Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-17 15:50:28    
Uzuri wa mji wa Kashi wanakoishi Wa-uygur mkoani Xinjiang

cri

Mji wa Kashi mkoani Xingjiang ni mji wanakoishi  watu wa kabila la Wa-uygur. Huu ni mji uliowekwa chini ya hifadhi ya taifa kutokana na kuwa na historia ndefu. Watu husema kama ukitembelea mkoa wa Xinjiang bila kufika mji wa Kashi ni sawa na bure.

Wakazi wanaoishi katika mji huo wengi zaidi ni wa kabila la Wa-uygur, na mila na desturi za wakazi hao zinaonekana zaidi katika uwanja wa Etigar uliopo katikati ya mji huo. Huu ni uwanja wenye eneo kubwa lenye maua, ni mahali ambapo wakazi wanapumzika, kufanya sherehe kubwa na mikutano ya halaiki. Watu wanaofurika katika uwanja huo karibu wote ni Wa-uygur, baadhi wanakaa kwenye kingo za eneo la maua na baadhi wanafanya biashara ambao wanatangaza biashara zao kwa matamshi yasiyo sanifu ya lugha ya Kichina.

Pembezoni mwa uwanja huo kuna vibanda vingi vya kuuzia vitu vya sanaa vya kikabila, hasa mapambo ya nguo. Kofia ndogo zilizotariziwa kwa ajili ya wanaume na wanawake, wazee na watoto zinaonekana kila mahali. Katika duka moja la kofia, muuzaji ni msichana wa Kiuygur, anaitwa Aysha, alitueleza,

"Sisi Wa-uygur wasichana tuna mila ya kuvaa sketi ndefu kwa nje na kuvaa suruali ndefu kwa ndani, watoto huvaa kofia ndogo na wanawake wanavaa hijabu."

Wasichana  licha ya kupenda kuvaa kofia ndogo, na pia wanapenda kusuka nywele kwa mikia mingi hadi kumi kadhaa, na kuchomeka kitana chenye umbo la mwezi mchanga kwenye nywele zao. Kuhusu mikia hiyo Bi. Aysha alisema,

"Kwa kawaida wasichana watoto husuka mikia 19, 21, au 41. 41 ni tarakimu inayopendwa kwa sababu ni tarakimu iliyo kwenye Kurani, lakini wanawake walioolewa wanaruhusiwa kusuka mikia miwili tu."

Watu wa kabila la Wa-uygur wanapenda kuvaa mapambo, kwa mfano mkufu uliotengenezwa kwa mfupa na kuwa na kisu kiunoni. Kwenye duka moja la mapambo, muuza duka kijana aitwaye Mehmetcan alitushawishi tununue kisu kiitwacho Enjisha. Alisema,

"Kisu cha Enjisha kimetengenezwa kwa ufundi mkubwa wa mikono. Katika mji wa Kashi kuna wilaya moja iitwayo Enjisha, katika wilaya hiyo wenyeji karibu wote ni mafundi wa kutengneza visu hicho."

Ufundi wa kutengeneza visu ni wa hali ya juu, na kwenye mpini wa kisu inawekwa shaba, mifupa au fedha kwa nakshi za kikabila. Bw. Mehmetcan alisema kisu kama hicho licha ya kuwa ni pambo, pia kina matumizi mengi.

"Kisu hiki kinatumika katika kuchinja mbuzi, kukata nyama, na wakati unapokula nyama choma unakata mwenyewe. Wanawake wa kabila la Wa-uygur wana tabia ya kutembea na kisu hiki kila wakati."

Chakula cha Wa-uygur kina utamaduni wake. Chakula kisichoweza kukosekana kwa Wa-uygur ni nyama choma. Aina za nyama choma ni nyingi na mshikaki ni nyama ya kawaida, na mbuzi mzima wa kuchomwa ni nyama ya kifahari. Katika hoteli kubwa chakula hicho ni cha lazima kwa ajili ya kuwakaribisha wageni wa heshima.

Pilau pia ni chakula kingine cha lazima katika hoteli. Kuhusu mapishi ya pilau mhudumu wa hoteli alisema,

"Pilau inapikwa kwa mchele na nyama ya mbuzi pamoja na viungo vya mdalasini, iliki, pilipili na karoti. Watu wanakula kwa kutumia vidole vitatu vya mkono wa kulia."

Mhudumu huyo alituambia inasikitisha kama tusipokula aina moja ya chapati mkoani Xinjiang inayoitwa Nang. Nang ni chapati kubwa na nene inayoumuka kwa kuokwa, umbo lake ni duara na juu yake huchomwa vitundu vidogo vidogo na kutiwa nakshi.

Baada ya kueleza chakula muhimu kwa Wa-uygur sasa tuje kwenye muziki wa kabila hilo. Kwenye duka moja la ala za muziki, kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa anapiga muziki kwa ala ya kikabila.

Watu wa kabila la Wa-uygur wanatumia muziki, fasihi na dansi kueleza maisha yao ya furaha na matumaini yao, na muziki wao ni wa pekee katika aina zote za muziki wa kikabila duniani.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-17