Balozi wa China nchini Cameroon Bw. Huang Changqing na waziri wa uchumi na fedha wa Cameroon Bw. Polycarpe Abah, tarehe 30 mwezi Agosti huko Yaoundé walisaini makubaliano kuhusu China kutoa mkopo wa kiserikali wenye riba nafuu wa dola za kimarekani milioni 23 kwa Cameroon, ili kuunga mkono ujenzi wa mradi wa utoaji wa maji mjini Douala.
Bw. Huang Changqing alisema, mkopo huo ni sehemu ya kutimiza ahadi iliyotolewa nchini China kwenye mkutano wa wakuu wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka 2006 hapa Beijing, pia ni kutimiza ahadi aliyotoa rais Hu Jintao wakati wa ziara yake nchini Cameroon mwanzoni mwa mwaka 2007.
Bw. Abah alisema katika miaka kadhaa iliyopita, China imekuwa inatoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya uchumi na jamii nchini Cameroon, hii inaonesha moyo wa ushirikiano kati ya kusini na kusini. Imefahamika kuwa ujenzi wa mradi wa utoaji wa maji utaanza mwishoni mwa mwaka 2007, hadi mwishoni mwa mwaka 2008 yaani mwisho wa kipindi cha kwanza cha mradi, uwezo wa utoaji wa maji katika mji wa Douala utafikia mita za ujazo laki 1.6 kutoka mita za ujazo laki 1.15 za hivi sasa, na sifa ya maji pia itaboreshwa sana.
Kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha na teknolojia, utoaji wa maji katika mji wa Douala umekuwa unakabiliwa na matatizo mengi katika miaka kadhaa iliyopita, maji ya bomba yanaweza kutumika kwa theluthi moja ya sehemu ya mji huo, na sifa ya maji ni mbaya sana. Na kutokana na kuwa tatizo la maji ya kunywa limekuwa halitatuliwi, magonjwa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kipindupindu yanaenea kwa kasi, na kila mwaka yanasababisha vifo vya watu zaidi ya 200.
*****************
Kikundi cha 16 cha madakatari wa China kilichokuwa kinatoa msaada nchini Togo kimekamilisha majukumu yake kwa mafanikio, na tarehe 30 mwezi Agosti kilirudi nchini China kutoka Lome, mji mkuu wa Togo. Madakatari wa kikundi hicho wote wanatoka mkoa wa Shanxi, China. Katika miaka miwili iliyopita, watu hao 21 walishinda taabu mbalimbali, kuonesha moyo wa kibinadamu, na kutoa huduma za matibabu kwa wakazi wa huko. Walitoa mchango mkubwa katika kuzidisha maelewano na urafiki kati ya wananchi wa China na Togo. Ufundi mzuri na moyo wao ulisifiwa na wizara ya afya ya Togo, wakuu wa hospitali na wakazi wa huko waliowahudumia.
Imefahamika kuwa kikundi cha 17 cha madakatari wa China kinachotoa msaada nchini Togo kiliwasili Lome tarehe 23 Agosti. Ubalozi wa China nchini Togo ulifanya sherehe ya kukikaribisha kikundi kipya na kukiaga kikundi cha 16 kurudi nyumbani. Balozi wa China nchini Togo Bw. Yang Min na waziri wa afya wa Togo Bw. Charle Agba walihudhuria sherehe hiyo na kutoa risala.
China imetuma vikundi vya madaktari nchini Togo kwa miaka zaidi ya 30, na madaktari kutoka China wanasifiwa na wananchi wa Togo. Hivi sasa madaktari wa kikundi cha 17 wameanza kufanya kazi nchini Togo.
****************
Waziri wa kilimo wa China Bw. Sun Zhengcai tarehe 31 mwezi Agosti aliwasili nchini Ethiopia kwa ziara. Wakati wa ziara yake hiyo, Bw. Sun Zhengcai alifanya mazungumzo na naibu waziri mkuu wa Ethiopia ambaye pia ni waziri wa kilimo na maendeleo ya vijiji vya nchi hiyo Bw. Addisu Legesse. Kwenye mazungumzo hayo Bw. Addisu alisema Ethiopia inapenda kuimarisha zaidi ushirikiano wa kilimo kati yake na China, ili kuinua kiwango chake cha kilimo na uzalishaji wa nafaka.
Bw. Addisu alipokutana na waziri wa kilimo wa China Bw. Sun Zhengcai alisema, China ina uzoefu mkubwa katika elimu ya ufundi wa kazi ya kilimo, uzalishaji wa mazao ya kilimo unaofuata vigezo, kuendeleza soko la kimataifa na teknolojia ya kilimo cha bustani inayostahili kuigwa na nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Ethiopia.
Bw. Addisu hasa alitaja ushirikiano kati ya China na Ethiopia katika mradi wa elimu ya ufundi wa kazi ya kilimo. Alisema walimu kutoka China waliwafundisha wataalamu wa kilimo wa Ethiopia ufundi muhimu wa kilimo, na kuhimiza maendeleo ya elimu ya kazi ya kilimo nchini humo.
Bw. Sun Zhengcai alisema hatua nane za ushirikiano kati ya China na Afrika zilizotangazwa na Rais Hu Jintao wa China kwenye mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana, ni mwelekeo wa ushirikiano wa kilimo kati ya China na Ethiopia. Wizara ya kilimo ya China itaendelea kushirikiana na wizara ya kilimo na maendeleo ya vijiji ya Ethiopia, na kuhimiza maendeleo ya ushirikiano na maingiliano kati ya nchi hizo mbili katika sekta ya kilimo.
Tarehe 1 mwezi Septemba, waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Meles Zenawi alikutana na Bw. Sun Zhengcai. Bw. Meles alisema maendeleo ya uchumi wa Ethiopia yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni yanahusiana na ushirikiano uliopo kati ya Ethiopia na China. Bw. Zenawi alisema, nchi hizo mbili zina ushirikiano katika sekta mbalimbali. Ushirikiano kati yake na China unainufaisha sana Ethiopia, na ana matumaini kuwa ushirikiano huo utaendelea. Alisema China inafanya kazi kubwa kusaidia Ethiopia kupunguza umaskini. Teknolojia ya kilimo na uzoefu wa uzalishaji wa kilimo wa China vinahimiza maendeleo ya uchumi wa Ethiopia.
Bw. Sun Zhengcai alisema ushirikiano katika kilimo kati ya China na Ethiopia umepata mafanikio makubwa. China inaisaidia Ethiopia kujenga kituo cha vielelezo vya teknolojia ya kilimo, ili kutoa mafunzo kwa Ethiopia na kuhimiza matumizi ya teknolojia ya kilimo ya China, na kuinua kiwango cha uzalishaji wa nafaka ili kuboresha maisha ya wakulima wa sehemu hiyo.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-14
|