Xian ni mji mkuu wa mkoa wa Shanxi, uliopo kaskazini magharibi mwa China, ambao ni mji mkongwe maarufu, pia ni sehemu ya kwanza walipoishi Waislamu wa China. Mjini Xian, kuna mtaa wenye historia ndefu sana wa watu wa kabila la Wahui, ambao ni Waislamu. Katika miaka ya karibuni, ili kuhifadhi mabaki ya kale katika mtaa huo wa watu wa kabila la Wahui, na pia kuwaandalia mazingira mazuri ya kuishi na kufanya shughuli za kidini, serikali ya China imefanya megni katika uhifadhi na uboreshwaji wa mataa huo.
Mtaa wa Wahui upo katika sehemu ya magharibi ya mji wa Xian. Tokea karne ya 10, watu wa kabila la Wahui walianza kujikusanya na kuishi mjini Xian. Hivi sasa, mtaa huo una eneo la hekta zaidi ya 50 lenye wakazi wapatao elfu 60, na miongoni mwao, theluthi moja ni Wahui.
Mtaa huo upo ndani ya mji wa Xian. Kutokana na manedeleo ya mji huo, katika miaka ya karibuni, makazi mengi ya mtaa huo yamebomolewa, na yale yanayobaki ni machache yenye mtindo wa kijadi. Lakini hali ya makazi hayo ni mbaya sana. Licha ya hayo, miundo mbinu ya mtaa huo, mfano wa barabara, mabomba ya ugavi wa maji na mifereji ya uchafu, imepitwa na wakati, hali ambayo imeleta matatizo kwa maisha ya wakazi wa huko.
Mwaka 1998, serikali ya China ilianza juhudi za kuboresha mazingira ya huko, na kazi hiyo kwanza ilifanyika katika eneo la hekta 16 la katikati ya mtaa huo.
Katika kazi hiyo, China pia ilitafuta ushirikiano wa kimataifa, ambapo serikali ya Norway ilitoa misaada ya Yuan za Renminbi milioni 5, sawa na dola za kimarekani laki 6 na elfu 20, pamaoj na mafundi wake kushiriki kwenye ukarabati wa majengo.
Bw. Zhang Xiyuan anashughulikia uboreshaji wa mtaa wa Wahui, anaeleza kuwa, "Kutokana na jitihada za miaka minne, watu wa pande mbili, China na Norway, walitunza makazi mengi ya watu, hususan nyumba tatu za ua za Wahui zenye mtindo maalumu. Vile vile, walikarabati barabara iliyopo katikati ya mtaa huo, na kuweka mfumo wa ugavi wa maji na mifereji ya uchafu."
Mwandishi wetu wa habari alitembelea nyumba moja ya ua iliyotunzwa ambayo ilishinda tuzo ya uhifadhi wa urithi wa kiutamaduni katika sehemu ya Asia na Pasifiki, iliyopewa na Shirika la elimu, sayansi na utamaduni la Umoja wa Mataifa mwaka 2002. Mwenyeji wa nyumba hiyo ya ua ni mzee mwislamu Bw. An Shouxin mwenye umri wa miaka 71. Alieleza kuwa, nyumba hiyo yenye ua imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 200, na anafurahia hatua ya serikali za China na Norway kugharamia ukarabati wake. Mzee huyo anasema, "Hili ni jambo zuri sana, mimi ni mwalimu, mapato yangu si makubwa. Siwezi kumudu gharama za ukarabati wake kwa kujitegemea hata kwa kutumia akiba yangu ya maisha. Katika ukarabati wa safari hii, tatizo la huduma za maji na maji machafu limetatuliwa, barabara imetengenezwa na mazingira yameboreshwa sana."
Pamoja na kukarabati na kutunza makazi ya watu katika mtaa huo wa Waislamu, serikali ya China pia ilitenga fedha maalumu kwa ajili ya ukarabati wa misikiti kadhaa ndani ya mtaa huo. Msikiti mmojawapo unaitwa msikiti mkuu wa Xian, ambao ni mkbuwa kuliko yote katika mtaa huo.
Msikiti huo mkuu ulijengwa miaka 1,200 iliyopita, sasa ni miongoni mwa majengo yanayopewa uhifadhi wa ngazi ya taifa. Katika miaka ya karibuni, serikali ya China ilifanya ukarabati mara kadhaa katika msikiti huo. Hatua hizo si kama tu zimedumisha sura ya awali ya msikiti huo, bali pia kuboresha mazingira ya sehemu zilizo karibu na msikiti. Kuhusu mabadiliko hayo, imamu Ma Liangji wa msikiti huo, ambaye pia ni naibu mkuu wa Shirika la dini ya Kiislamu la China, alisema, "Hapo mwanzoni, ilikuwa ni wakazi wa mtaa huo peke yao waliokuja kwenye msikiti wetu kufanya ibada, lakini sasa msikiti wetu umewavutia Waislamu kutoka sehemu nyingine za China, hata kutoka sehemu nyingine duniani."
Kazi ya uboreshaji wa eneo la hekta 16 la katikati ya mtaa wa Wahui imekamilishwa kwa jumla, na hivi sasa, ukitembelea kwenye mtaa huo, unajikuta katika barabara zilizopangwa vizuri na mazingira mazuri, ambapo kuna nyumba zenye ua za mtindo wa kijadi wa Kichina, maduka, mikahawa ambayo majengo hayo ni yenye mtindo wa Kiislamu, pamoja na misikiti nadhifu. Kazi ya ukarabati imedumisha sura ya kale ya mtaa huo, na pia kufanya mzingira ya huko kulingana na maisha ya kisasa.
Mwandishi wetu wa habari pia alipata habari kuwa, serikali ya mji wa Xian imetunga mpango mmoja wa uhifadhi wa jumla kwa ajili ya kubadilisha sura ya mtaa mzima wa Wahui. Bw. Zhang Xiyuan anayeshughulikia kazi hiyo alisema, "Kwa mujibu wa mpango huo wa uhifadhi wa jumla, mtaa wa Wahui utakuwa eneo la utalii ambalo litaweza kuonesha umaalumu wa utamaduni wa Kiislamu, ambapo maeneo ya bustani na yanayotumika na watu wote yatapanuka, na sehemu za kufanya shughuli za kidini zitaboreshwa zaidi. Kazi yote ya uhifadhi na ukarabati itakapokamilishwa, itaweza kukidhi mahitaji ya kila mkazi wa huko kwa maisha yake ya kila siku na kufanya shughuli za kidini."
Idhaa ya Kiswahili 2007-08-29
|