Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-05 19:58:55    
"Balozi" anayehimiza mawasiliano kati ya wafanyabiashara wa China na Rwanda

cri

 Wachina wengi nchini Rwanda wanamfahamu Bw. Pierre, ambaye aliwahi kupewa udhamini wa kuja kusoma nchini China. Hivi sasa Bw. Pierre ni daktari wa hospitali iliyoko Kigali, mji mkuu wa Rwanda. Bw. Pierri mwenye umri wa miaka 40 alikuja nchini China mwaka 1992, kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1999 alikuwa anasoma kwenye chuo kikuu cha pili cha matibabu cha Shanghai. Baada ya kuhitimu kwenye chuo kikuu hicho Bw. Pierre alirudi barani Afrika, na kuanza kufanya kazi kwenye hospitali ya Jinja nchini Uganda hadi mwaka 2000. Mwaka 2000 Bw. Pierre alikuja nchini China kwa mara ya pili, na kupata zaidi mafunzo katika chuo kikuu cha Wuhan, na mwaka 2003 alirudi nchini Rwanda. Kwa kuwa anaweza kuongea vizuri lugha ya Kichina, na anaelewa sana hali ya China, hivyo kati ya mwaka 2003 na mwaka 2004 akiwa mkalimani, Bw. Pierre aliwaongoza wafanyabiashara wa Rwanda kuja nchini China mara kwa mara ili kununua bidhaa ndogo ndogo na zana nyingine. Mwaka 2005 Bw. Pierre alirudi kuendelea kufanya kazi kwenye hospitali ya Jinja nchini Uganda, na mwaka 2006 alitumwa kwenye hospitali nyingine mjini Kigali. Ingawa yeye ni daktari, lakini jamaa zake wengi ni wafanyabiashara, hivyo alipokuwa mtoto Bw. Pierre alipata maoni mengi kuhusu biashara. Lakini zamani hakujua kama baadaye atakuja kuwa "balozi" wa kuhimiza mawasiliano ya kibiashara kati ya China na Rwanda. Kutokana na maendeleo ya ushirikiano kati ya China na Rwanda katika sekta za uchumi na biashara, bidhaa nyingi zaidi zilizotengenezwa na China ziliingia kwenye soko la Rwanda, bidhaa hizo zina sifa nzuri, na bei yake ni nafuu. Mjini Kigali kuna supamaketi inayoitwa "T2000" ambayo inauza bidhaa zinazotengenezwa nchini China, supamaketi hiyo inapendwa sana na wakazi wa huko.

Lakini Bw. Pierre alisema, hivi sasa wafanyabiashara wengi wa Rwanda bado hawaielewi vizuri China, na wafanyabiashara kadhaa wa nchi za nje walieneza uvumi kuwa sifa ya bidhaa za China ni mbaya, hivyo wafanyabiashara wengi wa Rwanda walinunua bidhaa kwa gharama kubwa kutoka kwa wafanyabiashara wa Ulaya, Marekani au Dubai.

Bw. Pierre alisema aliwahi kuishi nchini China kwa miaka kumi, na alijionea mwenyewe maendeleo ya uchumi na ustawi wa soko nchini China. Alipoona wafanyabiashara wa Rwanda hawawezi kutumia soko kubwa na fursa nyingi za China, aliamua kuwasaidia kufanya mawasiliano na kampuni za China. Kama wafanyabiashara wa Rwanda wakitaka kufanya biashara nchini China, Bw. Pierre atawasiliana na viwanda husika nchini China kwa kupitia rafiki zake walioko nchini China, halafu atawaongoza wafanyabiashara hao kuja nchini China na kuchunguza na kununua bidhaa. Kila mwaka Bw. Pierre anakuja nchini China pamoja na wafanyabiashara wa Rwanda, na kununua bidhaa ndogo ndogo na zana za mashine zilizotengenezwa China.

Bw. Pierre anafurahia sana kipindi chake cha kuwasaidia wafanyabiashara wa Rwanda kuwasiliana na viwanda nchini China. Anasema biashara nyingi alizowafahamisha zinafanyika kwa mafanikio, alisema anapenda kuwa "daraja" kati ya China na Rwanda. Wafanyabiashara wengi wa Rwanda hivi sasa bado hawaifahamu vizuri China, anataka kuwaambia kuwa sifa ya bidhaa zilizotengenezwa na China ni nzuri, wasiogope kufanya biashara na viwanda vya China.

*****************************

Ubalozi wa China nchini Cameroon tarehe 24 mwezi Septemba katika jumba la makumbusho la taifa la Cameroon mjini Yaoundé ulifanya maonesho ya picha yanayoitwa "Beijing inakukaribisha", ili kuadhimisha miaka 58 tangu Jamhuri ya Watu wa China ianzishwe.

Waziri wa utamaduni wa Cameroon, waziri wa wanawake na familia wa Cameroon, waziri wa vijana wa nchi hiyo, mabalozi wa nchi mbalimbali nchini Cameroon, wajumbe wa kampuni za China na wachina waishio nchini Cameroon walihudhuria ufunguzi wa maonesho hayo. Balozi wa China nchini Cameroon Bw. Huang Changqing kwenye hotuba yake aliwakaribisha wageni kutoka nchi mbalimbali kuja China kuangalia michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing, kuelewa utamaduni na historia za China na kuona ari na dhamira ya wananchi wa China. Bw. Huang Changqing alisema China itaendesha michezo ya Olimpiki yenye umaalumu na kiwango cha juu kwa msingi wa Olimpiki ya hifadhi ya mazingira, teknolojia na utamaduni na jamii.

Waziri wa utamaduni wa Cameroon alisema katika miaka kadhaa iliyopita, China na Cameroon zilipata mafanikio makubwa katika ushirikiano wa sekta ya utamaduni, alieleza matumaini yake kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kuimarisha ushirikiano ili kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano kati yao. Imefahamika kuwa picha zaidi ya 60 zilioneshwa kwenye maonesho hayo, ambazo zilieleza juhudi za Beijing katika maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008.

Habari nyingine zinasema maonesho kama hayo na shughuli za mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Nigeria pia zilifanyika tarehe 18 mwezi Septemba katika shule ya sekondari ya pili mjini Abuja, Nigeria. Maonesho hayo yaliandaliwa kwa pamoja na ofisi ya utamaduni ya ubalozi wa China nchini Nigeria na kamati ya elimu ya ngazi ya sekondari ya mji mkuu ya Nigeria, ili kutangaza michezo ya Olimpiki itakayofanyika hapa Beijing na utamaduni wa China kwa walimu na wanafunzi wa huko.

Maofisa wa elimu wa huko na maofisa wa kibalozi wa nchi kadhaa nchini Nigeria walihudhuria ufunguzi wa maonesho hayo. Na wakulima na wanafunzi 200 walishiriki kwenye shughuli za mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Nigeria. Konsela wa ubalozi mdogo wa China nchini Nigeria anayeshughulikia mambo ya utamaduni Bw. Jiang Weiming alitoa hotuba akisema, lengo la maonesho hayo ni kuadhimisha miaka 58 tangu Jamhuri ya Watu wa China iasisiwe na kutangaza michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 hapa Beijing. Alieleza matumaini yake kuwa mawasiliano ya utamaduni kati ya China na Nigeria yanaweza kuendelea kati ya wanafunzi wa shule ya sekondari.