Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-09-24 15:21:02    
Maonesho ya kimataifa ya vitabu mjini Beijing

cri

Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu mwaka 2007 mjini Beijing yalimalizika hivi karibuni kwa mafanikio makubwa, wachapishaji kutoka nchini na nchi za nje walikuwa na pilikapilika nyingi wakati wa maonesho hayo. Hayo ni maonesho kabambe ambayo wadau wa China na wa nchi za nje wanaona maonesho hayo ni jukwaa muhimu la mawasiliano ya kiutamaduni kati ya China na nchi za nje.

Maonesho ya kimataifa ya vitabu yalifanyika kuanzia tarehe 30 Agosti hadi tarehe 3 Septemba mjini Beijing. Mashirika ya uchapishaji zaidi ya 1,400 kutoka nchi na sehemu 58 yalishiriki kwenye maonesho hayo. Miongoni mwa mashirika hayo licha ya mashirika maarufu duniani kama vile kundi la uchapishaji John Wiley la Marekani na kundi la uchapishaji Elsevier la Singapore, pia kulikuwa kuna mashirika mengi kutoka nchi za Asia na Afrika, zikiwemo Bangladesh, Oman, Afrika Kusini, Umoja wa Falme za Kiarabu, Azerbaijan na Uzbekistan ambapo ilikuwa ni mara ya kwanza kwao kushiriki kwenye maonesho hayo.

Mkurugenzi wa Idara Kuu ya Usimamizi wa Uchapishaji nchini China ambayo ni moja ya waandaaji wa maonesho hayo Bw. Liu Binjie kwenye ufunguzi alitoa makaribisho makubwa kwa washiriki wa maonesho hayo. Alisema,

"Maonesho ya kimataifa ya vitabu mjini Beijing ni fursa nzuri kwa wachapishaji kuwasiliana, kushirikiana na kupeana uzoefu. Ni matumaini kuwa washiriki watatumia fursa hiyo vya kutosha kufanya biashara ya haki za kunakili, maingiliano ya shughuli za uchapishaji na kubadilishana uzoefu ili kustawisha sekta ya uchapishaji duniani."

Tokea Maonesho ya Kimataifa ya Vitabu mjini Beijing yafanyike mwaka 1986, kiwango chake kimekuwa kinaongezeka mwaka hadi mwaka. Mwaka huu eneo la maonesho lilifikia mita za mraba elfu 34, ambalo ni ongezeko la 30% kuliko mwaka uliopita, aina laki moja za vitabu zilioneshwa kwenye maonesho hayo. Kiwango hicho ni kikubwa kuliko maonesho yote yaliyopita.

Mashirika 42 ya uchapishaji kutoka Ujerumani yalishiriki kwenye maonesho na aina za vitabu 1,500, na yalifanya "wiki ya vitabu ya Ujerumani" katika maduka makubwa ya vitabu na sehemu nyingi za utamaduni mjini Beijing. Waziri wa utamaduni wa Ujerumani Bw. Bernd Neumann alisema,

"Tunaona fahari kushiriki kwenye maonesho haya, tutatumia nafasi hii kuwafahamisha watu wa China utamaduni na fasihi ya Ujerumani."

Bw. Neumann alieleza kuwa kati ya nchi zinazonunua haki za kunakili kutoka Ujerumani, China ilikuwa katika nafasi ya 10 tokea mwaka 1997, lakini kuanzia mwaka 1998 hadi 2000 China imekuwa katika nafasi ya kwanza. Kwa hiyo maonesho ya kimataifa ya vitabu mjini Beijing yana umuhimu mkubwa kwa Ujerumani."

Katika maonesho hayo licha ya China kuingiza vitabu kutoka nchi za nje, pia ilifanya shughuli nyingi za kutangaza duniani mashirika ya uchapishaji ya China. "Kongamano la Kimataifa kuhusu Uchapishaji" liliwashirikisha wachapishaji zaidi ya 300. Naibu mkuu wa kampuni ya Amazon.com ya Marekani Bw. Diego Piacentine kwenye kongamano hilo alisema, anafurahia mchango wa kampuni yake katika shughuli za kueneza vitabu vya China duniani. Alisema,

"Ili kukidhi mahitaji ya vitabu vya China yanayoongezeka siku baada siku, tumeanzisha tovuti ya Amazon.com, na hivi sasa tumekuwa na aina za vitabu vya Kichina elfu 80, na idadi hiyo inaendelea kuongezeka."

Miaka miwili iliyopita, China ilianza kutekeleza mpango wake wa kusambaza vitabu vyake katika nchi za nje, na inahamasisha mashirika ya nchi za nje yatafsiri na kuchapisha vitabu vya China kwa kutoa msaada wa fedha. Kwenye maonesho hayo vitabu vya China zaidi ya 1,000 vilichaguliwa ili mashirika ya nchi za nje yachague, na kwa mara ya kwanza ilialika washauri 12 wa nchi za nje kusaidia shughuli za uenezi wa vitabu vya China duniani.

Katika maonesho hayo, Wataalamu wa lugha ya Kichina wa Ujerumani Bw. Kubin Wolfgang na wengine wawili walipata tuzo ya Idara Kuu ya Usimamizi wa Uchapishaji nchini China. Tuzo hiyo inatolewa kwa watu wa nchi za nje waliotoa mchango mkubwa katika kuchapisha na kutafsiri vitabu vya China na kustawisha maingiliano kati ya China na nchi za nje. Bw. Kubin Wolfgang ni profesa wa Chuo Kikuu cha Bonn, mbali na kuandika vitabu vingi kuhusu fasihi ya China alichapisha vitabu vingi vya China kwa pesa zake. Alipozungumza na waandishi wa habari kwa lugha fasaha ya Kichina alisema, ili vitabu vya China vifanikiwe kuenea duniani wanahitajika wafasiri wengi Wachina wenyewe. Alisema,

"Mnatutegemea sisi kuieleza China duniani, lakini sisi tuko wachache, waandishi wa vitabu na wasomi wa China ni wengi, na sisi tunaweza tu kusoma sehemu ndogo ya vitabu vyao, kwa hiyo kuna haja ya China ijipatie yenyewe wafasiri, waandishi na wachapishaji wenye uwezo wa lugha za kigeni."

Mwenyekiti anayeshughulikia maonesho ya kimataifa ya vitabu ya Frankfurt alishiriki kwenye shughuli nyingi wakati wa maonesho ya vitabu ya Beijing. Katika hotuba yake alisema, kwenye maonesho ya kimataifa ya vitabu ya Frankfurt, mashirika ya uchapishaji ya China yanaongezeka kwa 20% kila mwaka, ongezeko la haraka kama hilo halikutokea kwa nchi nyingine. Anaona kuwa ingawa idadi ya vitabu vya Ujerumani vinavyouzwa nchini China ni kubwa kuliko vitabu vya China vinavyouzwa nchini Ujerumani, lakini hali hiyo hakika itabadilika, kwa sababu mwaka 2009 China itakuwa ni nchi muhimu katika maonesho ya vitabu ya Frankfurt.

Idhaa ya kiswahili 2007-09-24