Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-16 16:14:16    
Barua 1014

cri

Msikilizaji wetu Bwana Lewis Juma Munyasia wa sanduku la posta 2566 Bungoma Kenya, anasema yeye ni msikilizaji wetu sugu na ametuandikia barua akitaka salamu zake za pongezi ziwafikie watangazaji wote wa Radio China kimataifa pamoja na wasikilizaji wake. Angependa kuishukuru na kuipongeza sana Radio China kimataifa kwa kusoma barua yake kwenye kipindi cha sanduku la barua cha jumapili tarehe 29 Aprili, 2007.

Anasema kwa mtazamo wake, Radio China imataifa kimekuwa ni chombo muhimu ambacho kimeendelea kuboresha hali ya maelewano na ushirikiano wa kipekee baina ya watu wa Afrika na China, maendeleo ya kibiashara na kuimarisha uchumi katika nchi za Afrika. Manufaa au faida ya Radio China kimataifa ni kuwa, imeleta ufahamu kwa watu wa Afrika juu ya mambo kadha wa kadha kuhusu maendeleo na ushirikiano mwema kati ya China na Afrika. Pia imempa ufahamu zaidi juu ya mwelekeo ambao China na wachina wameuchukua ili kuhakikisha kuwa maendeleo yanapatikana kote duniani bila kuyumbishwa kisiasa. Elimu ya sayansi na teknolojia vimeendelea kuimarika, na pia hali ya maisha ya waafrika inazidi kuboreshwa, hali ya ajira kwa jamii za Afrika inazidi kuimarika kutokana na wachina kuwekeza barani Afrika. Kuna miradi mbalimbali ya ukarabati wa miundo mbinu, barabara na hata uwanja wa ndege kama ule wa kimataifa wa Jomo Kenyatta ambao unaendelea kukarabatiwa sasa na wachina.

Anasema hii imekuwa changamoto kwa waafrika haswa wanapofahamu jinsi wachina walivyo na bidii kama mchwa katika kujiletea maendeleo endelevu. Hali hii imedhihirika kutokana na wachina wanavyofanya kila juhudi kuhakikisha kuwa kila tone la maji katika msimu wa mvua linahifadhiwa kwa matumizi ya baadaye katika kilimo cha mboga, matunda na kadhalika. Hali hii imezidi kuboresha maisha na uchumi wa wachina kwa kiwango kikubwa.

Anasema wote hao wanafahamu kuwa China ni nchi yenye idadi kubwa kabisa ya watu kote duniani, na pia ni nchi inayopiga hatua kubwa kimaendeleo. Yeye ana imani kuwa urafiki kati ya China na nchi nyingine ukizidi kuboreshwa, kutakuwa na mambo mengi zaidi ya kufundishana ambayo ni ya umuhimu katika maisha yao na maendeleo katika jamii na nchi zao barani Afrika.

Anasema safari ya Bwana Ayub Mutanda Shariff nchini China mwaka jana imempa ufahamu zaidi na kuelewa jinsi wachina walivyo wakarimu na marafiki wa kweli. Anasema angependa kutumia fursa hii kuiomba Radio China kimataifa iendelee kuboresha ushirikiano zaidi, na kuelimisha wasikilizaji wake kuhusu mambo kadha wa kadha ambayo yatazidi kuleta maendeleo, na ambayo wapenzi wake watajivunia mara kwa mara. Angependa kuomba pia Radio China Kimataifa iwe na vipindi vya mafunzo ya sayansi na teknolojia kama vile ujenzi wa miradi ya gesi ya kinyesi na kilimo, kwa mfano kilimo cha mapea ya kichina, matunda na mboga mbalimbali ambayo yanaweza kupata soko nchini China. Anasema kwa hakika fursa kama hii itawapa wao wapenzi wa Radio China kimataifa jambo la kujivunia katika maisha yao na pia itawainua kiuchumi.

Anasema ameongea na wapenzi wa CRI katika maeneo yao na wanaomba waanzishe darasa la kujifunza lugha ya Kichina, ili kuboresha maelewano zaidi katika lugha. Kizuizi kikubwa katika mpango huu ni vitabu na mwalimu. Kama kuna uwezekano wowote wa kufadhili mpango huu ili ufanikiwe, wanatuhakikishia kuwa watashukuru na watafanya vizuri zaidi. Hii itakuwa ni furaha kwao maana itakuwa ni mwanzo wa maendeleo na ubalozi mwema. Na Atakuwa na furaha isiyo na kifani kusikia kutoka kwetu na kuzidi kuwasiliana nasi kila mara.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Bwana Lewis Juma Munyasia kwa barua yake yenye maelezo ya dhati na kututia moyo kwa maoni na mapendekezo yake kuhusu matangazo yetu. Tumeona ametoa maoni ya kuwepo kwa vipindi vya kuwafundisha wasikilizaji wetu mambo mbalimbali, kuhusu kilimo na hata matumizi ya nishati, tunafurahi kusikia wasikilizaji wetu wanapenda kupata ujuzi wa mambo ya maisha ya kila siku kutoka kwenye matangazo yetu. Hata hivyo mkifuatilia vizuri kipindi cha elimu na afya, mtasikia mambo mengi tunawafundisha wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mutanda Ayub Shariff wa Bungoma Kenya ametuletea barua pepe akisema, ana furaha kemkem kupata fursa ya kuwasalimu watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa popote pale walipo. Anasema anasikitika kwa kuwa ni muda sasa hajapata muda wa kuwasiliana nasi mara kwa mara kama ilivyokuwa hapo awali. Hata hivyo anapenda kutufahamisha kuwa, katika kipindi hicho alikuwa anafuatilia matangazo yetu bila kuchoka. Labda kwa siku chache ambazo kwa kweli kila msikilizaji amekosa kuyapata. siku kama Jumapili ya tarehe 2 mwezi wa kumi wakati matangazo yalikatishwa ghafla bila hata kuomba samahani kwa wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Vilevile jumamosi ya tarehe sita mwezi wa kumi hali hiyo ilirudia tena, na mara hii matangazo hayakufika kabisa. Anasema kwa matukio kama haya yanawatutia wasiwasi na kuwavunja moyo wa kufuatilia vizuri matangazo. Anasema wanafahamu kuwa nchi yao kwa sasa iko kwenye pilikapilika za kampeni za uchaguzi, kwa hiyo kuna wakati shirika la KBC linarusha matangazo ya Rais hewani moja kwa moja popote alipo. Lakini anachoomba ni kuwa hiyo isiwe tatizo, bali idhaa ingepanga kurusha habari kwa wakati mwingine unaofaa.

Tunamshukuru sana Bw Mutanda kwa maelezo yake, na tunampa pole kwa pilikapilika nyingi za kazi. Tunafurahi kwa kutujulisha kuhusu hali iliyotokea kwenye usikivu wa matangazo yetu katika hizo siku mbili, bila shaka ni kutokana na matakwa ya shughuli za kitaifa kama ulivyosema. Lakini hata hivyo ni vizuri wasikilizaji wetu mlio nje ya Nairobi mkumbuke kuwa, kama matangazo yetu yanayopitia KBC yakikatishwa kwa muda, mnaweza kutupata kwenye masafa mafupi. Hata hivyo tunakushukuru Bw Mutanda kwa maoni yako mazuri.

Msikilizaji wetu Bwana Nyanyuki Omonywa kutoka Kenya ametuletea barua pepe akisema, ni fahari yake kubwa kuwasalimu wafanyakazi na watangazaji wa Radio China kimataifa. Anasema hii ni mara yake ya kwanza kuwasiliana nasi. Lakini kwa muda mrefu amekuwa akisikiliza vipindi motomoto vinavyorushwa hewani na Radio China Kimataifa. Anatoa salamu zake kwa watangazaji wa CRI bila kumsahahu Mama Chen, Fadhili Mpunji, Jane Lutaserwa, Josephine Liumba na wengineo. Anamaliza kwa kusema yeye anaendelea kutusikiliza.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Bwana Nyanyuki Omonywa ambaye hakuandika anuani yake kamili kwenye barua pepe. Tunamkaribisha kwa mikono miwili kusikiliza matangazo yetu. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza kwa makini na kutuletea barua za kueleza maoni na mapendekezo yake, kuhusu matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Bwana Mbarouk Msabah wa P.O. BOX 52483 Dubai, Falme za Kiarabu ametuletea barua pepe akisema, angependa kuchukua fursa hii kutoa pongezi zake za dhati kwa Radio China Kimataifa, kutokana na kufunguliwa kwa kituo kipya cha pili barani Afrika ambacho kitaweza kupeperusha matangazo yake kwa njia ya mawimbi ya FM hapo tarehe 1 Oktoba mwaka huu huko Niamey nchini Niger. Kituo hicho ambacho kitapeperusha matangazo ya Radio China Kimataifa kwa lugha tatu ikiwemo lugha kuu inayotumika katika eneo la nchi za Afrika Magharibi yaani Kihausa pamoja na matangazo kwa lugha ya Kifaransa na Kichina.

Anasema kwa kweli hatua hiyo inadhihirisha jinsi gani Radio China Kimataifa inayokwenda sambamba na kuimarisha zaidi mahusiano baina ya Jamhuri ya Watu wa China na bara letu la Afrika kwa kupitia njia mbalimbali. Bila shaka kuboreka kwa mawasiliano kwa njia ya radio kutaweza kusaidia sana kuimarika kwa mahusiano ya kiuchumi na kisiasa kati ya pande hizo mbili. Kwani ni wazi kabisa kuna haja kubwa kwa Waafrika kufahamu mengi juu ya Jamhuri ya Watu wa China kama vile historia yao, tamaduni na mila zao pamoja na hatua zao za kukuza uchumi na maendeleo yao ya kijamii.

Anasema kwa mantiki hiyo ushirikiano wa Watu wa China na Watu wa bara la Afrika utaweza tu kuimarika zaidi ikiwa pande hizi mbili zitakuwa zinaelewana vilivyo, na kwa maoni yake binafsi njia moja ya kuelewana ni kuwasiliana, na bila shaka njia hii ya matangazo ya redio itasaidia sana kuimarisha mawasiliano hayo.

Tunamshukuru sana Bwana Mbarouk Msabaha Mbarouk kwa barua pepe ya kutoa pongezi kwa Radio China Kimataifa kuanzisha Kituo cha matangazo ya FM huko Niamey nchini Niger. Kweli Bwana Mbarouk ambaye ni msikilizaji wetu wa tangu zamani sana, ambaye anafuatilia sana matangazo yetu na kila mara ametoa maoni na mapendekezo yake kwa matangazo ya Radio China Kimataifa. Ufuatiliaji wa wasikilizaji wetu ndiyo uungaji mkono kwa kazi zetu, chini ya juhudi za pamoja za sisi wa Radio China Kimataifa na wasikilizaji wetu waliopo popote pale barani Afrika, hakika tutaendelea vizuri na kazi yetu ya matangazo. Tunakushukuru sana Bwana Mbarouk na wasikilizaji wetu wengine kwa ufuatiliaji wenu na michango yenu.

Kuanzia kesho tarehe 15 Oktoba Mkutano mkuu wa 17 wa Chama cha kikomunisti cha China utafunguliwa hapa mjini Beijing, huu utakuwa Mkutano muhimu sana katika historia, ambao utaamua mikakati muhimu na kuchagua kamati kuu ya chama ya awamu mpya na kuamua mambo makubwa ya chama na serikali. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watafuatilia matangazo yetu kuhusu Mkutano mkuu huo wa Chama tawala cha China, na kutuletea barua kwa wakati kueleza maoni yenu, asanteni sana.

Idhaa ya kiswahili 2007-10-16