Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-03 20:39:54    
Watu wa kabila la Watajik wanaoishi kwenye uwanda wa juu wa Pamirs

cri

Uwanda wa juu wa Pamirs uliopo kusini magharibi mwa sehemu inayojiendesha ya kabila la wauyghur ya Xinjiang, unajulikana sana nchini na nje kutokana na kuwa na milima 14 yenye urefu wa mita zaidi ya 8,000. Wachina wa makabila madogo madogo yakiwemo makabila ya Watajik, la Wauyghur, la Wakeerkezi na Wahui wanaishi kwenye uwanda huo wa juu, miongoni mwao, watu wa kabila la Watajik wanachukua asilimia 90 ya idadi ya watu wa huko. Watu hao wanajulikana kama Mwewe wa Pamirs, zamani walifanya hasa kazi za ufugaji, na wengine walikuwa wakulima. Wilaya inayojiendesha ya Tashenkuergan ya kabila la Watajik ilianzishwa mwaka 1954 baada ya ukombozi wa China kutokana na msaada wa serikali kuu ya China, uchumi wa kabila la Watajik umeendelea kwa kasi, na maisha ya watu wa kabila hilo yameboreshwa kwa kiasi kikubwa.

Mwelezaji wa kituo cha utamaduni wa kabila la Watajik cha wilaya ya Tashikuergan Bw. Ebul alisema, watu wa kabila la Watajik walianza kuishi kwenye uwanda wa juu wa Pamir katika karne 10 kabla ya kristo, wao ni watu wenye ngozi nyeupe wa China. Alisema,

"Watu weupe wana pua inayochongoka sana, uso mrefu na macho yaliyopo ndani sana. Wengine wanasema watu wa kabila la Watajik wanafanana na Wagiriki, lakini ngozi yao ni nyeusi zaidi, hii inatokana na kuwa jua kali zaidi kwenye uwanda wa juu."

Watu wa kabila la Watajik walianzisha utamaduni wao maalumu, na sikukuu ya kikabila ni sehemu muhimu ya mila na desturi za kabila hilo. Watu hao wanaamini dhehebu la Mayi la dini ya Kiislamu, hivyo wana sikukuu ya Kurban ya dhehebu hilo. Je, watu wa kabila la Watajik wanasherehekea vipi sikukuu ya Kurban, Bw. Ebul alisema,

"Tunachinja mbuzi wakati wa sikukuu ya Kurban. Tunachagua mbuzi mwanzoni mwa mwaka, mbuzi huyo ni lazima awe mweupe. Tunachinja mbuzi huyo juu ya paa la nyumba , kwa kuwa tunaona mbuzi huyo atakayochinjwa ni mtakatifu, na damu yake haipaswi kuanguka kwenye ardhi chafu, halafu tunapaka damu hiyo kwenye mapaji ya uso wa watoto ili wapate baraka."

Watu wa kabila la Watajik si kama tu wana sikukuu maalumu ya kijadi, bali pia wana desturi zenye historia ndefu. Kwa mfano, watu wakikutana, wanawake watabusu viganja vya wanaume, wazee watabusu masikio ya watoto, na watoto wabusu kiini cha viganja vya wazee ili kuonesha heshima wakati wa kusalimiana."

Ili kuelewa zaidi utamaduni wa kabila la Watajik, mwandishi wetu wa habari alimtembelea msomi wa kabila hilo Bw. Madalhan kwenye kijiji cha Tashenkuergan.

Nyumba ya watu wa kabila la Watajik zinajengwa kwa mawe, ni tofauti na nyumba za watu wa kabila la Wahan, milango yake hujengwa ikitazama upande wa jua. Bw. Madalhan alisema watu wa kabila la Watajik wanachukulia mwewe kuwa ni alama ya ushujaa, wana hadithi na nyimbo nyingi kuhusu mwewe, kwa mfano filimbi ya mwewe ambayo ni ala ya muziki ya kabila hilo ina hadithi nzuri. Alieleza akisema,

"Kulikuwa na mvulana na msichana waliokuwa wanapendana sana, mtawala wa huko alipojua aliwatenganisha. Kila siku msichana huyo alipofanya kazi alisikia mpenzi wake kuimba nyimbo. Mvulana huyo alikuwa na mwewe mmoja, mwewe huyo alipokufa alimwambia kijana huyo kuwa mfupa wa bawa lake unaweza kutengenezwa kuwa filimbi. Mvulana huyo akawa na filimbi nzuri iliyoweza kupigwa muziki wa kuvutia. Wakati mvulana huyo alipokuwa akipiga filimbi hiyo, msichana alikuwa akicheza dansi, na mwishoni alibuni aina ya ngoma ya mwewe."

Bw. Madalhan alisema filimbi za mwewe hupigwa zikiwa kwa jozi ili kuonesha nia imara ya mapenzi. Watu wa kabila la Watajik wanapenda sana kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Wakati wa kusherehekea sikukuu au harusi, watu hao huimba na kucheza ngoma bila kujali kama wao ni watoto au wazee, wanawake au wanaume.

Mbali na hayo, watu wa kabila la Watajik wana ushujaa wa kulinda maskani na taifa. China ina mipaka mrefu katika uwanda wa juu wa Pamirs, katika maelfu ya miaka iliyopita, watu wa kabila la Watajik wanabeba wajibu wa kuwasaidia wanajeshi wa mipaka ya China kulinda nchi. Katika milima mirefu inayofunikwa na theluji, wakati wanajeshi wa mipaka wanapokumbwa na matatizo, watu hao hujitokeza na kuwasaidia. Mwenyekiti wa baraza la mashauriano ya kisiasa la wilaya ya Tashenkuergan Bw. Moni Tablit alisema,

"Katika miaka elfu mbili iliyopita, mchango mkubwa zaidi uliotolewa na watu wa kabila la Watajik kwa taifa la China ni kulinda sehemu ya mpaka. Watu wote wa kabila hilo ni wazalendo, wanapenda taifa na maskani yao, hakuna mtu hata mmoja wa kabila la Watajik aliyekimbilia nchi za nje, wanatoa msaada mkubwa kwa wanajeshi wa mipaka katika kulinda ardhi ya China."

Wakati mwandishi wetu wa habari walipomaliza mahojiano kwenye sehemu ya watu wa kabila la Watajik, nyimbo nzuri za kabila hilo ilisikika kutoka sehemu mbali. Kwenye uwanda huo mkubwa, nyimbo na ngoma huwa ni ishara za kabila la Watajik.

Wapendwa wasikilizaji, mlikuwa mkisikiliza maelezo kuhusu watu wa kabila la Watajik wanaoishi kwenye uwanda wa juu wa Pamirs. Kipindi hiki cha makabila madogo madogo nchini China kinaishia hapa kwa leo, ni mtangazaji wenu-------, asanteni kwa kuwa nasi, kwa herini.