Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-03 16:58:01    
Maeneo ya Shannan?chimbuko la utamaduni wa Tibet

cri

Maeneo ya Shannan yaliyoko upande wa kusini wa milima ya Tanggula na Gandise na sehemu ya kati na ya mwisho ya mto Yalu Tsangpo ni chimbuko la utamaduni wa kale wa Tibet, mahali hapo palikuwa na utajiri na penye utamaduni mkubwa katika zama za kale. Katika maeneo hayo kuna kasri la kwanza la Yongbulakang na hekalu la kwanza la Changzhusi la dini ya Kibuddha mkoani Tibet.

Mkoani Tibet kuna hadithi inayosimuliwa miongoni mwa Watibet, inasema kuwa babu wa watu wa Tibet alikuwa ni kima aliyetawa, kima huyo aliishi katika maeneo ya Shannan na jina la mji mkuu wa Shannan, Zedang, katika lugha ya Kitibet ina maana ya "mahali pa kucheza kwa kima".

Umaarufu wa Shannan hautokani na hadithi hiyo peke yake, bali unatokana zaidi kwa kuwa na Enzi ya Kifalme ya Tufan katika zama za kale. Mkuu wa Idara ya Mabaki ya Kale ya Mkoa wa Tibet Bw. Gengduinacuo alisema,

"Enzi ya Kifalme ya Tufan ilianza katika maeneo ya Shannan na iliacha mabaki mengi kama makasri, mahekalu na makaburi, sehemu ya makaburi ya Chongjie imewekwa na serikali chini ya hifadhi ya kitaifa, makaburi hayo ni ya vizazi vya mfalme Songtsam Gambo."

Mkuu huyo alituambia kuwa mabaki maarufu katika maeneo ya Shannan ni kasri la Yongbulakang na mahekalu ya Changzhusi na Sangyesi. Kasri la Yongbulakang ni kasri la kwanza kabisa mkoani Tibet, kasri hilo ilijengwa katika karne ya pili K.K. katika lugha ya Kitibet neno "Yongbulakang" lina maana ya "kasri lililojengwa kwenye mguu wa nyuma wa swala jike", kwa sababu mahali penye kasri hilo ni mgongo wa mlima ambao umbo lake ni kama mguu wa swala aliyelala, na kasri hilo lilijengwa kwenye mguu huo. Mkuu wa ofisi inayotunza kasri hilo Bw. Pubuduoji alieleza,

"Kasri hilo lilijengwa kwa ajili ya mfalme wa kwanza wa Tibet Niechizanpo, mfalme Songtsam Gambo na mke wake, binti wa mfalme Wencheng wa kabila la Han waliwahi kuishi katika kasri hilo. Baada ya ujenzi wa kasri la Potala kukamilika, kasri la Yongbulakang liligeuzwa kuwa hekalu. Kasri la Yongbulakang limekuwa chini ya hifadhi ya kitaifa na kuwa sehemu ya utalii."

Ndani ya kasri hilo kuna picha nyingi za ukutani zikieleza hadithi za maisha ya mfalme wa kwanza wa Tibet Niehezanpo, picha hizo pia zinaeleza hadithi nyingi zinazosimuliwa na Watibet.

Jengo linalovutia zaidi katika kasri hilo ni mnara wa kuangalia mbali uliojengwa kwa mawe. Tofauti na majengo mengine, yote yalijengwa kwa mawe ya kiasili bila kuchongwa, ingawa miaka zaidi ya elfu mbili imepita, lakini majengo hayo yanaendelea kuwa mazima.

Mkuu wa ofisi ya kutunza kasri la Yongbulakang Bw. Pubuduoji alieleza kuwa watu wengi wanatembelea au kufanya ibada kwenye kasri la Yongbulakang kutoka sehemu mbalimbali nchini na nchi za nje. Mtalii kutoka Ubelgiji aitwaye Macela de Bock alisema,

"Nashangaa kuona majengo ya hapa. Kabla ya kuja hapa tuliwahi kutembelea hekalu la Sangyesi, hapa ni kituo chetu cha pili katika utalii wa leo."

Hekalu la Sangye lilijengwa zaidi ya miaka elfu moja iliyopita, ni hekalu lenye historia ndefu sana kati ya mabaki ya utamaduni wa Kitibet. Hekalu hilo lilijengwa kwa matabaka matatu na kila tabaka lilijengwa kwa mtindo wake wa Kitibet, Kihindi na mtindo wa kabila la Kihan. Ndani ya hekalu hilo kuna mabaki mengi kuhusu historia ya Tibet, dini ya Kibuddha, picha na sanamu. Picha zilizochorwa kwenye kuta zina urefu wa mita 92, na kati ya picha hizo picha kuhusu mchezo wa polo, ni picha ya mwanzo kabisa inayoonesha mchezo huo duniani.

Bw. Ding Shixu ni mtalii kutoka mji wa Shenzhen, mji uliopo kusini mwa China, alipoona mabaki hayo alisema kwa furaha,

"Mandhari ya hapa inanivutia kweli na siwezi kusahau maishani mwangu, nashukuru kwamba Tibet inazingatia sana utunzaji wa mabaki ya kale."

Licha ya makasri na mahekalu, maeneo ya Shannan pia ni chanzo cha opera ya Kitibet. Miaka 500 iliyopita, ili kujenga daraja sufii Tangdongjiebu alichangisha fedha kwa kuwashirikisha vijana kuonesha opera, baadaye opera hiyo iliendelea na kuwa opera maalumu ya Kitibet.

Hivi leo maeneo ya Shannan yanavutia watalii wa sehemu mbalimbali duniani, na katika maeneo hayo wenyeji wameanza shughuli za aina mbalimbali za kibiashara, maisha ya wenyeji yameinuka haraka.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-03