Msikilizaji wetu Paul Mungai Mwangi wa sanduku la Posta 69 Injinia, Kenya, ametuletea barua yake ambayo anasema kwanza anapenda sisi na wasikilizaji wote tupokee salamu zake kupitia Radio china katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Pia anapenda shukurani zake ziwafikie wasikilizaji wote wa Radio china kimataifa kwa kuungana pamoja kama familia moja ya CRI.
Anasema yeye akiwa huko Injinia, Kenya anaona fahari kubwa kuwa mwanachama wa Radio China kimataifa na kusikia salamu zake zikisomwa hewani katika kituo hiki na watangazaji wa kimataifa. Anawaomba wasikilizaji wenzake waendelee kuiboresha Radio China kimataifa kwa kutoa maoni na mapendekezo. Anapendekeza Radio China kimataifa tutoe fulana maalumu, ambazo tutawatumia wasikilizaji wetu wote, ili wakivaa iwe njia mojawapo ya kuwavutia wasikilizaji zaidi.
Pia anapendekeza tuongeze nafasi maalumu kwa ajili ya washindi wa chemsha bongo ili kuwapa nafasi wasikilizaji wengi zaidi wa CRI kutembelea China. Mwisho anawasalimia wafuatao: Ayub mutanda wa Bungoma, Kenya Manko Ngogo wa Tarime, Tanzania, Mbaruk msabaha wa Dubai Falme za Kiarabu, na wazazi wake Mwangi Gichimu na Margaret wakiwa Injinia. Anawaomba wasikilizaji hao aliowasalimia wamtumie picha.
Tunamshukuru kwa dhati Paul Mungai Mwangi na wasikilizaji wengine wanaotuletea barua kueleza maoni na mapendekezo yao, tutazingatia kwa makini, kama ikiwezekana tutarekebisha kazi husika kwa kufuata mapendekezo ya wasikilizaji wetu.
Msikilizaji wetu Bwana Ali Hamisi Kimani wa sanduku la Posta 34 Ndori, nchini Kenya ametuandikia barua akisema ana matumaini kuwa ni wazima sana na tunaendelea kuchapa kazi barabara. Anasema yeye na familia yake ni wazima wa afya njema na wanaendelea kusikiliza na kufurahia vipindi na matangazo yetu. Anasema anatushukuru sana kutokana na jitihada zetu za kuhakikisha tunaendelea kuwasiliana kila mara kwa kumtumia kadi za salamu, bahasha zilizolipiwa, picha za maua na ndege na kadhalika. Picha zinazoonyesha uwanja utakaotumika kwa ajili ya michezo ya olimpiki mwaka 2008 mjini Beijing, zinampa hamu ya kuitembelea China. Anaamini kuwa siku moja atafanikiwa kutembelea China.
Pia amefurahishwa na mbinu tunazotumia kuhakikisha kuwa tunatangaza salamu za wasikilizaji wengi kadiri inavyowezekana, na tulivyoboresha kipindi cha Jifunze kichina kiasi kwamba sasa kila mtu anaweza kufuatilia vizuri na kwa urahisi. Anatarajia kuwa vipindi vingine tutavishughulikia ipasavyo. Mwisho anamaliza barua yake akiwa na matumaini kuwa ombi lake la kupata jarida la urafiki na kutumiwa majibu sahihi ya chemsha bongo ya mwaka 2006 tutalishughulikia.
Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija wa sanduku la posta 1067 Kahama Shinyanga, Tanzania ametuletea barua anasema ana matumaini makubwa kuwa sote hatujambo, na yeye huko aliko Kahama, Shinyanga, Tanzania hali yake ni nzuri. Na anaendelea kuitegea sikio radio yao pendwa ambayo ni Redio China Kimataifa.
Anapenda kutumia fursa hii kutu\oa maoni yake kuhusu usikivu wa matangazo yetu huko Shinyanga. Anasema anasikitika kuwa huko Shinyanga matangazo yetu yanasikika kwa taabu. Ombi lake ama kilio cha wasikilizaji wa Radio China kimataifa walioko Tanzania, bado wanaendelea kuwaomba wahusika wa Redio China Kimataifa kuwa matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya CRI yawekwe kwenye masafa ya FM kupitia Redio Tanzania Dar es salaam pamoja na Sauti ya Tanzania Zanzibar.
Yaani usikivu wa matangazo ya CRI idhaa ya Kiswahili hapo Kahama Shinyanga ni mgumu sana matangazo yanafika kwa shida sana, afadhali alipokuwa katika mkoa wa Mwanza, ambako usikivu wa matangazo ya CRI ulikuwa mzuri kidogo. Labda kwa kuwa mkoa wa Mwanza uko karibu na Kenya na labda ni kutokana na Radio China kimataifa kuwa kituo cha masafa ya FM huko Kenya. Mwisho anawaomba wasikilizaji wenzake akina Ayub Mutanda Shariff, Mbarouk Msabaha, Kassim Abed Ngea, Mogire Machuki, Gulam Haji karimu, Ras Franza Manko Ngogo, Geoffrey Njereka, Mussa Emanuel Duttu, Yakubu Said Idambila pamoja na wengineo wote waliopo sehemu mbalimbali duniani ambao hakuwataja majina yao, waendelee kutoa michango yao katika idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa katika vipindi vya sanduku la barua, salamu zenu pamoja na vipindi vinginevyo vinavyotangazwa na idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa.
Tunamshukuru sana Bwana Stephen Magoye Kumalija kwa barua yake ya kutueleza hali ya usikivu wa matangazo yetu kwenye sehemu anakoishi. Kweli wasikilizaji wetu wa Tanzania wengi wametuletea barua wakilalamikia hali hiyo. Tunasikitishwa sana na hali hiyo, na mara kwa mara tumefikisha maoni ya wasikilizaji wetu kwa ofisi husika, tena tunafanya juhudi kwa kila tuwezalo, hasa hivi karibuni balozi mpya wa China nchini Tanzania atafunga safari kwenda huko, tulikutana naye na kumwomba atusaidie kuwasiliana na Radio Tanzania Dar es Salaam, hali kadhalika kwa maofisa wa idara mbalimbali za Tanzania waliokuja China kwa ziara, pia tumewaomba wajitahidi kutusaidia kuhimiza ushirikiano kati yetu na Radio Tanzania Dar es Salaam. Na ushirikiano kati ya Radio China kimataifa na Radio ya Zanzibar hauna tatizo, baada ya kukamilisha mradi husika unaojengwa kwa msaada wa wizara ya biashara ya China, ushirikiano kati yetu utaanza mara moja. Kwa hivyo sasa tunaweza tu kuwaomba wasikilizaji wetu mtuvumilie na kutuelewa, iko siku hali ya usikivu itaboreshwa.
Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija anasema katika barua yake nyingine kuwa, anapenda kutumia fursa hii ili kuwapa pole sana marafiki zake wa sehemu ya kusini mwa China waliokumbwa na mafuriko, ambako watu wengi walikufa kutokana na mafuriko hayo, na zaidi ya watu wapatao laki sita wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na maporomoko ya ardhi pamoja na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizokuwa zinazoendelea kunyesha katika mikoa ya kusini mwa nchi ya China.
Hususan katika sehemu hii ya pili anapenda kutumia fursa hii ili kumpongeza rais wa Jamhuri ya Watu wa China bwana Hu Jintao kwa kuhudhuria mkutano wa nchi zilizo tajiri kiviwanda duniani yaani G 8 huko Ujerumani, ambapo alihudhuria mkutano huo kama msikilizaji.
Anasema pia anaomba vipindi vya sanduku la barua na kuwa nami jifunze kichina pamoja na kipindi cha elimu na sayansi viongezwe muda, pia kama ikiwezekana matangazo yote ya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa. Matangazo ya Kiswahili yarushwe hewani kwa kupitia Redio Tanzania Dar es salaam na pamoja na Sauti ya Tanzania Zanzibar, ana amini kuwa tukifanya hivyo nasi wasikilizaji wetu kutoka Tanzania bara na Tanzania visiwani watapata usikivu mzuri zaidi siku hadi siku. Ni matumaini yake kuwa tutaendelea kuwaletea habari muhimu na nyeti kutoka sehemu mbalimbali duniani kutoka hapa idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa, vilevile pia na wao wasikilizaji wa Redio China Kimataifa kutoka kila pembe hapa ulimwenguni wataendelea kutuma barua na maoni pamoja na mapendekezo, ili kuboresha matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Redio China Kimataifa. Anamaliza barua yake kwa kuomba atumiwe magazeti mbalimbali ya China Today, kadi za salamu na bahasha zilizolipiwa gharama za stempu.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-11
|