Bw. Chen Kexin ni mwongozaji wa filamu wa Hong Kong aliyepata tuzo mara nyingi zaidi, yeye pia ni mwongozaji wa filamu aliyegundua na kuwasaidia sana waongozaji filamu vijana barani Asia.
Bw. Chen Kexin ana umri wa miaka 45, aliwahi alisoma katika Chuo cha Filamu cha Los Angeles kilicho chini ya Chuo Kikuu cha California, baadaye alirudi Hong Kong, na alianza kujishughulisha na mambo ya filamu baada ya kushauriwa na baba yake. Katika wakati ambapo ushindani kwenye mambo ya filamu ulikuwa mkali, yeye pamoja na rafiki yake walianzisha kampuni ya filamu iitwayo UFO mwanzoni mwa miaka 90, kampuni hiyo ilifanikiwa kupiga filamu kadhaa zilizoonesha utamaduni wa jadi wa China. Mwaka 1994 filamu aliyoongoza utengenezaji inaitwa "He Is a Woman, She Is a Man" ilimpatia umaarufu mkubwa. Bodi ya viongozi ya kampuni ilimtaka atengeneze filamu hiyo ya mwendelezo. Alisema kama ni lazima atengeneze filamu hiyo, ni sharti akubaliwe kutengeneza filamu moja ya kimapenzi ambayo gharama yake ya utengenezaji si kubwa. Baada ya miezi minne alikamilisha filamu yake ya kimapenzi iitwayo "Utamu wa Mapenzi".
"Filamu ya 'Utamu wa Mapenzi' inaeleza kuwa katika miaka ya mwimbaji mashuhuri wa Taiwan aitwaye Deng Lijun, vijana wawili wa kike na wa kiume, Xiao Jun na Li Qiao, walivyopendana kwa muda wa zaidi ya miaka kumi. Hadithi hiyo inaeleza kuwa, vijana hao wawili walifika Hong Kong kutoka sehemu ya ndani ya China kwa garimoshi na kila mmoja alianza maisha yake mapya. Filamu hiyo inaeleza toka mwanzo jinsi walivyokutana, kufahamiana, na kuchumbiana. Lakini kutokana na sababu mbalimbali hawakuweza kuishi pamoja. Baadaye Li Qiao alifuatana na mwingine kwenda nchi ya mbali baada ya kuona kuwa mapenzi yake na Xiao Jun yamekufa, lakini kwa bahati walikutana tena kwenye mazishi ya mwimbaji Deng Lijun. Filamu inavutia kutokana jinsi mapenzi yanavyoelezwa kwa kugonga hisia za watazamaji. Filamu hiyo ilipata tuzo kubwa katika mashindano ya filamu huko Hong Kong. Watu wengi waliona kuwa filamu hiyo ambayo hadithi yake siyo ya kutatanisha kwa matuko mengi, inaweza kuvutia watazamaji namna hii, ni kama haikuongozwa na mwongozaji kijana. Bw. Chen Kexin alisema,
"Waongozaji vijana huwa na mori na mori wao hufanya filamu zao ziwe na dosari ya kueleza mambo kijujuu. Lakini mimi sina mori huo, ni kweli kwamba niliongoza filamu hiyo kama mwongozaji mzee."
Bw. Chen Kexin anaona kitu kinachomfurahisha ni kuwa watu wengi wanatizama filamu yake na kuwa na hisia za namna moja wakicheka, wakilia, ingawa wanatofautiana kwa umri wa miaka, kazi na maisha, lakini hisia za hao wote zinaguswa. Alisema hayo ndio anayotaka kuwaletea watazamaji.
Filamu hiyo ya "Utamu wa Mapenzi" ilimfanya ajulikane zaidi miongoni mwa waongozaji wa filamu huko Hong Kong. Lakini baada ya filamu hiyo Bw. Chen Kexin kwa muda mrefu hakutengeneza tena filamu. Alisema pengine aliathirika sana na filamu hiyo na hakuweza kuongoza filamu nyingine. Ili kuachana na athari ya filamu ya "Utamu wa Mapenzi" alijilazimisha kutengeneza filamu nyingine iitwayo "Labda ni Mapenzi". Hii ni filamu ya mapenzi yanayoelezwa kwa nyimbo na dansi. Alisema, alitaka kujaribu kutengeneza filamu ya aina nyingine tofauti na alizotengeneza zamani.
Filamu ya "Labda ni Mapenzi" ilipooneshwa tu mara ilipendwa sana na wapenda nyimbo na dansi. Filamu hiyo ilichangia zaidi umaarufu wake, na filamu hiyo ilimpatia tuzo nyingine. Kama mhusika mkuu katika filamu hiyo alivyosema, maisha ya binadamu humu duniani ni kama hadithi ya filamu, na wao wenyewe ndio watu wanaosimuliwa ndani ya hadithi. Alisema, anajaribu kuonesha vya kutosha maisha yao.
"Nataka kuonesha maisha ya binadamu kadiri niwezavyo na nafasi ya ninayowaachia watazamaji kufikiri zaidi ni ndogo."
Hivi sasa, Bw. Chen Kexin anatengeneza filamu nyingine ya "Ndugu wa Damu". Hii ni filamu ya kivita, Bw. Chen Kexin ambaye ana uzoefu wa kutengeneza filamu za mapenzi, hiyo ni mara yake ya kwanza kutengeneza filamu ya kivita, lakini ana uhakika wa kufanikisha filamu hiyo.
Ingawa Bw. Chen Kexin amekuwa mwongozaji wa filamu kwa zaidi ya miaka kumi na anasikia uchovu, lakini anajitahidi kuendelea na kazi yake.
"Mimi nina shughuli nyingi kuliko wengine. Sisemi hivi kwa kujivunia, bali kwa kujitahadharisha, kwa sababu mwongozaji wa filamu asipokuwa na nafasi ya kutafakari yaliyopita ili ajiendeleze, basi ataachwa nyuma. Mimi licha ya kuzongwa na mambo mengi ya kampuni na pia nasimamia upigaji wa filamu kadhaa."
Mbali na kusimamia upigaji wa filamu Bw. Chen Kexin anatumia muda mwingi kushiriki kwenye shughuli za huduma za jamii, amewagundua na kuwasaidia waongozaji vijana wengi wa Asia na yeye aliwahi kuwa msimamizi wa utengenezaji wa filamu ya Thailand ya "Mama wa Kambo" na filamu ya Korea ya Kusini "Siku Moja Nzuri ya Spring".
Idhaa ya kiswahili 2007-09-10
|