Mkoa wa Yunnan ni mkoa mkubwa kwa utalii nchini China, watu wengi wamewahi kusikia kuhusu miji ya Dali, Lijiang na Shangri-la. Lakini mahali tunapotaka kuwafahamisha leo ni mahali pengine penye mandhari ya kupendeza, mila na desturi nzuri, sehemu hiyo inaitwa Puzhehei, na iko katika wilaya ya Qiubei, mkoani Yunnan.
Puzhehei ni jina la maziwa yenye chokaa (karst), ambayo yako umbali wa kilomita 280 kutoka Kunming, mji mkuu wa mkoa wa Yunnan. Neno la Puzhehei katika lugha ya Kiyi ya huko ni mahali penye samaki na kamba wengi. Sehemu hiyo ina maji safi kwenye eneo la zaidi ya hekta 3,000, ambapo maziwa ya Puzhehei, Luoshuidong, Xianrendong na mengineyo yanaungana pamoja kama mkufu, milima yenye misitu inaungana na maziwa, na maziwa yanaizunguka milima. Mkurugenzi wa idara ya utalii ya wilaya ya Qiubei Bw. Zhao Wenliang alieleza umaalumu wa Puzhehei kwa maneno machache,
"Ninaeleza umaalumu wa kijiji cha Puzhehei kwa maneno kumi na sita ya Kichina, 'maskani yenye maji, ardhi oevu ya chokaa, dunia ya maua ya yungiyungi, na mashamba mengi yenye maji."
Bw. Nie Wei kutoka Kunming amewahi kufika kwenye kijiji cha Puzhehei mara nyingi, alisema,
"Hapa ni mahali pazuri sana. Maji ni safi na milima ni ya kupendeza. Mandhari nzuri ya hapa ni ya kimaumbile, milima na maji ya hapa ni safi na hayajachafuliwa."
Baada ya kufika kwenye kijiji cha Puzhehei, karibu watalii wote wanapenda kukaa ndani ya mashua madogo na kujiburudisha kwenye ziwa kubwa. Mashua za aina hiyo ni ndogo, zina nafasi kwa ajili ya watu 6 au 7 hivi, watu wanaweza kuchezea maji wakinyoosha mikono yao ndani ya mashua, wenyeji wanapiga makasia taratibu, hivyo mashua inakwenda polepole, hivyo watalii wana nafasi ya kutosha kuangalia mandhari nzuri. Maji ya ziwa ni maangavu, samaki, kamba na majani yaliyoko chini ya maji yanaonekana vizuri sana, kuna ndege wanaoishi karibu na maji, ambao mara kwa mara wanaingiza kichwa ndani ya maji kukamata samaki na bata pori, ndege aina ya egret wanatembea taratibu kwenye sehemu yenye maji machache. Ukitazama kutoka mbali, kuna milima mingi mikubwa na midogo, ingawa milima ya huko siyo mikubwa sana, lakini ina maumbo ya kupendeza.
Wakati mzuri wa kutembelea huko ni majira ya joto na ya mpukutiko, kwa sababu mbali na milima na maziwa ya kupendeza kwenye kijiji cha Puzhehei, kuna maua ya yungiyungi yanayochanua vizuri. Baada ya kupita kona moja, mashua za watalii zinafika kwenye sehemu yenye maua mengi ya yungiyungi. Utaona majani makubwa ya yungiyungi yameenea kwenye maji yasiyo na upeo wa macho, matone ya maji yaliyoko kwenye majani ya yungiyungi yanakwenda upande mmoja na kurudi kwenye upande mwingine. Maua ya yungiyungi yana rangi za aina nyingi, nyekundu, nyeupe na hudhurungi, maua mengine yamechanua sana, wakati maua mengine bado ni vitumba, maua ya yungiyungi yanakuwa ni mengi mno, lakini maua yote yanatofautiana kwa maumbo. Upepo mwororo unapotokea harufu nzuri ya maua ya yungiyungi inaburudisha sana watu. Watu wakiwa ndani ya mashua ndogo, wanaona majani, maua na mbegu za yungiyungi zote ziko karibu na mikono yao.
Watalii waliofika kwenye kijiji cha Puzhehei, licha ya kuangalia mandhari nzuri, pia hupenda kurushiana maji. Watu wanaofahamiana na watu wasiofahamiana wanashiriki kwa pamoja wakitumia bastola za maji, beseni na ndoo, shangwe na vicheko vinajaa kwenye maziwa. Ingawa watalii wanalowa maji, lakini mioyoni mwao wanafurahi sana.
Mandhari nyingine inayovutia watalii kwenye kijiji cha Puzhehei ni mapango ya chokaa, sehemu hiyo ina mapango ya aina hiyo kumi kadhaa, watu husema, "penye mlima hapakosi mapango". Mapango sita kati ya mapango mengi ya huko yakiwemo ya mwezi, kijinga na malaika, yamefunguliwa kwa watalii. Ndani ya mapango hayo kuna mawe mengi yaliyochomoza kutoka ardhini, mawe mengine ni yenye maumbo ya ajabu, mawe ya chokaa ni yenye rangi ya kupendeza na kama ya kioo kidogo mtu anaweza kuona vitu vilivyoko katika upande wa pili wa mawe hayo. Tena mapango hayo ya chokaa yanaungana na vijito, ndani ya mapango pia kuna mandhari nzuri iliyoundwa na mawe yenye maumbo ya ajabu, maji yasiyofahamika chanzo chake pamoja na mashimo ya kutisha.
Watalii wanapotembelea kijiji cha Puzhehei, wasisahau kujifunza desturi, mila na utamaduni wa wenyeji wa huko. Puzhehei ni mahali wanapokaa watu wa kabila la Wayi, mbali na kabila la wayi, pia kuna watu wa makabila ya Wazhuang, Wayao na Wamiao. Watu wa makabila mbalimbali wanaishi huko kwa mapatano na urafiki, na kila kabila lina utamaduni wa jadi wa kipekee. Kijiji cha pango la malaika kilichoko kwenye sehemu ya Puzhehei, kinasifiwa kuwa ni kijiji cha kwanza cha mapatano ya utamaduni cha kabila la Wayi mkoani Yunnan, kijiji cha Nahong ni kijiji cha utamaduni cha kabila la Wazhuang, na kijiji cha Puzhehei chenye familia karibu elfu moja ni kijiji kikubwa chenye wakazi wa makabila matatu ya Wazhuang, Wayi na Wamiao.
Katika miaka ya hivi karibuni, wilaya ya Qiubei imekuwa inazingatia sana uendelezaji wa utalii, majengo yanayotoa huduma kwa watalii yanakamilishwa hatua kwa hatua, watalii waliofika kwenye kijiji cha Puzhehei, licha ya kuweza kuona mila na desturi za wakazi wa huko, kula chakula cha wakulima na kutembea kwenye makazi ya watu wa makabila mbalimbali, pia wanaweza kuhudumiwa vizuri na hoteli pamoja na mambo mengine ya burudani. Maendeleo ya sekta ya utalii yanatoa huduma nzuri kwa watalii, huku yakihimiza maendeleo ya uchumi ya huko. Ofisa wa serikali ya wilaya ya Qiubei Bw. Bai Guangfu alimwambia mwandishi wetu wa habari,
"Wilaya ya Qiubei inachukulia sekta ya utalii kuwa sekta muhimu ya nguzo ya uzalishaji mali kwa maendeleo ya Qiubei, tangu utalii uanzishwe kwenye sehemu hiyo, imefanya kazi kubwa kwa maendeleo ya uchumi na jamii ya wilaya hiyo, inaongeza pato la wakazi wa eneo lile, hususan kuleta mabadiliko makubwa ya kupendeza katika ujenzi wa kijiji na utalii kwenye familia za wakulima, hasa wa kijiji cha pango la malaika na kijiji cha Puzhehei.
|