Leo kwanza tunawaletea Orodha ya majina ya washindi katika mashindano ya chemsha bongo kuhusu vivutio vya "Mkoa wa Sichuan, maskani ya Panda"
Wasikilizaji wawili waliopata nafasi ya kwanza ni kama wafuatao: Bw. Ras Franz Manko Ngogo wa S.L.P. 71 Tarime?Mara, Tanzania, na Bw Xavier L. Telly-Wambwa wa S.L.P. 2287 Bungoma Kenya.
Wasikilizaji wanne waliopata nafasi ya pili ni kama wafuatao:
Bwana Mbarouk Msabah Mbarouk wa S.L.P. 52483 Dubai U.A.E, Bwana Martin Y. Nyatundo wa S.L.P. 3701 Kisii Kenya, Bi. Mwanahija Khamis Mohamed wa S.L.P. 2439 Zanzibar Tanzania, na Bwana Marwa F. Gati wa S.L.P. 495 Tarime?Mara Tanzania.
Wasikilizaji wanane waliopata nafasi ya tatu ni kama wafuatao: Bw Josephati L. Nyalandu wa S.L.P. 1632 Singida Tanzania, Bw Emanuel Benard wa S.L.P. 71 Tarime?Mara Tanzania, Bw Chacha Mabarara wa S.L.P. 71 Tarime?Mara Tanzania, Bw Daniel Chacha wa S.L.P. 245 Tarime?Mara Tanzania, Bw Hillary K. Kirui wa S.L.P. 42422 Nairobi Kenya, Bw Kepher O. Gichana wa S.L.P. 2028 Kisii Kenya, Bw Cabriel Gimonge Gimosa wa S.L.P. 423 Migori?Suna Kenya, na Bw Paul Mungai Mwangi wa S.L.P. 69 North Kinangop Kenya.
Tunawapongeza sana wasikilizaji wote hawa kwa juhudi zao hadi kuweza kujipatia ushindi. Kwa wasikilizaji ambao hamkuweza kupata ushindi tunawaomba msikate tamaa, kwani Radio China kimataifa inaandaa shindano la chemsha bongo kila mwaka, kwa hiyo bahati yenu iko njiani. Na sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.
Msikilizaji wetu Yakub Saidi Idambira wa sanduku la posta 124 Kakamega, nchini Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu nyingi kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, akiwa na matumaini kuwa wote ni wazima na tunaendelea kuchapa kazi ya kuwahudumia kwa matangazo na vipindi vya kuelimisha, kutoa habari na kuburudisha. Anasema kwa upande wake yeye ni mzima wa afya na anaendelea na shughuli zake za kila siku za ujenzi wa taifa.
Anasema lengo la kutuandikia barua hii ni kutaka kutufahamisha mabadiliko ya anuani yake kuwa sasa itakuwa 124 badala ya hii ya 2519, hivyo anasema tukimwandikia barua tutumie anuani hii mpya ya 124, na anatumai kuwa tutakumbuka mabadiliko haya. Pia anapenda kutoa pongezi hasa kwa Mama Chen na Bw Fadhili Mpunji kwa jinsi wanavyokitangaza kipindi cha jifunze kichina kwa lahaja za kichina na kisha kutafsiri katika lahaja na ngeli za Kiswahili, ili kuwawezesha wasikilizaji kutamka kwa urahisi na kuandika.
Anasema hii inaonesha na kudhihirisha wazi kuwa Radio China Kimataifa unawajali na kuwathamini wasikilizaji wetu, na pia kuwachukulia kuwa kiungo muhimu katika harakati zetu za kutoa habari na mawasiliano. Jambo la muhimu anaona kuwa viongozi na Idara husika kuchapisha vijitabu vidogo vya Jifunze Kichina ili kutoa mchango mkubwa wa kuendeleza lugha ya kichina, na hivyo kuwavutia wasikilizaji wengi na hasa walioko vijijini.
Matarajio yake ni kuwa uongozi wa Radio China tutazingatia maoni na mapendekezo yake na kuyatekeleza kwani itakuwa ni ufanisi mwingine kwa Radio China Kimataifa hasa katika wakati huu wa utandawazi. Kwa niaba ya wasikilizaji wa mkoa wa magharibi anauomba uongozi wa Radio China na serikali ya watu wa China kuanzisha kitengo cha lugha ya kichina katika chuo cha Masinde Muliro kilichoko huko Kakamega katika makao makuu ya mkoa wa magharibi, kama ilivyofanyika katika chuo kikuu cha Nairobi kuanzishwa kwa kitengo hicho. Wasikilizaji na wanafunzi wengi wa mkoa huo watanufaika kwa kujifunza lugha ya kichina kwa urahisi.
Mwisho anamaliza barua yake kwa kusema anatumai tutatuma ujumbe kwenda mkoani magharibi kufanya utafiti chuo cha Masinde Muliro, ili tuweze kuanzisha kitengo cha kujifunza lugha ya kichina. Watafurahi kukutana na Mama Chen na watangazaji wengine, na wanamkaribisha Mama Chen mkoani magharibi, kwani wana hamu ya kumuona. Anatutakia kila la kheri na baraka katika shughuli zetu.
Tunamshukuru sana Yakub Saidi Idambira kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu kipindi cha jifunze Kichina, kweli tumetiwa moyo sana, ingawa tulifanya majaribio ya kubadilisha njia ya kuwafundisha wasikilizaji wetu Kichina, njia hiyo ya majaribio inawafurahisha wasikilizaji wetu kweli, huu ni uungaji mkono kwa juhudi zetu. Tunaendelea na juhudi na kuzingatia kwa makini maoni na mapendekezo ya wasikilizaji wetu. Kwani katika siku zijazo kazi ya maandalizi ya kipindi cha jifunze Kichina bado itakuwa ni kubwa sana, kwa jumla vipindi vitakuwa vingi, hata muda utaongezwa, kama majaribio yetu yataweza kukubaliwa na wasikilizaji wetu, tutajitahidi kuboresha maandalizi yetu kwa kadiri tuwezavyo.
Msikilizaji wetu mwingine ni Bw. Mbarak Mohamed Abucheri wa sanduku la Posta 792 Kakamega, nchini Kenya, ametuletea barua ya kutupongeza kwa kuboresha kipindi chetu cha Jifunze kichina na anatupa salamu nyingi wafanyakazi wote wa Radio china Kimataifa na kwamba anatumai kuwa sisi ni wazima wa afya njema. Anasema yeye pia ni mzima na anaendelea na shughuli za kulijenga taifa, bila kusahau kusikiliza Radio China Kimataifa kwa vipindi vya habari, elimu na burudani.
Anapenda kuchukua nafasi hii kutoa pongezi zake za dhati kwa uongozi wa Radio China Kimataifa kwa kuchukua hatua ya kukiboresha kipindi cha jifunze kichina. Katika kukiboresha zaidi kipindi hiki, anapendekeza tuchapishe vijitabu vya Jifunze kichina, na turekodi vipindi vya jifunze kichina katika kanda na tuwatumie wasikilizaji wetu. Anamaliza barua yake kwa kusema anatarajia mapendekezo yake tutayazingatia.
Katika barua yake nyingine msikilizaji wetu Mbarak Mohamed Abucheri anatupa pongezi na kutushukuru kwa kuanzisha kitengo maalumu cha mafunzo ya lugha ya kichina na utamaduni katika kituo cha FM, jijini Nairobi. Anasema hakika hii ni hatua nyingine muhimu katika kuboresha matangazo na vipindi vya idhaa ya Kiswahili na kujenga uhusiano na kudumisha mawasiliano kati ya wasikilizaji na Radio china kimataifa. Anaipongeza serikali ya China kwa ushirikiano na serikali ya Kenya kwa mawazo na fikra zilizokomaa, kuanzisha kitengo maalumu cha mafunzo ya lugha ya kichina ambacho anasema kitatoa nafasi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na wasikilizaji nchini Kenya na Afrika mashariki kwa jumla kujifunza lugha na tamaduni mbalimbali za kichina vizuri zaidi.
Anatumai kuwa wanafunzi wengi wataweza kuzungumza na kutamka maneno ya kichina kwa ufasaha, na wengine kwa kuandika lugha, ngeli na lahaja za kichina kwa umakini. Pia wanafunzi na watu wa China watanufaika kwa kujifunza lugha ya Kiswahili na Kiingereza kutoka kwa ndugu zao wa Afrika mashariki, kwa kuzingatia mpango wa kubadilishana wanafunzi wa vyuo vikuu, ambapo wanafunzi kutoka Kenya hupata nafasi ya kuja China kupata elimu ya juu, na wanafunzi kutoka china kwenda Kenya katika vyuo vikuu ili kujifunza lugha na tamaduni mbalimbali.
Mwisho anaomba idhaa ya Kiswahili ya Radio china tuanzishe mpango wa kujifunza kichina kwa kutoa nafasi maalumu kwa wasikilizaji wetu. Kwa kuanza mpango huu anapendekeza tuanze na nafasi tano. Anashukuru na kutupongeza kwa kumtumia jarida la China Today na kadi za salamu.
Tunamshukuru kwa dhati Mbarak Mohamed Abucheri na wasikilizaji wengine wanaotuletea barua kueleza maoni na mapendekezo yao kuhusu kipindi cha kujifunza Kichina, tutazingatia kwa makini, kama ikiwezekana tutarekebisha kazi husika kwa kufuata mapendekezo ya wasikilizaji wetu.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-04
|