Kabila la washe ni moja ya makabila madogo madogo nchini China, wengi wao wanaishi katika sehemu ya pwani ya mkoa wa Fujian na mkoa wa Zhejiang. Mababu wa kabila la washe walikuwa wanapenda kuishi maisha ya kuhamahama, na waliwahi kuishi katika sehemu nyingi za kusini mwa China. Na katika maisha yao ya kuhamahama, nyimbo zilikuwa zinafuatana nao siku zote, kurithisha nyimbo zao kizazi hadi kizazi.
Huko Ningde, mkoani Fujian kuna kijiji kidogo kinachoitwa Bailukeng, ambacho kinaegemeana na mlima na bahari, wanakijiji wengi wa kijiji hicho ni wa koo tatu za Zhong, Lei na Lan. Watu wa kabila la washe ni hodari wa nyimbo, wanaimba wakati wowote kama vile kufanya kazi, kupumzika, kuwa na furaha hata na huzuni. Uimbaji nyimbo umekuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu wa kabila la washe.
Mzee Zhong Changyao mwenye umri wa miaka 75 kwa sasa alisema, kwenye sehemu wanakoishi watu wa kabila la washe husikika sauti ya nyimbo nyororo za kabila hilo, hasa katika sikukuu za jadi za kabila hilo huandaa tamasha kubwa linalowashirikisha watu elfu kadhaa. Mzee Zhong aliwahi kushiriki katika tamasha nyingi za kuimbizana nyimbo alipokuwa kijana. Alisema:
"Usiku wa siku moja mimi na binamu yangu wa kike tulikuwa tunaenda kwenye kilele cha mlima kuimbizana nyimbo hadi usiku wa manane. Njiani wakati tukirudi kulikuwa na dhoruba na mvua kubwa, na tulilowa kabisa, lakini tulifurahi sana."
Mzee Zhong alisema, kabila la washe lina lugha yake, lakini lugha yao haina herufi za maandishi, hivyo nyimbo zote za kabila hilo zilikuwa zinarekodiwa kwa lugha ya Kihan. Kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii, watu wa kabila la washe na wahan walikuwa wamechanganya zaidi na zaidi, na mila na desturi za kabila la washe zilikuwa zimetoweka siku hadi siku, vijana wa kabila la washe hata hawajui kuongea lugha yao, sembuse kuimba nyimbo zao, hivyo nyimbo za kabila la washe zinakabiliwa na hatari ya kutoweka kabisa. Hali hiyo imempa mzee Zhong wasi wasi kubwa. Alisema:
"Zamani familia zote za kijiji cha Bailukeng zilikuwa na vitabu vya nyimbo vilivyonakiliwa kwa mkono. Lakini hivi sasa kutokana na kufariki dunia kwa wazee wa rika langu, vitabu vingi vya nyimbo vimepotea bila kuhifadhiwa."
Katika miongo kadhaa iliyopita, tamasha la kuimba nyimbo lilikuwa karibu kutoweka katika kijiji cha Bailukeng na vijiji vingine vya kabila la washe. Ili kuokoa nyimbo za jadi za kabila la washe, mwaka 2002 mzee Zhong aliamua kukusanya nyimbo hizo kwa kujigharimia. Alisema:
"Katika miaka mitano iliyopita nilikuwa nimetembelea vijiji 71 vya watu wa kabila la washe katika wilaya 5 kukusanya nyimbo za jadi za kabila la washe. Nilikuwa tayari nimekusanya nyimbo zenye maneno zaidi ya laki nane."
Siku moja mzee Zhong alipopata habari kuwa, katika familia moja ya kijiji kingine chenye umbali mrefu kutoka kijiji alichoishi kuna vitabu vingi vyenye nyimbo zaidi ya 1000 za kabila la washe alifurahi sana. Lakini alipofika kuomba kuzikusanya alikataliwa, hivyo alipaswa kuzinakili moja moja kwa mkono. Mke wake Bi. Lei Wenyupia anapenda kuimba nyimbo, hivyo alikuwa amempa uungaji mkono mkubwa. Akisema:
"Mume wangu amefanya kazi ya kukusanya nyimbo za kabila la washe kwa miaka zaidi ya mitano, mimi pia napenda kuimba nyimbo, hivyo nikiwa na wakati humsaidia kunakili nyimbo alizozikusanya. Ni jambo lenye maana kurithisha utamaduni wa kabila la washe."
Nyimbo za kabila la washe zilizokusanyiwa na mzee Zhong ni pamoja na nyimbo za mapenzi, nyimbo za riwaya na nyinginezo. Amesifiwa sana kwa nia yake imara na upendo wake mkubwa kwa nyimbo za kabila la washe, na juhudi zake zimeleta matokeo mazuri . Mwanakijiji Lei Along alisema:
"Sisi vijana wa kijiji cha Bailukeng tulikuwa hatujui kuongea lugha ya kabila la washe, sembuse kuimba nyimbo za jadi za kabila letu. Lakini kufundishwa na mwalimu Zhong Changrao, hivi sasa tumefahamu umaalum wa nyimbo za kabila la washe. Kabila la washe lina lugha yake lakini lugha hiyo haina herufi, hivyo historia, utamaduni na lugha ya kabila hilo zinapaswa kurithishwa kwa njia ya kuimba nyimbo kizazi hadi kizazi."
Hivi sasa kazi ya kuokoa na kuhifadhi nyimbo za kabila la washe imefuatiliwa na serikali ya huko na watu wa kabila hilo. Serikali ya huko imeanzisha ofisi ya kuokoa utamaduni wa kabila la washe, na kuweka mpango wa kuchapisha nyimbo za kabila la washe zilizokusanywa na Bw. Zhong na watu wengine. Tunatumai kuwa nyimbo za jadi za kabila la washe zitaimbwa na vizazi vijao bila kusita.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-05
|