Wilaya ya Shan mkoani Shandong mashariki mwa China, ni sehemu inayozalisha pamba kwa wingi nchini China. Mwishoni mwa mwaka jana, kiwanda cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe nchini China-Kampuni ya kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe ya wilaya ya Shan ya Guoneng ilianzishwa huko. Kiwanda hicho kinatumia nishati endelevu, hivyo sio tu kinahimiza maendeleo ya uchumi wa huko, bali pia kinabana matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira.
Nishati ya viumbe ni nishati kubwa ya nne duniani baada ya makaa ya mawe, mafuta na gesi, na nishati ya viumbe ni pamoja na mabua ya mazao ya kilimo na takataka zinazotokana na utengenezaji wa mbao. Kwa kuwa nishati ya viumbe ni safi, na inasaidia kuhifadhi mazingira, hivyo serikali ya China inahimiza maendeleo ya nishati hiyo, na kuufanya uendelezaji wa nishati hiyo kuwa sehemu muhimu ya kutekeleza mkakati wa nishati kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Mwezi Septemba mwaka 2004, kamati ya maendeleo na mageuzi ya China ilianza rasmi ujenzi wa mradi wa kiwanda cha kwanza cha kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe. Baada ya mradi huo kuthibitishwa, suala muhimu lilikuwa kuchagua sehemu ya kujenga kiwanda hicho. Kwa kuwa nishati ya kiwanda hicho ni mabua ya ngano na pamba na takataka zinazotokana na shughuli za kilimo na misitu, hivyo upatikanaji wa kutosha wa nishati kwa ajili ya kiwanda hicho ilikuwa ni lazima uzingatiwe kwanza.
Mkurugenzi wa ofisi ya nishati ya idara ya kilimo ya wilaya ya Shan Bw. Zhou Tingying alisema, hiyo ni wilaya inayozalisha kwa wingi mazao ya kilimo na bidhaa za mbao, wakulima wa huko wanapanda ngano, pamba na karanga, ambayo yanatoa malighafi nyingi ya mabua na mbao kwa ajili ya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya viumbe. Alisema,
"Kwenye wilaya ya Shan kuna watu milioni 1.17, miongoni mwao idadi ya watu wanaojishughulisha na kilimo ni laki 9.7, na eneo la mashamba yanayolimwa ni hekta laki 1, na eneo linalotumika kwa ajili ya kilimo cha pamba ni zaidi ya hekta elfu 20, hivyo kuna maliasili ya kutosha ya nishati ya viumbe."
Baada ya mwaka mmoja na zaidi, kiwanda cha kwanza cha uzalishaji wa umeme kwa nishati ya viumbe kilianzishwa wilayani Shan nchi China. Baada ya kuanzishwa kwa kiwanda hicho, ili kuhakikisha utoaji wa nishati ya mabua, wilaya hiyo ilianzisha vituo vinane vya kununua mabua. Vituo hivyo vinane viko kwenye sehemu mbalimbali, pia vina wafanyakazi wengi, ambao wanagawanya nishati mbalimbali za mabua, malighafi zinazotokana na utengenezaji wa mbao na magome ya miti. Naibu meneja wa kampuni ya kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe ya wilaya ya Shan ya Guoneng Bw. Liu Chengjiang aliona kuwa, nishati hizo zinakidhi mahitaji ya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya viumbe.
Wakazi wa huko walifahamisha kuwa, kabla ya kujengwa kwa kiwanda hicho, mabua yalikuwa yanachukuliwa kuwa ni takataka, hakuna mtu aliyefikiri kuwa mabua yanaweza kuleta mapato ya ziada. Lakini kiwanda hicho kinatumia mabua ya ngano na pamba kuwa nishati ya kuzalisha umeme, na kinaleta mapato mengi kwa wakulima wa huko. Meneja wa kampuni ya kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe ya wilaya ya Shan ya Guoneng Bw. Liu Guangqiang alisema,
"Kwa kupitia kununua takataka hizo, kila mwaka tunaweza kuwapatia wakulima wa huko Yuan za RMB milioni 40 hadi 50."
Hivi sasa teknolojia ya nishati ya viumbe duniani bado iko katika kipindi cha mwanzoni cha maendeleo, na kiwango cha kuendeleza viwanda na biashara bado kiko chini, hivyo faida za miradi mingi ya kuzalisha umeme sio kubwa.
Naibu meneja mkuu wa kampuni ya uzalishaji wa umeme kwa nishati ya viumbe ya wilaya ya Shan ya Guoneng Bw. Liu Chengjiang alisema,
"Tumeridhishwa na mradi huo, kila siku tunaweza kuzalisha kilowati laki 7.2 za umeme, hadi tarehe 2 mwezi Juni, tulizalisha kilowati milioni 97 za umeme."
Licha ya hayo, jambo linalofurahisha zaidi ni kuwa, mazingira ya wilaya ya Shan na sehemu za karibu yameboreshwa kidhahiri. Nishati ya viumbe sio tu zimetumika badala ya makaa ya mawe na mafuta, bali pia zinaweza kupunguza utoaji wa hewa ya carbon dioxide inayosababisha kuongezeka kwa hali joto. Utafiti husika wa shirika la nishati la kimataifa umeonesha kuwa, mabua ni nishati safi, mbali na hayo, mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya viumbe unachukua hatua nyingi za kushughulikia uchafuzi, hivyo athari zake mbaya kwa mazingira ni ndogo zaidi.
Aidha, kurudisha na kutumia mabaki ya kilimo kunawasaidia wakulima wa huko kubadilisha tabia zao za kuteketeza mabua uwanjani, na hivyo kukifanya kijiji kuwa na sura mpya ya usafi. Bw. Liu Chengjiang alimwambia mwandishi wetu wa habari kwa furaha akisema,
"Tukiwa wajenzi, tunaweza kuzalisha kilowati ya kwanza ya "umeme bila uchafuzi" kwa taifa letu, tunafurahi sana."
Habari zinasema China imetunga sera nyingi za kuhimiza na kuendeleza miradi ya nishati endelevu, na itatoa uungaji mkono wa kifedha katika utafiti na maendeleo ya teknolojia. Wataalam wanasema katika hali hiyo, mwendo wa maendeleo ya sekta ya nishati endelevu ya China umeharakishwa. Lakini ikiwa shughuli mpya, bado kuna matatizo mengi katika teknolojia, sheria husika na uwekezaji na ukusanyaji mitaji katika mchakato wa ujenzi na uendelezaji wake. Ni kwa kutatua matatizo hayo tu, ndipo sekta ya nishati endelevu inaweza kuwa na maendeleo endelevu.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-04
|