. Maembe mekundu, mananasi ya kijani na majano, ndizi kubwa na mapapai matamu yanapendwa na wakazi wa China bara waliotembelea maonesho hayo.

Kwenye maonesho yaliyofanyika mjini Dalian, watu wengi walionja matunda yaliyozalishwa kisiwani Taiwan. Mwanafunzi wa darasa la nne la shule ya msingi Gengzhi alionja mapera kwenye maonesho hayo. Alisema,

"Nafikiri matunda ya aina hiyo ni ya ajabu, sijawahi kuyaona. Niliwahi kusikia darasani kuwa mapera ni matunda matamu sana."

Ushirikiano kati ya China bara na Taiwan katika mambo ya kilimo una uwezo mkubwa wa kupata maendeleo. Tangu China bara itunge sera kadhaa za kilimo zinazoinufaisha Taiwan mwaka 2005, mazao ya kilimo ya Taiwan yenye sifa nzuri yanakubalika zaidi kwa wateja wa China bara. Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2006 China bara iliingiza tani 3500 za matunda kutoka Taiwan bila ya kutoza ushuru. Thamani ya biashara ya matunda hayo ilikuwa zaidi ya dola za kimarekani milioni 4, ambayo iliongezeka kwa kiasi kikubwa kuliko mwaka 2005. Mwanzoni mwa 2007, China bara ilitangaza sera 20 mpya za kilimo zinazoinufaisha Taiwan. Mazao ya kilimo ya Taiwan yameingia kwenye soko la China bara muda mfupi uliopita, hivyo wakazi wengi wa China bara bado hawajui mengi kuhusu mazao ya kilimo ya Taiwan.

Katibu mkuu wa shirikisho la kilimo la Taiwan Bw. Zhang Yongcheng alisema, maonesho hayo yataongeza umaarufu wa mazao ya kilimo ya Taiwan katika China bara, na uuzaji wa mazao ya kilimo ya Taiwan kwa China bara utakuwa ni jambo la kawaida. Bw. Zhang alisema,

"Maonesho hayo yatawasaidia wakazi wa China bara wajue mazao ya kilimo ya Taiwan yenye sifa nzuri. Tunatumai kuwa maonesho hayo yataendelea, na wakazi wa China bara watatembelea maonesho hayo na kusikiliza maelezo ya wakulima wa Taiwan kuhusu mazao yao."

Bw. Zhang Yongcheng alisema wakulima wa Taiwan wana matumaini kuwa uuzaji wa mazao ya kilimo ya Taiwan katika China bara utakuwa ni jambo la kawaida. Hivi sasa njia ya kawaida ya uuzaji wa mazao ya kilimo ya Taiwan katika China bara inaanzishwa hatua kwa hatua, baadaye bei za mazao ya kilimo ya Taiwan zitapungua. Bw. Zhang anaona kuwa kutimiza mawasiliano ya moja kwa moja ya biashara, posta na usafiri kati ya China bara na Taiwan mapema kadri iwezekanavyo, kuongeza mazao ya kilimo yaliyotengenezwa kwa kina, na pande mbili kufanya juhudi pamoja kuanzisha mfumo wa uuzaji wa mazao ya kilimo ya Taiwan kwa China bara ni hatua zinazoweza kutekelezwa.

Ofisa wa wizara ya kilimo ya China alisema, Taiwan ina aina nzuri za mazao ya kilimo, teknolojia ya kisasa ya kilimo, uzoefu wa usimamizi na soko la mazao ya kilimo linalofungua mlango; na China bara ina maliasili nyingi, miundo mbinu iliyokamilika na hali tulivu ya uchumi, mambo hayo ni msingi wa kuendeleza mawasiliano na ushirikiano kati ya China bara na Taiwan katika mambo ya kilimo. Kuimarisha ushirikiano katika mambo ya kilimo kunaweza kusukuma mbele pande mbili zirekebishe miundo ya kilimo, kunufaishana, kusaidiana na kupata maendeleo kwa pamoja.

Benki ya uagizaji na uuzaji wa bidhaa nje ya China ni idara ya kipekee iliyosaidia kuandaa maonesho hayo. Katika miaka mingi iliyopita, benki hiyo ilifanya juhudi kutoa msaada kwa ushirikiano kati ya makampuni ya China bara na Taiwan, na imetoa mchango mkubwa kwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China bara na Taiwan. Katika miaka miwili iliyopita, benki hiyo ikifuata sera mbalimbali za kilimo zinazoinufaisha Taiwan, ilitoa uungaji mkono kwa uwekezaji wa wafanyabiashara wa Taiwan katika China bara.

Mfanyakazi wa benki hiyo Bw. Li Jun alisema benki hiyo itaendelea kutoa huduma kwa makampuni na wafanyabiashara wa Taiwan wanaoshughulikia uzalishaji wa mazao ya kilimo. Bw. Li alisema,

"Benki yetu itaendelea kutoa uungaji mkono wa kifedha kwa mashirikisho, makampuni na masoko ya mazao ya kilimo ya Taiwan."

Idhaa ya kiswahili 2007-08-28