Kati ya milima na mito mikubwa maarufu ya nchini China, ni michache tu inayoweza kuwa na hadhi ya heshima kubwa kutoka zamani za kale hadi hivi sasa. Nchini China mlima Taishan ni mahali pa kuabudu budha kwa wafalme, na ni alama ya ustaarabu na imani katika zama za kale nchini China.
Mlima Taishan wenye mwinuko wa mita zaidi ya 1,500 uko katika mji wa Taian, mkoani Shandong, mashariki mwa China. Neno la Tai katika lugha ya Kichina lina maana ya neema na salama, msemo mmoja wa zamani nchini China unasema, "kama mlima Taishan ni salama, basi sehemu zote ni salama", kutokana na msemo huo, unaweza kujua ni kwa nini wachina wanauita mlima Taishan ni "mlima wa kwanza nchini China".
Wafalme wa zamani walipopanda mlima Taishan, walianzia kwenye hekalu la Dai lililoko chini ya mlima huo. Kuna njia moja iliyotumiwa na wafalme ya kuanzia kwenye lango la kusini la mji wa Taian hadi kwenye kilele cha mlima, na hekalu la Dai liko kwenye njia hiyo inayopita katikati ya mji huo. Hekalu la Dai lilikuwa mahali pa kufanya sherehe kubwa ya kupanda mlima kwa wafalme, mawe mengi yaliyochongwa maneno ya kumbukumbu yako kwenye hekalu hilo, yanaeleza kuhusu sherehe za kuabudu mungu za wakati ule, na kueleza jinsi watu wa kale walivyomcha Mungu. Mwongoza watalii Bi Li Xinfeng alisema, tokea karne ya tatu KK, wafalme walipokwenda huko kupanda mlima Taishan, walikuwa wanaandika maneno ya kumbukumbu.
"Mengi ya mawe hayo yalijengwa wakati wafalme walipofika hapa. Wafalme wakifika hapa walitaka kujenga mawe ya kumbukumbu kuhusu shughuli zake za kujenga hekalu la Dai na kutoa sadaka kwa mungu wa mlima, shughuli hizo zote zinaelezwa kwa maneno yaliyochongwa kwenye mawe. Kwa kuwa mawe hayo yalijengwa miaka mingi iliyopita, mengi yamevunjika kutokana na kupigwa na jua na mvua."
Kama watu wakipanda mlima kwa kutumia ngazi za mawe toka kwenye hekalu la Dai, kupita kwenye mlango wa kwanza wa mlima Taishan, unaoitwa "mlango wa mbingu", huko kuna mawe mengi ya kumbukumbu pamoja na mlango wa mawe wa kumbukumbu unaojulikana kuwa ni "mahali pa kupanda mlima kwa Confucius", Confucius, ambaye ni mwasisi wa kundi la wananadharia wa nadharia ya Confucius, aliwahi kupanda mlima Taishan, na alisema ukubwa wa mlima Taishan unafanya nchi ionekane ndogo, mlango wa mawe wa kumbukumbu ulijengwa kama kumbukumbu ya matembezi yake.
Kwenye njia ya mlima kati ya "mlango wa mbinguni" wa kwanza hadi "mlango wa mbinguni" wa kati, kuna mawe makubwa yaliyochongwa maneno ya msahafu wa King Kong miaka elfu moja iliyopita. Kama ukiangalia sehemu ya chini kwenye "mlango wa mbingu" wa kati, ambao urefu wake ni zaidi ya mita 800 kutoka kwenye usawa wa bahari, majengo marefu ya mjini yanaonekana madogo kama kete kwenye mchezo wa bao. Kama ukiangalia kwa sehemu ya juu, njia yenye mizunguko 18 inaonekana kama ngazi iliyotundikwa angani. Kuanzia "mlango wa mbinguni" wa kati hadi mlango wa tatu wa mawe unaojulikana kwa "mlango wa mbingu" wa kusini, kuna sehemu moja ya njia iliyochongoka zaidi, hivi sasa watalii wanaweza kupita kwenye sehemu hiyo kwa cable-car. Lakini kutumia cable-car kunapoteza raha ya kupanda mlima huo, Bibi Liu mwenye umri wa miaka 60 alisema, inasikitisha kama mtu alifika kwenye mlima Taishan bila kupanda mlima kwa miguu.
"Kupita sehemu hiyo kwa kutumia cable-car hakufurahishi. NI vizuri kupita kwenye njia ndogo inayozunguka-zunguka mlimani na kupita kwenye miti. Tunasikitika kwa kufika juu kwa kutumia cable-car. Tunataka kupanda mlima kwa miguu, ili tuwe na furaha zaidi, hatuogopi uchovu."
Kupanda mlima Taishan kwa kufuata njia ya mlimani, sehemu iliyochongoka zaidi na ngumu zaidi ni sehemu inayoitwa "mizunguko 18", watu waliofika kwenye mlima Taishan wanajua kuwa sehemu ile ya "mizunguko 18" ingawa ina mwinuko chini ya mita 100, lakini ina ngazi zaidi ya 1,600, na njia hiyo inaonekana kama iko wima kabisa ina urefu wa zaidi ya mita 400. Sehemu ya mwanzo ya "mizunguko 18" haina mwinuko mkubwa, lakini inainuka hatua kwa hatua, hadi kuwa kama iko wima kabisa, ngazi ndogo zina nafasi ndogo, ambayo haitoshi kuweka mguu mmoja, watalii wanapanda mlima wakisaidiwa kwa mikongojo huku wakihema.
Baada ya kufika kwenye "mlango wa mbingu" wa kusini, watu wanaweza kuona mbali. Washairi walisema, ukisimama huko, "upepo mwororo unavuma kutoka umbali wa kilomita elfu kumi", huko watu wanasikia sauti ya upepo unaovuma, machoni mwao ni mawingu ya mbinguni na milima isiyoonekana sawasawa ya mbali, hapo uchovu wote unatoweka.
Kama ukienda mbele zaidi kwa upande wa mashariki, utafika kwenye "mtaa wa mbingu" wenye shughuli nyingi za biashara, kwenye sehemu hiyo tambarare watu wanaweza kupata chakula, vinywaji na vyumba vya kulala usiku.
Juu ya "mtaa wa mbingu" kuna mabaki ya hekalu la dini ya kidao linalojulikana kwa jina la "Bixiasi". Dini ya kidao ni dini asili ya China, kuna majengo mengi ya dini ya kidao kwenye mlima Taishan, na hekalu la "Bixiasi" ni maarufu zaidi kati ya majengo hayo. Bw. Wang Junshan wa ofisi ya wasimamizi ya hakelu la Dai alisema, inasemekana, kuwa mwanzilishi Bi Xia alikuwa mlinzi wa mlima Taishan, aliwahi kugombea ardhi ya huko na kaka yake jemadari Huang Feihu, walikubaliana kuwa atakayetangulia kufika kwenye mlima Taishan atatawala mlima. Kwa kuwa Bi Xia hakuwa na nguvu kubwa kama kaka yake mkubwa, hivyo alifanya ujanja, hatimaye dada yake huyo alimshinda kaka yake. Hivi sasa sanamu ya shaba ya Bi Xia bado imewekwa katika hekalu la "Bixiasi"
Kwenye kilele cha mlima Taishan kuna kiwanja kimoja, inasemekana kuwa huko palikuwa ni mahali pa kuabudu mabudha kwa wafalme.
"Wafalme kuwaabudu mabudha kwenye kilele cha mlima ni kutoa sadaka kwa mabudha walioko mbinguni, walifikiri kuwa mafanikio waliyoyapata ni mafanikio ya mabudha"
Mtalii David Pratt kutoka Marekani mwenye umri wa miaka 78, amekaa nchini China kwa miaka kadhaa, hivi sasa anafundisha katika chuo kimoja cha mji wa Jinan, mji mkuu wa mkoa wa Shandong, na aliwahi kushiriki mara kadhaa kwenye michezo ya kimataifa ya kupanda mlima Taishan. Bw. Pratt siyo mtu mwepesi, alipofika kwenye kilele cha mlima, alikuwa anahema sana, alisema mlima Taishan ni changamoto na una mambo mengi ya utamaduni.
"Mlima Taishan ni mzuri na mkubwa, kupanda mlima huo sio rahisi, lakini ninapenda historia ya mlima Taishan, utamaduni wake, wafalme waliwahi kufika hapa kutoa sadaka na kuomba wabarikiwe na mungu."
Mandhari ya kilele cha mlima ni nzuri ajabu, asubuhi jua linachomoza ghafla kutoka mawinguni na kupaka mlima kwa rangi ya dhahabu.
|