Ni watangazaji wenu Chen na Fadhili Mpunji tunawakaribisha katika kipindi hiki cha Sanduku la barua. Leo tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.
Msikilizaji wetu Richard Chenibei Mateka wa sanduku la Posta 65 Kapkateny, mlima Elgon, Kenya ametuandikia barua akianza kwa kutusalimu na kututakia kila la heri katika kazi za kila siku hapa Radio China kimataifa. Anasema lengo la barua yake ni kutaka kutueleza machache kuhusu mlima Elgon. Japokuwa kumekuwa na mivutano ya kugombea ardhi katika wilaya ya Elgon baina ya koo na pia kuna tatizo la upungufu wa chakula, lakini anasema hayo yasiwafanye watalii kutoka nje wawe na wasiwasi wanapotembelea mlima Elgon. Anaomba Radio China Kimataifa na vyombo vingine vya habari pamoja na mashirika ya haki za binadamu wasisite kutembelea eneo hilo.
Pia anawaomba viongozi wa karibu watembelee eneo hilo ili watoe maoni yao. Watalii kutoka nje wanapotembelea katika eneo hilo, hawapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu suala la usalama anasema katika wilaya ya mlima Elgon na ofisi zote, kazi za utalii zinaendelea kama kawaida. Na kwa upande wa matangazo ya Radio Kichina Kimataifa, anasema usikivu wa matangazo ni mzuri, hivyo tuko pamoja nao. Anamaliza barua yake kwa kutushukuru na kuwa na matumaini kuwa tutazingatia maoni yake, na kama tunataka kujua mengi kutoka huko Elgon, basi yuko tayari kutueleza.
Msikilizaji mwingine ni Yakub Saidi Idambira wa Klabu ya wasikilizaji wa Kakamega, sanduku la Posta 2519, Kenya, ameanza barua yake kwa kutusalimu watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Anasema ametuletea barua akitaka kutufahamisha kuwa amepokea Jarida la China today tulilomtumia, hivyo anashukuru sana kwa kumtumia zawadi hiyo ambayo anasema imemfanya ajifunze mambo mengi yenye manufaa yakiwemo ya uchumi, jamii na sayansi na Teknolojia.
Pia anapenda kutoa shukurani kwa wafanyakazi wote wanaoandaa jarida la China today kwa kazi yao nzuri na kwa utafiti wanaofanya katika kuwachapishia wasomaji kila wanachohitaji kukisoma. Anasema jarida hilo tulilomtumia lina masuala mbalimbali na hasa kuhusu taifa la China na kueleza sera za kimataifa. Ana matumaini kuwa kwa kupitia jarida la China today, wasomaji wengi wamelifahamu taifa la China kwa karibu zaidi.
Hivyo anawapa moyo wafanyakazi wa jarida la China today kuendeleza na kutekeleza majukumu yao ya kujenga uhusiano mwema kwa kuwapa habari wasomaji walio wengi kuhusu masuala mbalimbali zaidi. Anatoa ushauri kuhusu wahusikia wafikirie kuanzisha toleo la Kiswahili kwa ajili ya wasomaji na wazungumzaji wa Kiswahili, kwani kwa kuchapisha toleo hilo watawafikia wasomaji wengi walioko mijini na vijijini hivyo, ni matumaini yake kuwa tutawafahamisha wahusika.
Kwa upande wa Radio China Kimataifa anasema anaomba tuanzishe utaratibu wa kuwatumia CD na DVD ili waweze kusikiliza na kutazama vipindi mbalimbali vya Radio China kwa urahisi na kwa njia hiyo anasema wasikilizaji wengi watanufaika kwa haraka na kwa muda mfupi. Itakuwa ni mwanzo mzuri tukituma CD na DVD moja moja kwa kila klabu ya wasikilizaji
Anaomba CD na DVD hizo ziwe na vipindi vya kuigiza, jifunze kichina, mahojiano na wasikilizaji na muziki na nyimbo mbalimbali kutoka Afrika na China na mafunzo ya tamaduni za China. Mwisho anasema matumaini yake ni kuwa mapendekezo yake tutayapa umuhimu mkubwa na anatutakia ufanisi na baraka katika kazi zetu za kuwahudumia vizuri katika miaka yote.
Tunamshukuru Yakub Saidi Idambira kwa barua yake ya kutuelezea maoni yake kuhusu jarida la China ya leo, ni matumaini yetu kuwa, kama wasikilizaji wetu mnakuwa na maswali baada ya kusoma jarida la China today, mnaweza kutuletea maswali hayo na tutayajibu, ili tuweze kuwasaidia kuongeza ufahamu juu ya hali ya nchini China. Na kuhusu ombi lako la kutuma CD au DVD, ombi lako limefika. Lengo la Radio China kimataifa ni kufanya matangazo yake yawafikie wasikilizaji wengi kadiri iwezekanavyo na kwa njia nyingi, kwa hiyo wakati ukifika unayoomba yataweza kufanyika
Msikilizaji wetu wa sasa ni Bw. Mbarak Mohamed Abucheri wa sanduku la Posta 729 Kakamega, Kenya, yeye kwenye barua yake ameanza kwa salamu kwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa na kututakia kila la kheri tunapofanya kazi ya kuwahudumia kwa upekee na kiustadi. Anatushukuru na kutupongeza kwa kazi yetu nzuri. Pia anapenda kuushukuru uongozi wa Radio China Kimataifa kwa kurefusha muda wa Mama Chen, kutokana na uhodari na utaalamu wake katika kutekeleza wajibu wa kuendeleza na kuipeleka mbele Radio China Kimataifa katika nyanja ya utangazaji.
Anasema hatua hii iliyochukuliwa na uongozi wa Radio China Kimataifa ni muhimu na ya busara nyingi, na hasa ikizingatiwa kuwa Mama Chen ana uzoefu wa miaka mingi katika mambo ya utangazaji na usimamizi. Kutokana na usimamizi wake anasema hadhi ya matangazo ya Kiswahili ya Radio China kimataifa imeongezeka na kufikia kiwango cha kimataifa.
Wasikilizaji wanapokea kila wanachohitaji, kwa maana ya masuala ya kijamii, kisiasa, kiuchumi, sayansi na teknolojia, utamaduni, michezo na mengine mengi. Hivyo basi kuongeza muda wa Mama Chen ni mchango mkubwa kwa watangazaji chipukizi kupata nafasi ya kujifunza kutoka kwa Mama Chen. Kwa watangazaji chipukizi anasema iwe changamoto kwao kujifunza kutoka kwa Mama Chen ili wapate ujuzi na taaluma ya utangazaji na kuandaa vipindi kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya wasikilizaji.
Akiwa mmoja wa wasikilizaji anapenda kuona taaluma hiyo yenye umuhimu inarithiwa, mwisho anamaliza barua yake kwa kutoa ombi la kuanzishwa kipindi cha kupokea maoni kutoka kwa wasikilizaji kuhusu huduma wanazotoa watangazaji ili wasikilizaji waweze kumchagua mtangazaji bora wa mwaka na hivyo kuleta ushindani katika kazi. Kwa wale wasikilizaji wanaotoa maoni, mapendekezo na mawazo mazuri nao wapewe tuzo, lakini pia, watangazaji wapewe nafasi ya kuchagua wasikilizaji au msikilizaji aliyetoa maoni, mapendekezo na mawazo mazuri ambayo yametekelezwa na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha vipindi vya Radio China kimataifa.
Anasema kwa kubuniwa na kuanzishwa kwa kipindi hiki kutasaidia kuondoa mazoea ya wasikilizaji ya kutegemea tu chemsha bongo kwa ajili ya kupata ushindi wa nafasi maalumu wenye nafasi chache za kuitembelea China.
Tunakushukuru sana Bw Mbarak Mohamed Abucheri kwa maoni na mapendekezo uliyotoa. Tumefurahishwa na maoni yako ya kuwa na mbinu nyingine za kuwafanya wasikilizaji wawe na njia nyingi za kuongeza ujuzi wa kuifahamu China mbali na chemsha bongo. Mbali na kipindi cha chemsha bongo, kila mara tunawatumia wasikilizaji wetu majarida yanayozungumzia mambo mbalimbali kuhusu China, ili wafahamu zaidi China. Wazo lako ni zuri tunakubaliana nalo, tutajitahidi liwafikie wahusika.
Msikilizaji wetu mwingine ni Stephen Magoye Kumalija wa sanduku la Posta 1067 Kahama, Shinyanga Tanzania, anasema kwa furaha kubwa ana matumaini kuwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa hatujambo. Kwa upande wake anasema ni mzima na anaendelea kusikiliza Radio China Kimataifa kwa habari muhimu kote duniani. Ametuandikia barua hii ili kutoa shukurani nyingi za dhati kwa serikali ya jamhuri ya watu wa China kwa kuzindua mtambo mkubwa wa satellite huko Nigeria wenye thamani ya dola za kimarekani milioni mia tatu. Mtambo huo uliowekwa nchini Nigeria, utaisaidia sana Nigeria na wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wanapata shida sana kufanya mawasiliano kwa njia ya simu.
Vile vile anatoa shukurani zake kwa Radio China Kimataifa kwa kuendelea kumtumia bahasha zilizolipiwa gharama za stempu, kadi za salamu pamoja na kalenda ya mwaka huu. Kwa kumaliza barua yake anaomba tumtumie magazeti yanayochapishwa katika lugha mbalimbali. Na katika barua yake nyingine fupi anasema anaomba kitengo cha mafunzo ya lugha ya kichina ichapishe kitabu cha kuwa nami jifunze kichina na kitabu hicho tuwatumie wasikilizaji ambao wana nia ya kujifunza lugha ya kichina.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-18
|