Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-07 16:32:16    
China na Somalia zaimarisha uhusiano wa kirafiki

cri
Tarehe 31 mwezi Agosti, Rais Abdullahi Yusuf Ahmed wa serikali ya mpito ya Somalia na balozi wa China nchini Kenya Bw. Zhang Ming ambaye yuko ziarani nchini Somalia walisaini waraka kuhusu serikali ya China kutoa msaada bila malipo wa dola za kimarekani milioni 1.6 kwa serikali ya Somalia, ili kuunga mkono juhudi za kufufua uchumi na ukarabati wa nchi hiyo.

Fedha hizo dola za kimarekani milioni 1.6, ni pamoja na dola milioni 1 kwa ajili ya ukarabati wa Ikulu ya nchi hiyo, dola laki 5 kwa ajili ya mambo ya afya na nyingine laki 1.3 kwa ajili ya dawa za kutibu malaria. Bw. Zhang Ming alimwambia rais Yusuf kwamba labda fedha hizo za msaada si nyingi, lakini zinaweza kuonesha udhati wa moyo wa wananchi wa China kuwasaidia wananchi wa Somalia. Balozi Zhang alisema, serikali ya China siku zote inaunga mkono mchakato wa amani ya Somalia, kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali ya mpito ya Somalia katika kurejesha amani nchini humo, na kufanya ukarabati wa nchi. Pia alipongeza kufungwa kwa mafanikio kwa mkutano wa maafikiano ya kitaifa wa Somalia, na kuusifu mkutano huo kuwa ni wa kihistoria katika mchakato wa amani ya Somalia.

Rais Yusuf alishukuru uungaji mkono na msaada wa serikali ya China, akisema ingawa mkutano wa maafikiano ya kitaifa umemalizika, lakini serikali ya mpito ya Somalia itaendelea na juhudi katika kutimiza maafikiano ya kitaifa kote nchini.

Siku hiyo balozi Zhang Ming vilevile alimtembelea waziri mkuu wa serikali ya mpito ya Somalia Bw. Ali Mohamed Gedi, ambapo Bw. Gedi alimwelezea Bw. Zhang hali ya ujumla ya hivi sasa nchini Somalia, akisema sasa huduma za kijamii ambazo zinahusiana na maisha ya kila siku ya wananchi na elimu ambayo ni uti wa mgongo wa taifa zinapaswa kupewa kipaumbele katika kurejeshwa.

Balozi Zhang alimwambia Bw. Gedi kwamba, kuanzia mwaka huu, serikali ya China itatoa udhamini wa masomo kwa wanafunzi 20 wa Somalia kwa mwaka, ambao watasoma katika vyuo vikuu nchini China.

Urafiki wa Somalia na China ulianza tangu enzi na dahari. Mnamo mwaka 1960 Somalia na China zilianzisha uhusiano wa kibalozi, Somalia ni moja kati ya nchi za Afrika ambazo zilianzisha mapema zaidi uhusiano wa kibalozi na China. Baada ya hapo hadi mwaka 1990, urafiki na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili uliendelea vizuri. Mwaka 1971, Somalia pamoja na nchi nyingine zilitoa mchango mkubwa katika kuisaidia China kurudisha kiti chake halali kwenye Umoja wa Mataifa.

Kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1990, misaada ya kila aina iliyotolewa na China kwa Somalia ni yenye thamani ya Yuan za Renmibi za China milioni 500, ni sawa na dola za kimarekani milioni 67, kiasi hicho kwa China ya wakati ule ambayo ni nchi iliyoanza kupiga hatua ya kwanza kimaendeleo, ni kikubwa sana. Misaada hiyo ni pamoja na misaada bila malipo, mikopo bila riba, vile vile China ilisaidia Somalia kujenga barabara, uwanja wa michezo, hospitali, viwanda, jumba la taifa la maonesho na vituo vya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji.

Siku hiyo mwandishi wetu wa habari aliambatana na Bw. Zhang Ming katika kutembelea miradi kadhaa mjini Mogadishu, kama vile hospitali ya Benadir, jumba la taifa la maonesho, kiwanda cha sigara na uwanja wa michezo. Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa, majengo hayo ni kama yalivyo mejengo mengine karibu yote mjini Mogadishu, ambayo hayatumiki kwa sasa, kutokana na kuharibiwa kwa kiasi tofauti katika vita vilivyodumu kwa miaka 17 tangu mwaka 1991 wakati serikali ya Mohamed Siad Barre ilipoangushwa. Lakini kwa kuangalia mabaki ya majengo hayo, tunaweza kupata picha kuwa, wakati ule majengo yalikuwa mazuri. Mwandishi wetu wa habari alituambia, uwanja ule wa michezo ambao sasa ni kama kambi ya kijeshi, ulikuwa wa kisasa, ulikuwa na uwanja wa mpira wa kikapu, uwanja wa mpira wa mikono, bwawa la kuogelea, la mchezo wa kupiga mbizi, hata kulikuwa na uwanja wa Tennis, katika wakati ambapo Tennis ilikuwa ni mchezo wa kigeni sana kwa wachina walio wengi, uwanja wa michezo mkubwa kama huo hata nchini China ulikuwa chache sana.

Isitoshe kabla ya mwaka 1991, mawasiliano ya kiutamaduni kati ya Somalia na China yalikuwa ni makubwa. China iliwahi kutuma kikundi cha makocha kufudisha nchini Somalia. Ushirikiano katika mambo ya afya kati ya nchi hizo yalianza mwaka 1965, mwaka huo, wahudumu 10 wa afya walikwenda Somalia kufanya kazi. Hata mnamo mwaka 1991 wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoanza nchini Somalia, kulikuwa na wahudumu 19 wa afya kutoka China nchini Somalia.

Baada ya kulipuka kwa vita hivyo, wafanyakazi wa ubalozi wa China nchini Somalia, wahudumu wa afya na wahandisi wa China hawakuwa na la kufanya ila tu kuondoka, na mpaka sasa hawajarudi nchini humo. Ujumbe ulioongozwa na Balozi Zhang Ming ndiyo ujumbe wa ngazi ya juu zaidi kutoka Serikali ya China kufanya ziara nchini Somalia tangu mwaka 1991.

Ingawa Mawasiliano kati ya Somalia na China yaliathiriwa kwa kiasi fulani na vita, lakini urafiki kati yao wa tangu zamani bado unadumu. Tangu Somalia ikumbwe na vita, serikali ya China haijaacha ufuatiliaji wake hata dakika moja juu ya nchi hiyo na wananchi wake. Siku zote China inaunga mkono juhudi za jumuiya ya kimataifa na ya kikanda katika kutatua kwa amani suala la Somalia, na kushiriki kwa juhudi katika majadiliano yanayohusu Somalia katika Umoja wa Mataifa, na pia China inafanya kazi kama mratibu wa suala la Somalia katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tangu mwaka 2003 mpaka sasa. Vilevile China imetoa misaada ya kibinadamu mara nyingi kwa Somalia, hasa kwa serikali yake ya mpito tangu ianzishwe mwaka 2004. Mwaka 2006, serikali ya China inaendelea kuunga mkono serikali ya mpito ya Somalia kusukuma mbele mchakato wa amani nchini humo, huku viongozi wa nchi hizi mbili wakikutana mara kwa mara. Mwezi wa tano mwaka huu, Bw. Li Zhaoxing ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje wa China na Bw. Ismail aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Somalia walikutana jijini Beijing, na mwezi Novemba marais wa nchi hizo mbili walikutana huko Beijing tena.

Serikali ya mpito ya Somalia pia inazingatia sana uhusiano kati yake na China, inasisitiza mara nyingi kushikilia sera ya China Moja, na kueleza matumaini yake kuwa China itaweza kushiriki katika ukarabati wa Somalia. Mwaka 2005 mwezi Desemba, Bw. Mohamed Ahmed Awil alifika Beijing kuanza kazi yake kama balozi wa Somalia nchini China.

Wakati nilipokuwa nchini Somalia pamoja na balozi Zhang Ming, picha ambayo nitakumbuka kwa daima siyo majengo yenye mashimo, maduka yanayofungwa, barabara bovu wala walinzi wa amani, magari ya kijeshi, bunduki, bali ni ukarimu wa wasomalia kwa wachina. Wakati sisi tulipoingia ukumbi ulipofanyika mkutano wa maafikiano ya kitaifa, wakati balozi Zhang Ming alipotoa hotuba katika mkutano huo, washiriki zaidi ya 2000 wa mkutano huo walitukaribisha kwa kushangilia hata kuimba. Methali ya kiswahili inasema kuwa akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki, urafiki kati ya wasomalia na wachina ulianzia wakati wa shida, ndiyo sababu unaweza kudumu hadi leo. Siyo Somalia peke yake, urafiki kati ya China na nchi nyingine nyingi za Afrika ni kama hiyo.

Sasa mkutano wa maafikiano ya kitaifa ya Somalia yaani National Reconciliation Congress umemalizika, bila huhudhuriwa na makundi ya kupinga serikali, makubaliano yaliyopatikana katika mkutano huo hatuwezi kusema yana uwakilishi kamili, lakini mkutano huo mwenyewe ni hatua muhimu iliyopigwa na serikali ya mpito ya Somalia watu wa Somalia ya kuelekea amani. Wakati nilipoondoka Mogadishu niliona ukuta kadhaa zenye maneno ya kisomalia, nilitafsiriwa kwamba maneno hayo yanasema Amani ni maziwa ya mama, weka chini silaha na kujenga taifa. Tunaamini kuwa kutokana na moyo na juhudi za wasomalia, kutokana na misaada ya jumuiya ya kimataifa, Somali itaendelea kuelekea amani hatua kwa hatua.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-07