Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-12 15:55:57    
Tamasha la 7 la maonesho ya sanaa duniani

cri
Tamasha la 7 la maonesho ya sanaa duniani lilifanyika huko Suzhou, mashariki ya China kuanzia tarehe 25 Septemba hadi tarehe 1 Oktoba. Tamasha hilo liliandaliwa na Shirikisho la wasanii na wafasihi wa China na Serikali ya umma ya Mkoa wa Jiangsu na kuendeshwa na serikali ya umma ya Suzhou mkoani Jiangsu, Shirikisho la wasanii wa China na idara nyingine.

Bendi ya Sisi Tambala ya Tanzania ilikuja China kushiriki kwenye tamasha hilo. Mimi nikiwa mwandishi wa habari nilikwenda Suzhou kuwahoji wasanii hao wa Tanzania. Walipojua mimi ni mchina anayejua kusema Kiswahili walifurahi sana wakaimba wimbo kueleza furaha yaoKiongozi wa Bendi hiyo ya Sisi Tambala ya Tanzania Bwana Kibiriti Kijuja aliniambia kuwa, hii ni mara yao ya kwanza kuja China, na walifurahi kupata fursa ya kushiriki kwenye tamasha hilo, alisema:

Kwanza tumepata kutoka upande wa China, wao wachina tumeona wanathamini sana utamaduni wao. Tumeona hivyo kwa lugha, tumeona kwa vyakula, tumeona hata kwa michezo, na ngoma na muziki, sisi watanzania tumejifunza utamaduni wenu kumbe tumeona kuheshimu utamaduni wa taifa na muziki wa taifa ndiyo fahari?na ndiyo heshima.

Sisi wa Bendi ya "Sisi Tambala", tunafanya maonesho nchini Tanzania karibu nchi nzima, na mara hii tulitoka Tanzania na kuja China, tunafurahi Mfuko wa utamaduni wa Tanzania ulifanya kazi ya kutusaidia kupata nafasi hii ya kuja China kutupelekea kazi zetu kwa walioandaa tamasha hili, na hawa walitukubalia kazi zetu kazipenda na kazichagua, kwa hiyo tunamshukuru Mama Sayore ambaye ni mtendaji mkuu wa Mfuko wa utamaduni wa Tanzania, vilevile tunashukuru serikali ya Tanzania na wizara ya utamaduni ya Tanzania kwa sababu ilitupa nguvu sana, na tulipeperusha bendera ya taifa, kweli tunaona taifa letu linathamani sana utamaduni wetu, tunashiriki kwenye tamasha hilo tungepeperusha sana bendera ya taifa letu Tanzania.

Wasanii kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Afrika kusini, Russia, Australia, Korea ya kusini, Cuba, Uswiz, Peru, Marekani, Hungari, Sri Lanka, Ujerumani, Singapore, Japan, Ieland, na nchi nyingine pia walishiriki kwenye tamasha hilo, ambapo walifanya maonesho ya kuimba nyimbo na kucheza ngoma, ili wachina waweze kujua zaidi utamaduni wa nchi mbalimbali, kufanya mawasiliano ya kiutamaduni na kutafuta njia ya ushirikiano kwenye sekta ya utamaduni. Bwana Kibiriti alisema:

Tunajua tumejenga urafiki na tuko hapa tutakuwa tukijenga uhusiano wa karibu kwenye sekta hiyo ya utamaduni, hasa tutajenga uhusiano huo kati ya vijana wa Tanzania na China kwenye sekta hiyo, kwenye muziki na ngoma, tutawasiliana mara kwa mara, tunapenda sana, kwa kweli tumejenga uhusiano wa karibu sana, wanatupenda sana, na sisi tunawapenda sana, tunakumbuka kitu kimoja muhimu sana kwamba uhusiano huo toka enzi ya baba wa taifa Mwalimu Julius K. Nyerere alipokuwa kuuweka, kwa hivyo uhusiano huo unaendelezwa, kwa hivyo sisi vijana wa leo tunaendeleza uhusiano huo wa Tanzania na China.

Alipozungumzia Bendi ya Sisi Tambala na utamaduni wa Tanzania Bwana Kibiriti alisema:

Tunaonesha muziki wa Tanzania ambao ni muziki wa asili, ambao una vionjo vyetu vya asili, pamoja na mavazi yetu ya kitaifa, vilevile tuna vitenge vile vya kitaifa, kanga na tunayo ngoma, na vionjo vyetu vya asili, tunayo mambo mengi ya asili ya utamaduni wetu, tunapiga muziki wetu kwa vionjo vya kijadi na kuutengeneza kuwa muziki wa kisasa, lakini ni wenye utamaduni wetu. Tunazo nguo za kiutamaduni kabisa, nguo za kimasai, kwa hivyo tutaonesha muziki wetu wa kitaifa, nyimbo, mavazi na lugha yetu ya Kiswahili. Tunaona watu wengi wanajaribu kufuatilia mambo ya Afrika, wachina wengi wanayajua, na sasa tunataka wachina wengi hata wa kawaida wajue Tanzania ipo, ni nchi ya namna gani, na watu wake ni wa namna gani, ambao ni watu wema, wenye amani lakini wanataka sana kufurahi na kupanga mambo pamoja

Kiongozi wa msafara huo aliniambia akisema:

Lengo la safari yetu ni kushirikiana na wasanii wa mataifa mbalimbali katika kuenzi utamaduni wetu wenyewe, utamaduni unaunga mataifa, sisi tunapenda sana utamaduni wetu kushirikiana na wenzetu kujifunza mbinu mpya na kujifunza kutoka kwa wenzetu kwa namna gani tungeendeleza utamaduni wetu, kwani utamaduni ni vitu vyenye thamani sana, utamaduni ungeendelezwa vizazi kwa vizazi. Tanzania na China ni marafiki, tunaendeleza sana ushirikiano kati yetu kwenye sekta ya uchumi, ningefurahi sana kama tungekuwa na uhusiano wa karibu zaidi katika sekta ya utamaduni, ili tuweze kushirikiana, wachina waweze kuwekeza kwenye mambo ya utamaduni, na tushirikiane kujenga ushirikiano wa pamoja wa Tanzania na China kwa sababu utamaduni unaweza kuwawezesha watu kuelewana zaidi na kuheshimiana, na tunaweza kujua kwa nini wenzetu wanafanya jambo fulani kwa namna fulani, na kuheshimu kwa jinsi alivyo. Tanzania na China zinastahili kushirikiana kwa undani zaidi katika sekta ya utamaduni, tunatarajia wawekezaji wa China wanaweza kwenda Tanzania kuwekeza kwenye sekta ya utamaduni, na siyo sekta ya uchumi na biashara nyingine tu, naona safari yetu ni mwanzo wa ushirikiano katika sekta ya utamaduni .

Idhaa ya kiswahili 2007-10-12