Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-24 19:26:43    
Mkoa wa Jilin waandaa wataalamu kwa ajili ya kuendeleza sehemu za vijijini

cri

Mkoa wa Jilin ulioko kaskazini mashariki mwa China ni mkoa wenye wakulima wengi, lakini mkoa huo unakabiliana na upungufu wa wataalamu wa kilimo. Ili kutatua tatizo hilo, mwaka 2005 mkoa huo ulianzisha mradi wa "kila kijiji kuwa na mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu" na kuandaa wakulima wapya wenye ujuzi wa teknolojia na biashara.

Tofauti na wanafunzi wa kawaida wa vyuo vikuu, wanafunzi wa mradi huo, watakuwa wataalamu maalum walioandaliwa na serikali kwa ajili ya maendeleo ya vijiji, pia wanalipiwa ada zote za masomo na serikali. Mradi huo unatekelezwa kwa pamoja na vyuo vitano vya mkoa huo. Katika miaka mitatu iliyopita, wanafunzi zaidi ya elfu 6 kutoka sehemu za vijijini wamejiunga na mradi huo.

Vyuo hivyo vitano vyote vinatilia maanani kuandaa wanafunzi hao, na mpango wa mafunzo yao umeweka mkazo kwenye ujuzi na teknolojia zinazotumika katika uzalishaji. Naibu mkuu wa chuo cha sayansi na teknolojia za kilimo cha Jilin Bi. Ma Lijuan alisema,

"tumeweka masomo ya lazima na masomo mengi ya kuchagua, ili kuwandaa wanafunzi hao kuwa wataalamu wa fani fulani, lakini pia wawe na uwezo kutenda kazi nyingine mbalimbali vijijini. Kwa mfano, baada ya kurudi nyumbani, watajishughulisha na kilimo, lakini huenda pia watajishughulisha kidogo na kazi za ufugaji, hii ni hali ya kawaida vijijini."

Vyuo vikuu vinavyoshiriki kwenye mradi huo vinatilia maanani kuandaa uwezo wa kutenda kazi halisi, mbinu za ufundishaji ni kuwawezesha wanafunzi wanaotoka sehemu za vijijini warudi nyumbani kufanya kazi kwenye mashamba baada ya masomo, ili kuwasaidia kuunganisha uzoefu halisi na ujuzi waliopata katika masomo. Eneo la sayansi na teknolojia la kijiji cha Minle katika wilaya ya Dawa ya mji wa Songyuan mkoani humo ni kituo cha majaribio cha chuo kikuu cha kilimo cha Jilin. Naibu maneja wa eneo hilo Bw. Cai Dejun alisema:

"katika miaka ya hivi karibuni eneo letu la viwanda limetoa mashamba ya majaribio kwa chuo kikuu cha kilimo, kila mwaka wanafunzi thelathini hivi wa chuo kikuu hicho wanakuja kufanya mazoezi ya kazi, na kila kijiji kinatoa mwanafunzi mmoja anayekuja kufanya majaribio hapa."

Baada ya mafunzo ya miaka miwili, mwezi Julai mwaka huu, kundi la kwanza la wanafunzi 1525 kutoka sehemu za vijijini wamehitimu na kurudi nyumbani kuanzisha shughuli zao binafsi. Mwandishi wetu wa habari aliwahoji wanafunzi kadhaa wahitimu wa chuo kikuu cha kilimo cha Jilin, wao wote walionesha hamu ya kutoa mchango wao baada ya kurudi nyumbani.

Imefahamika kuwa wanafunzi 580 kati ya wahitimu wa mwaka huu wameanzisha shughuli zao binafsi. Serikali katika ngazi mbalimbali pia zimetoa misaada kwao. Kuanzia mwaka 2007 Serikali ya mkoa wa Jilin ilichagua na kutoa misaada kwa miradi 100 miongoni mwa shughuli za wanafunzi hao. Serikali za wilaya na tafara pia zimetoa sera nafuu ili kuweka mazingira kwa wanafunzi hao kutoa mchango mkubwa zaidi katika ujenzi wa vijiji vipya. Katibu wa kamati ya chama ya mji wa Meihekou mkoani Jilin Bw. Wang Wenming alisema:

"tunawasaidia wanafunzi katika kutatua matatizo, ikiwemo kupata idhini mbalimbali au kutoa mapendekezo kuhusu shughuli za kilimo na ufugaji, ili waweze kupanua shughuli zao katika muda mfupi. Kamati ya chama ya mji huo inatenga Yuan laki moja kila mwaka ili kuwasaidia wanafunzi wanaorudi nyumbani kuanzisha shughuli zao binafsi, na kutoa mikopo isiyozidi Yuan laki moja kwa wanafunzi wanaotimiza masharti."

Kutokana na uungaji mkono wa serikali, wanafunzi hao wamekuwa wanajiamini na kutaka kuonesha uwezo wao na kutoa mchango kwa ajili ya kuendeleza maskani yao. Kijana Gao Junming mwenye umri wa miaka 26 anatoka tarafa ya Gaojiatun katika wilaya ya Nong'an mkoani humo, yeye alikuwa anashughulikia na kilimo cha matunda kwa miaka minne hadi mitano, lakini mara kwa mara anajiona kuwa hana ujuzi wa kutosha. Mwaka 2005, alifaulu mtihani na kujiunga na chuo kikuu cha kilimo cha Jilin, ujuzi wa kilimo cha matunda aliopata katika chuo kikuu unamsaidia sana. Hivi sasa amefahamu njia ya kupanda zabibu ya aina ya Marekani na kuanza kuieneza. Mavuno ya mwaka kesho yatamletea pato la Yuan elfu 20 hadi 30.

Mbali na kujiendeleza mwenyewe, Gao Junming pia aliwasaidia wanakijiji wenzie kujiendeleza. Mwanakijiji Jing Zhanhai alisema, kutokana na msaada wa Gao Junming, alipanda zabibu ya aina ya Marekani, pato lake la mwaka huu limeongezeka kwa mara nne hadi tano. Si kama tu majirani zake, hata wakulima wa sehemu 7 hadi 8 nyingine mkoani humo walikwenda nyumbani kwake kujifunza ujuzi.

Kama ilivyotokea kwa Gao Junming, wanafunzi wengi wahitimu wa mradi wa "kila kijiji kuwa na mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu" wamefanya juhudi kutafiti na kueneza teknolojia mpya na kusaidia wanakijiji wengine kujiendeleza.

Mradi huo umetia nguvu mpya kwenye sehemu za vijijini mkoani Jilin, pia umeweka tegemeo imara na kutoa wazo jipya kwa wakulima wanaoishi kwa kutegemea ardhi kizazi baada ya kizazi.