Hivi sasa nchini China kuna watu zaidi ya milioni 11 wenye mtindio wa ubongo. Huko Shanghai, mji wa mashariki ya China, ulianzishwa mradi uitwao "vituo vyenye matumaini" vyenye lengo la kutoa huduma kwa watu hao.
Katika mji huo, ambao ni mji mkubwa kabisa wa viwanda na biashara nchini China, kuna watu zaidi ya elfu 70 wenye mtindio wa ubongo. Kutokana na kuwa na matatizo ya ubongo, watu hao wana uwezo mdogo wa ujuzi na ufundi. Kwa kawaida wakimaliza masomo kwenye shule maalumu, asilimia kubwa ya watu wenye mtindio wa ubongo hawana budi kubaki majumbani kwao. Ni nadra kwao kuwasiliana na watu wengine, isipokuwa jamaa zao.
Mwaka 2005 serikali ya mji wa Shanghai ilianza kutekeleza mradi wa kujenga "vituo vyenye matumaini" kwenye mitaa mbalimbali. Mradi huo unatoa mafunzo bila malipo kwa watu wenye mtindio wa ubongo na kuwahamasisha wawasiliane na wengine kwenye jamii. Mpaka sasa vituo kana hivyo zaidi ya 240 vimeanzishwa huko Shanghai, ambavyo vinawahudumia watu elfu 11.5.
Bibi Shao Lili ni mama mzazi wa mtoto mwenye mtindio wa ubongo. Mama huyo mwenyewe ni mgonjwa anaugua vibaya, mume wake hana ajira. Mama Shao alisema, zamani mtoto wake alikuwa anakaa nyumbani bila kusema chochote. Kutokana na hali hiyo, mama huyo aliwahi kupoteza matumaini ya kuendelea kuishi. Tangu mtoto huyo aingie kwenye "kituo chenye matumaini", alianza kuwa mchangamfu, na kurudi nyumbani akiwa na furaha, hali ambayo inailetea matumaini familia hiyo yenye ugumu wa maisha. Mama Shao Lili alisema "Binti yangu ana ulemavu wa mtindio wa ubongo, lakini ninamthamini sana. Akipata furaha, familia yangu inakuwa na mabadiliko. "Kituo chenye matumaini" kilimsaidia binti yangu, pia kiliiokoa familia yangu, nilipata tena matumaini ya kuendelea kuishi na maisha yakawa na matumaini."
Katika vituo hivyo, watu wenye mtindio wa ubongo wanapata mafunzo ya kuishi, kufanya kazi na kuwasiliana na watu wengine, wanashiriki kwenye michezo na kufanya kazi nyepesi. Baada ya mafunzo hayo, wanaonekana kuwa uwezo mkubwa zaidi katika kufanya shughuli za kila siku kwa kujitegemea na kufanya mawasiliano na watu wengine. Zamani watu wengi wenye mtindio wa ubongo hawakusema chochote siku nzima, sasa wanapenda kuzungumza na jamaa. Wengi wao sasa wanaweza kuwasaidia wazazi wao kufanya kazi nyepesi za nyumbani, kama vile kufua nguo na kusafisha nyumba.
Dada Lu Xianping ana mtindio wa ubongo, amekuwa anashiriki kwenye shughuli za "kituo chenye matumaini" kwa zaidi ya mwaka mmoja. Alisema "Nafurahia kuwa hapa, kwani nina marafiki wengi. Pia kuna mwalimu wa dansi anatufundisha kucheza dansi na wanafunzi wa vyuo vikuu wanatufundisha lugha ya Kiingereza."
Walimu wengi wa "vituo vyenye matumaini" ni watu wanaojitolea, na wanafunzi wa vyuo vikuu wanachukua sehemu kubwa kati yao. Katika kila "kituo chenye matumaini", watu wanaojitolea zaidi ya 10 wanatoa huduma, wanawasaidia watu wenye mtindio wa ubongo kufanya kazi na michezo, kuwafundisha ujuzi, namna ya kuimba na kucheza dansi.
Dada Ning Shuxian bado anasoma kwenye chuo kikuu ni mmoja kati ya watu wanaojitolea kutoa huduma katika "kituo chenye matumaini". Alieleza kuwa amejifunza mengi kutokana na watu wenye mtindio wa ubongo. Alisema "Wanajifunza kwa haraka lugha ya Kiingereza. Siku nyingine nawafundisha majina ya matunda, wananiuliza maswali ambayo hata sisi wanafunzi wa vyuo vikuu tunashindwa kuyajibu, natafuta majibu kwenye kamusi kabla ya kuwaelezea. Wao ni watoto wenye furaha, ninapoona jinsi wanavyojitahidi kujifunza, nafikiri kuwa sisi pia tunaweza kufanya bidii kama wao. Na tunapokumbwa na shida, tutazikabili kwa ushujaa."
Suala la ajira kwa watu wenye mtindio wa ubongo siku zote ni suala gumu linalozikabili serikali mbalimbali, hasa suala la kuwapa ajira vijana wenye ulemavu huo wenye umri wa miaka kati ya 16 na 35. Kutokana na mpango wa serikali ya mji wa Shanghai, viwanda 50 maalumu vitajengwa ambapo watu wenye ulemavu kiasi wa mtindio watapewa kazi rahisi kwenye viwanda hivyo.
Hivi sasa kila kituo chenye matumaini huko Shanghai kinatoa mafunzo ya kazi rahisi za kutengeneza vitu vidogo kwa mikono, vitu hivyo vinauzwa na watu wenye mtindio wa ubongo ambao wanalipwa kwa kazi hiyo. Viwanda hivyo pia vinalipa bima za utunzaji wa uzee, matibabu na kukosa ajira kwa ajili ya watu hao wenye mtindio wa ubongo.
Hivi sasa dada Lu Xianping mwenye mtindio wa ubongo anapata mafunzo ya kutengeneza wanasesere kwenye "kituo chenye matumaini", pia ana mshahara wa uhakika kila mwezi. Alisema "Inanichukua muda wa wiki moja kwa kutengeneza mwanasesere mmoja. Hii ni kazi inayochukua muda na inahitaji umakini. Kila mwanasesere anauzwa kwa Yuan zaidi ya 100."
Mwezi Oktoba mwaka huu michezo ya 12 ya Olimpiki maalumu itafanyika mjini Shanghai, michezo ambayo inawashirikisha watu wenye mtindio wa ubongo. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa michezo hiyo kufanyika barani Asia na katika nchi zinazoendelea. Imefahamika kuwa wachezaji na makocha zaidi ya elfu 10 kutoka nchi na sehemu 170 hivi watashiriki kwenye michezo hiyo.
"Vituo vyenye matumaini" huko Shanghai vile vile vinatoa viwanja kwa watu wenye mtindio wa ubongo kufanya mazoezi ya michezo, ambao wana hamu kubwa na kufanyika kwa michezo ya Olimpiki maalumu kwenye maskani yao.
Lengo la michezo hiyo ni kusisitiza uwezo walio nao watu wenye mtindio wa ubongo, kuwasaidia watu hao waishi kama watu wengine, kama vile kuwa na ajira na kuanzisha familia. Hili pia ni lengo la "vituo vyenye matumaini" vya Shanghai, ambavyo vina nia ya kuwaandalia watu wenye mtindio wa ubongo mazingira mazuri zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-06
|