Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-29 19:03:09    
Mwigizaji nyota wa filamu Li Lianjie (Jet Lee)

cri

Bw. Li Lianjie anayejulikana kwa wengi kama Jet Lee, mwenye umri wa miaka 44, ni mwigizaji mashuhuri wa filamu za gongfu. Tokea mwaka 1982 alipoigiza filamu yake ya kwanza ya "Hekalu la Shaolin", hadi sasa ameigiza filamu 33 za michezo ya gonfu. Hivi karibuni filamu yake ya "Shujaa Huo Yuanjia" ilioneshwa mjini Beijing. Hii ni filamu inayosimulia hadithi ya shujaa Huo Yuanjia, mcheza gongfu hodari aliyeishi mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 nchini China.

Bw. Li Lianjie alipokuwa mtoto alisifiwa kuwa na kipaji cha gongfu. Alipokuwa darasa la pili katika shule ya msingi alishiriki kwenye mafunzo ya gongfu, kutokana na uhodari wake alichaguliwa na mwalimu wa timu ya gongfu ya Beijing na kuwa mchezaji wa timu hiyo. Tokea hapo maisha yake yamekuwa yanafungamana na mchezo wa gongfu, mwanzoni alikuwa mchezaji na baadaye alikuwa mwingizaji nyota wa filamu za gongfu. Alisema alipokuwa mtoto alikuwa hana tumaini lolote la mbali, ila tu alitaka kumsaidia mama yake kuondokana na umaskini. Alisema,

"Nilipokuwa mtoto nilikuwa sina matumaini makubwa ya mbali, ila tu nilitaka kumpatia pesa mama yangu na kumfanya mama anionee fahari, kwa sababu wakati huo nilikuwa sina baba."

Akiwa mchezaji wa gongfu aliwahi kupata tuzo nyingi za ubingwa katika mashindano, na aliwahi kuzuru nchi zaidi ya 40. mwaka 1982 mwongozaji wa filamu ya "Hekalu la Shaolin" Bw. Zhang Xinyan alimchagua kuwa mwigizaji mkuu katika filamu hiyo, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17. Katika filamu hiyo aliigiza kama sufii mmoja wa hekalu la Shaolin aliyekuwa hodari wa gongfu na kutetea haki. Filamu hiyo ilipooneshwa iliwavutia watazamaji wengi. Hii ni filamu iliyobadilisha maisha yake.

Lakini baada ya filamu ya "Hekalu la Shaolin" Li Lianjie alikuwa na hali mbaya kwa sababu alipofanya mazoezi ya gongfu alivunjika mguu. Alisema,

"Upasuaji ulifanywa kwa muda wa saa saba. Hili lilikuwa pigo kubwa nilipokuwa na umri wa miaka 19. Niliuliza hali yangu itakuwaje baadaye? Daktari aliniambia nitatembea kama watu wa kawaida, lakini sitaweza tena kuwa mchezaji wa gongfu. Kwa hiyo katika miezi miwili niliokuwa hospitalini nililia mara kadhaa, nilikuwa sijui nitafanya nini."

Tokea hapo alilazimika kuondoka kutoka timu ya mchezo wa gongfu, alijiunga na kundi la michezo ya sanaa huko Hong Kong na kushiriki katika filamu za gongfu. Katika muda wa miaka 20 hivi kila alipoigiza filamu ya gongfu Li Lianjie alikuwa anafunga bendeji kwenye mguu alioumia.

Katika muda wa miaka kadhaa alimaliza filamu zaidi ya kumi za gongfu, uhodari wake unasifiwa sana na watazamaji wa China. Mwaka 1992 alianzisha kampuni yake ya filamu ya Zhengdong, na alikamilisha filamu nyingi za gongfu, kila moja ilikuwa na mafanikio.

Mwaka 1988 Bw. Li Lianjie alihamia Marekani kuendeleza mambo yake. Baada ya mwaka 1997 alianza kushirikiana na Holywood, aliigiza filamu nyingi za gongfu zikiwa ni pamoja na Silaha za Hatari "Lethal Weapon 4", Romeo Lazima Auawe "Romeo Must Die", na Busu la Dragoni "Kiss of the Dragon". Tofauti na filamu za gongfu za Kichina, katika filamu hizo alicheza vitendo vya aina nyingine kabisa. Mwaka 2002, filamu ya "Shujaa" iliyoongozwa na mwongozaji mashuhuri wa China Bw. Zhang Yimou, ilipata mafanikio makubwa ndani na nje ya China. Katika filamu hiyo Bw. Li Lianjie alionesha uhodari wake wa ajabu.

Bw. Li Lianjie alisema ingawa amejiunga na Holywood, lakini alipozungumzia filamu zake alizoigiza nchini Marekani alisema,

"Huko Marekani watu wengi wananiheshimu lakini dunia yangu sio Marekani bali ni Asia, watu wanaonipenda na kunifahamu zaidi ni watazamaji wa China, ninapopita barabarani nchini Marekani hakuna mtu anayefahamu kwamba mimi ni Li Lianjie."

Bw. Li Lianjie alisema, maisha yake yamepita nusu, zamani alikuwa na lengo wazi, lakini sasa hana. Mwaka 2004 Tsunami ilipotokea katika sehemu ya Asia ya kusini alikuwa likizoni pamoja na familia yake kwenye kisiwa cha Maldives, aliponea chupuchupu. Kutokana na Tsunami amekuwa na ufahamu wa aina nyingine kuhusu maisha. Mwaka 2007 kwa kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu cha China alianzisha "Mfuko wa Li Lianjie", ili kuwasaidia watu waliokumbwa na misiba na matatizo.