Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-08-29 18:38:56    
'Daraja la lugha ya Kichina' linaloonesha upendo wa wageni wanaojifunza Kichina kwa utamaduni wa China

cri

Wasikilizaji, je mnachosikiliza sasa hivi ni kipindi cha burudani ambacho wachina wanashiriki? Basi mmekosea. Watu hao si wachina bali ni wagombea walioingia fainali kwenye mashindano ya sita ya lugha ya Kichina duniani.

Wagombea zaidi ya mia moja kutoka nchi 52 waliingia fainali kwenye mashindano hayo yaliyofanyika wiki iliyopita mjini Changchun, China. Wao wote wanaweza kuongea vizuri Kichina, na si hivyo tu, bali pia wanafahamu sana historia, utamaduni na vivutio nchini China, hata wanajua sana kuhusu kuandika na kuchora kwa mtindo wa Kichina, kupiga ala za Kichina na kucheza Gongfu.

Miongoni mwa wagombea hao, kijana mmoja kutoka Laos anajulikana sana. Mbali na matamshi yake sanifu ya Kichina, umaarufu wake kwa kiwango fulani unatokana na jina lake la Kichina, Liu Dehua, ambalo ni sawasawa na jina la mwimbaji nyota wa China. Bw. Liu Dehua alisema:

"nilipewa jina hilo na mama yangu, kwa kuwa anapenda sana nyimbo alizoimba na wahusika wa filamu alioiga Liu Dehua. Pia kutokana na sababu hiyo, alinipeleka kujifunza lugha ya Kichina."

Bw. Liu Dehua aliyeanza kujifunza Kichina kuanzia shule ya chekechea, mwanzoni alikuwa hapendi lugha hiyo kwa kuwa aliona lugha hiyo ni ngumu sana. Baadaye, msichana mmoja wa China alitokea na kubadilisha hisia yake kwa China na lugha ya Kichina. Bw. Liu alisema:

"siku moja, msichana mmoja wa China alihamishiwa kwenye darasa letu, alikuwa anapendeza sana. Lakini alikuwa hawezi kuongea Kilaos. Nilikuwa nataka kuzungumza naye, lakini nilikuwa naogopa kuchekwa kama nikiongoe Kichina vibaya. Kwa hiyo nilianza kujifunza Kichina kwa bidii, ili niweze kuzungumza na msichana huyo mrembo."

Lakini wakati Bw. Liu alipoweza kuongea vizuri Kichina, msichana huyo alihamishwa tena kutoka shule hiyo. Ndipo wakati huo, Bw. Liu alipogundua kwamba amekuwa na hamu ya kujifunza lugha ya Kichina na kupenda utamaduni mkubwa wa China. Kwa hiyo alichagua somo kuu la lugha ya Kichina alipojiunga na chuo kikuu. Bw. Liu alisema,

"nimegundua kuwa, wachina wapo kila nchi duniani, pia wako wengi nchini Laos. Kama nikijifunza vizuri Kichina, baada ya kuhitimu nitaweza kufanya biashara na wachina au kuwa mkalimani wa Kichina. Kazi hizo zinaleta pato kubwa,"

Bw. Liu alisema, mpaka sasa bado anakumbuka na kumshukuru msichana yule wa Kichina, ambaye alimfanya aipende China na lugha ya Kichina. Hivi sasa idadi ya wageni wanaojifunza Kichina imezidi milioni 30, ambao wengi wao wako katika nchi jirani za China zikiwemo Laos, Vietnam, Thailand, Korea ya Kusini na Japan. Hali hiyo inatokana na kuwa utamaduni wa nchi hizo unafanana na ule wa China, pia zina mawasiliano mengi na China, hivyo watu wengi wa nchi hizo wanajifunza Kichina.

Mbali na hayo wanajifunza Kichina si kama tu kwa ajili ya kupata ajira, bali pia wengi wao kweli wana hamu ya kufahamu lugha, utamaduni na historia ya China. Mgombea kutoka Japan Bi. Taniguchi Huruna aliyeanza kujifunza Kichina kwa sababu hiyo. Bi. Huruna alisema:

"mara ya kwanza niliposikia matamshi ya Kichina sanifu, niliona yanavutia sana, na pia nataka kujua kuongea lugha hiyo."

Katika fainali ya mashindano hayo, Bi. Huruna alivaa kimono chenye taswira ya maua ya chrysanthemum, alitoa hotuba ya dakika tatu kwa Kichina kuhusu 'dunia moja na ndoto moja'. Matamshi sanifu na hotuba yake nzuri viliwashangaza watazamaji wa China. Baadaye alikamilisha maonesho yake huku akishangliwa kwa kuimba wimbo mmoja wa Kichina Ronghua.

Mwishoni msichana huyo kutoka Japan alijitokeza miongoni mwa wagombea wote, na kupata udhamini wa masomo ya muda mfupi nchini China. Bi. Huruna alisema, anatumai kuwa atapata fursa nyingi zaidi za kutembelea China na kutembelea kwenye sehemu mbalimbali zenye vivutio nchini China. Pia alisema, hivi sasa wajapan wengi wana hamu kubwa ya kujifunza Kichina, na vyuo vikuu vingi nchini Japan vimeweka somo la lugha ya Kichina.

Hali hiyo si kama inatokea nchini Japan tu, vyuo vikuu mia mbili vya Korea ya Kusini vimekuwa na somo la lugha ya Kichina, na lugha hiyo imewekwa rasmi kwenye mtihani wa kujiunga na vyuo vikuu vya nchi hiyo; nchini Vietnam, lugha ya Kichina imekuwa lugha ya pili ya kigeni baada ya Kiingereza.

Mbali na hayo, kutokana na China kufungua mlango zaidi na uchumi wake kuendelea kukua, mawasiliano kati ya China na dunia yanaendelea kupanuliwa. Lugha ya Kichina ikiwa ni chombo muhimu kwa watu wa nchi mbalimbali kuifahamu China, imevunja kizuizi cha kijiografia, na kupendwa na watu wengi wa mabara ya Ulaya, Amerika na Afrika.

Msichana Huruna kutoka Japan na Bw. Liu Dehua kutoka Laos ni mifano miongoni mwa watu zaidi ya milioni 30 wa nchi za nje wanaojifunza na kuipenda lugha ya Kichina. Kutokana na ongezeko la kasi la uchumi na utamaduni unaong'ara, China inaonesha mvuto wake maalum kwa dunia nzima na kuvutia watu wengi wa nchi za nje kujifunza lugha hiyo ili kuifahamu China.