Mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China unajulikana kwa kuwa na eneo kubwa la mbuga na uchumi unaotegemea mifugo. Watu wakisikia kuhusu mkoa huo, wanapata taswira ya anga ya kibuluu, nyasi za rangi ya kijani, na wakazi wa huko ambao wengi ni wa kabila la Wamongolia wanaochunga mbuzi huku wakiimba. ..
Katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa halijoto duniani, ongezeko la kasi la idadi ya watu, na shughuli za binadamu, sehemu ya mbuga kwenye mkoa huo imeanza kupoteza rutuba na kubadilika kuwa jangwa. Hali hii imewafanya wakazi wa huko waanzishe juhudi za kuokoa maskani yao.
Kijiji cha Aolike ni kijiji kidogo kilichopo kwenye mbuga ya Xilinguole, kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ambapo wakazi wa huko ni wafugaji wanaohamahama. Tangu miaka ya 90 ya karne iliyopita, mbuga ya huko ambayo ni tegemeo la wafugaji ilianza kubadilika kuwa jangwa. Katika kipindi cha miaka kadhaa tu, jangwa liliimeza kabisa mbuga.
Mfugaji Namuhai wa kabila la Wamongolia ni mkazi wa kijiji hicho, alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, walikuwa wanashindwa kuendelea kuishi kwenye jangwa.
"Wakati huo asilimia 70 ya ardhi ya kijiji chetu ilibadilika kuwa jangwa, hatukuweza kuchunga mifugo, hata ilikuwa vigumu kupata maji safi ya kunywa. Tulifuga mifugo kwenye ardhi yenye mchanga, pato la wastani la mtu mmoja mmoja kwa mwaka halikufikia Yuan elfu 1, na kiwango cha maisha ya wafugaji kilishuka. Kama tungeendelea kuishi kwenye ardhi yenye mchanga, tungekabiliwa na tatizo la njaa."
Katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, kijiji cha Aolike si kijiji pekee kilichokumbwa na tatizo la jangwa. Mwaka 2002 serikali ya mkoa huo ilianza kutekeleza sera ya kuwahamisha wakazi wanaoishi kwenye sehemu zilizoathirika na jangwa, na kupanda mimea kwenye sehemu hizo. Kutokana na misaada ya serikali, wafugaji walinunua ng'ombe kwa kutumia mikopo, na wakaanza kufuga ng'ombe kwenye mazizi na kuzalisha maziwa.
Hivi sasa Bw. Namuhai na familia yake wanaishi kwenye nyumba ya matofali iliyojengwa na serikali. Alimwambia mwandishi wa habari kuwa, familia yake sasa ina pato la Yuan elfu 40 kwa mwaka. Kitu kinachomfurahisha zaidi ni kuwa, zamani akitoka nje alikuwa anasumbuliwa na mchanga, sasa usumbufu wa namna hiyo haupo tena. Na wajukuu zake wanaweza kuendelea na masomo shuleni, na ni rahisi kwa jamaa zake kwenda hospitali.
Hivi sasa ardhi yenye mchanga alipoishi Bw. Namuhai ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa kuboresha mazingira ya asili uliotungwa na serikali ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani. Katika ardhi hiyo, mbali na wakazi wa huko kuhamishwa, shughuli za ufugaji pia zinapigwa marufuku, na miti inapandwa.
Ofisa anayeshughulikia mazingira ya asili ya huko Bibi Li Shuping alisema "Hatua ya kwanza ni kupiga marufuku shughuli za ufugaji, halafu hatua nyingine tofauti zinachukuliwa kutokana na hali tofauti ya ardhi zilizoathirika na jangwa. Tunapanda mimea kwenye ardhi hizo."
Baada ya kuhama, mwanzoni Bw. Namuhai aliwahi kurudi maskani yake akisaidia kazi ya kupanda mimea. Katika miaka kati ya miwili au mitatu tu, hali ya mbuga ili boreshwa sana.
Takwimu zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2001 na 2006, kwenye mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, hekta milioni 16.67 za ardhi zilizoathirika na jangwa zilishughulikiwa, vile vile maeneo 19 ya mfano wa mazingira ya asili na maeneo 125 ya kuhifadhi mazingira yalianzishwa.
Kwenye mchakato wa kushughulikia jangwa, wakazi wa mkoa huo pia wamepata mbinu mpya ya kujiongezea mapato, mbinu hiyo ni kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa kutumia miiba ya manjano, ambayo ni aina ya mimea inayohimili ukame. Bidhaa hizo ni pamoja na chakula, viungo na vinywaji.
Kampuni ya vyakula vya Tianjiao ni moja ya kampuni zinazotengeneza bidhaa hizo. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Li Yunfei alieleza kuwa, miiba ya manjano ni mimea maalumu inayopandwa ili kuzuia ardhi isibadilike kuwa jangwa na kuzuia maporomoko ya mawe na udongo. Awali serikali ya huko ilikuwa inatenga fedha nyingi kila mwaka kwa ajili ya upandaji wa mmea huo, hatua ambayo ilileta manufaa ya kuboresha mazingira ya asili, na hivi sasa kampuni hiyo imezidi kupata ufanisi wa kiuchumi kutokana na kutengeneza bidhaa kwa kutumia mmea huo.
Bw. Li Yunfei alisema "Mmea huo una virutubisho vya aina zaidi ya 300 vinavyosaidia kujenga afya kwa binadamu. Kutokana na utengenezaji, tunazalisha vyakula vyenye virutubisho na bidhaa hizo zinauzwa vizuri sokoni."
Meneja mkuu huyo aliongeza kuwa, wafugaji na wakulima wengi wa huko wanaopanda mmea wa miiba ya manjano pia wameongezewa uwezo kutokana na shughuli za kampuni yake za kutengeneza bidhaa kwa kutumia mmea huo. Na wafugaji na wakulima wakishapata faida, wanatiwa moyo katika kilimo cha mmea huo, hali ambayo inahimiza kuboreshwa kwa mazingira asili ya huko.
Hivi sasa sekta ya uchumi wa mimea inayohimili ukame imepata maendeleo makubwa katika mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, ambapo wakazi wa huko wamepata manufaa ya kimazingira na faida za kiuchumi.
Idhaa ya kiswahili 2007-09-20
|