China ni nchi yenye hali ya masikilizano kati ya tamaduni na dini za aina mbalimbali. Hapa nchini China dini zenye waumini wengi zaidi ni dini ya Kibudha, Dini ya Kidao, dini ya Kiislamu, na dini ya Kikristo, na miongoni mwao dini ya Kidao ni dini pekee iliyoanzishwa na watu wa China.
Zamani sana binadamu walianza kuabudu maumbile, wakiamini kuwepo kwa roho mbalimbali na kufanya matambiko ili kufukuza roho mbaya. Miaka 2,500 iliyopita mwanafalsafa mmoja wa China aliyeitwa Lao Tzu aliandika kitabu kimoja kiitwacho Tao Te Ching, akiwashawishi watu wasilenge kutafuta ukubwa na kuwatendea mema wengine. Hadi kufikia miaka 2000 iliyopita, watu wa China walifungamanisha mawazo yaliyomo kwenye kitabu hicho na ibada kadhaa za kuabudu maumbile, wakaanzisha dini ya Kidao. Dini hiyo inaamini kuwa watu wanaweza kutakasa roho kwa kupitia kujizuia kiroho na kimwili. Kwa hiyo mwanafalsafa Lao Tzu anaheshimiwa kuwa mwanzilishi wa dini ya Kidao, na kitabu cha Tao Te Ching ni kama msahafu wa dini hiyo.
Hekalu la Baiyun liko katika sehemu ya magharibi ya mji wa Beijing. Hekalu hilo lilianza kujengwa mwaka 741 na kufanyiwa ukarabati na upanuzi kwa mara kadhaa. Mtawa mkuu wa hekalu hilo Bw. Yin Chengan anatoka mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani, alijiunga na dini hiyo katika miaka ya 1990 na kuwa mtawa kwenye mlima wa Laoshan, mkoani Shandong, mashariki mwa China ambako ni mahali patakatifu pa dini hiyo.
Bw. Yin alisema alianza kupata ufahamu kuhusu dini ya Kidao kutoka kwenye vitabu maarufu vya masimulizi ya kale ya China. Alisema (sauti 1) "Mwanzoni nilivutiwa na dini ya Kidao niliposoma hadithi. Kwa mfano kwenye kitabu maarufu cha kale cha China kina hadithi kuhusu mtawa wa dini ya Kidao, nilivutiwa sana. Na baadaye mimi mwenyewe nikawa mtawa wa dini ya Kidao."
Dini ya Kidao ina madhehebu mawili, moja linaitwa dhehebu la Quanzhen, na lingine linaitwa dhehebu la Zhengyi. Ni mwiko kwa watawa wa dhehebu la Quanzhen kuoa na kula nyama, watawa wa dhehebu hilo wanaishi kwenye hekalu na kujitenga na dunia ya nje. Na kwa watawa wa dhehebu lingine la Zhengyi hakuna mwiko kama huo. Mtawa mkuu Yin Chengan na watawa wengine wanaoishi kwenye hekalu la Baiyun ni wa dhehebu la Quanzhen.
Baada ya kupata mafunzo kwenye mlima wa Laoshan kwa miaka mitatu, mtawa Yin alianza safari ya kutembelea mahekalu maarufu ya dini ya Kidao kote nchini China. Mwishoni mwa mwaka 2000, alifika kwenye hekalu la Baiyun, hapa mjini Beijing na kuanza kuishi kwenye hekalu hilo.
Kuhusu asili ya dini ya Kidao, mtawa mkuu huyo alisema (sauti 2) "Dini ya Kidao inatoka kwenye jamii ya China, na mambo hayo yalijumuishwa na kupewa mtindo fulani wa kidini. Kwa hiyo mambo ya dini ya Kidao yanaonekana kila mahali kwenye jamii ya watu wa China."
Bw. Yin anapenda kuchora picha tangu alipokuwa mtoto mdogo, baada ya kuwa mtawa wa dini ya Kidao, sasa anapenda zaidi kuchora picha kuhusu malaika na mandhari nzuri ya maumbile ya milima na mito. Pamoja na kuendelea na utafiti wa dini ya Kidao, mtawa mkuu huyo amejiunga na shirika la wachoraji picha la China.
Kwenye hekalu la Baiyun kuna majumba 18 ya kufanya ibada, ambapo zimewekwa sanamu za watu mashuhuri makumi kadhaa kwenye historia ya dini ya Kidao. Kila siku mtawa mkuu Yin Chengan na watawa wengine wanafanya ibada kwa pamoja kwa wakati kwenye ukumbi mmoja mkubwa, ambapo wanasoma kwa sauti msahafu wa dini ya Kidao. Mtawa mkuu Yin alisema kutokana na ibada, watawa wanatakasa roho na kupata ufahamu mwingi zaidi wa dini.
Hivi sasa hekalu la Baiyun linawavutia watalii wengi, kwenye kila jumba kuna mtawa mmoja anayesimamia utaratibu. Bw. Lou Yunke ni mmoja wa watawa, alieleza kuwa kazi yake ni kusimamia vitu vilivyopo ndani ya jumba, kuhakikisha usalama, na kuwahudumia wafuasi wa dini ya Kidao na kujibu maswali yao. Vile vile watawa wanafanya ibada maalumu kutokana na maombi ya waumini wa dini.
Mbali na shughuli za kidini, mtawa Lou pia anapenda kufanya shughuli nyingine. Alisema (sauti 4) "Nafanya mazoezi ya kuandika maandishi ya Kichina. Hivi sasa pia najifunza kupiga kinanda cha Guqin, ambacho ni kinanda cha jadi cha China. Naona kinanda hicho kina sauti nzito iliyotulia, inafaa kwa watawa kupiga. Aidha siku nyingine naandika makala kuhusu mambo niliyopata kwenye utafiti wa dini ya Kidao."
Maisha ya watawa wa dini ya Kidao hayazuiliwi ndani ya hekalu, wanakwenda nje na kuwasiliana na waumini wengi wa dini hiyo mara kwa mara. Dini ya Kidao ina waumini katika nchi nyingine za Asia, Ulaya ya Magharibi, Marekani na Australia. Mtawa Hu Chenghai anakwenda sehemu mbalimbali nje ya China mara kwa mara ili kuwasiliana na waumini. Alisema (sauti 6) "Niliwahi kwenda Singapore mara mbili kufanya mawasiliano na watawa na waumini wa dini ya Kidao, vile vile niliwahi kwenda Malaysia na Taiwan, China. Tunazingatia sana mawasiliano ya kidini. Kila tunapokwenda nje kufanya mawasiliano, serikali inatusaidia."
|