Maonesho ya 3 ya uwekezaji na biashara ya Asia ya kaskazini mashariki yalifungwa mwanzoni mwa mwezi Septemba huko Changchun, mji mkuu wa mkoa wa Jilin, China. Katika maonesho hayo ya siku nne, wajumbe waliohudhuria mkutano huo walifanya majadiliano kuhusu "kuhimiza ushirikiano wa kikanda wa sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki" na "kustawisha kituo kikongwe cha viwanda vya kaskazini mashariki ya China". Wajumbe hao waliona kuwa, nchi 6 za Asia ya kaskazini mashariki zitatumia fursa hiyo ya maonesho, ili kuhimiza maendeleo ya kina ya ushirikiano wa sehemu hiyo.
Sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki ni pamoja na mikoa mitatu ya Liaoning, Jilin na Heilongjiang ya China na sehemu ya mashariki ya mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani wa China, mashariki ya mbali ya Russia, peninsula ya Korea, Japan na Mongolia, ina eneo karibu kilomita za mraba milioni 1.7. Naibu waziri mkuu wa China Bw. Zeng Peiyan kwenye maonesho hayo alisema, nchi za Asia ya kaskazini mashariki zinapakana au kutenganishwa kwa bahari, na mawasiliano ya kirafiki kati ya watu wa nchi hizo yana historia ndefu. Alisema katika mchakato wa kuimarishwa siku hadi siku kwa utandawazi wa uchumi duniani, nchi za Asia ya kaskazini mashariki zina nia ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati yao. Alisema,
"Uchumi wa nchi mbalimbali za Asia ya kaskazini mashariki unanufaishana, baadhi ya nchi zina nguvu kubwa ya kiuchumi, nyingine zina maliasili nyingi na nguvu kazi nyingi, na nyingine zina teknolojia ya kisasa ya uzalishaji na uzoefu wa usimamizi, hivyo kuna msingi mzuri kwa kuendeleza zaidi ushirikiano wa kikanda."
Katika miaka ya hivi karibuni, kadiri uchumi wa nchi mbalimbali za Asia ya kaskazini mashariki unavyoongezeka kwa hatua madhubuti, eneo la biashara na uwekezaji ndani ya sehemu hiyo pia linapanuka hatua kwa hatua, na uhusiano wa kutegemeana kwa uchumi kati ya nchi hizo unaongezeka. Kwa mfano biashara kati ya China na Russia imeongezeka kwa kasi kwa miaka 7 mfululizo, mwaka jana kwa mara ya kwanza thamani ya biashara ya nchi hizo mbili ilizidi dola za kimarekani bilioni 30, ambayo ilikuwa na ongezeko la asilimia 14 kuliko mwaka juzi wakati kama huu. Biashara kati ya China na Japan na biashara kati ya China na Korea ya Kusini pia zimepata maendeleo makubwa.
Wakati huo huo, katika miaka ya hivi karibuni ujenzi wa jukwaa la kuhimiza ushirikiano wa kiuchumi wa sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki unaharakishwa. Lengo la serikali ya China kufanya maonesho ya uwekezaji na biashara ya Asia ya kaskazini mashariki, ni kuhimiza mawasiliano na ushirikiano wa uchumi na biashara wa sehemu hiyo, na kuanzisha jukwaa la ushirikiano wa muda mrefu la kunufanishana, kushindana na kufunga mlango. Alipozungumza kuhusu jukwaa hilo, ofisa wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa Bibi Nataliya Yacheistova alisema,
"Maonesho ya uwekezaji na biashara ya Asia ya kaskazini mashariki yanatoa fursa nzuri kwa viwanda na makampuni ya nchi mbalimbali yaliyoshiriki kwenye maonesho hayo. Wafanyabiashara walioshiriki kwenye maonesho hayo waliweza kuonesha bidhaa zao, kufanya ushirikiano, kusaini makubaliano na kuonesha nia ya kuwekeza. Maonesho hayo hakika yamehimiza maendeleo na ustawi wa uchumi wa sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki."
Kadiri uchumi wa China unavyoendelea kwa kasi, ndivyo uchumi wa kituo kikongwe cha viwanda vya kaskazini mashariki cha China unavyoendelea vizuri. Hasa kuanzia mwaka 2003, China ilianza kutekeleza mkakati wa kustawisha kituo hicho, na kutoa sera mbalimbali kuvisaidia viwanda vya sehemu ya kaskazini mashariki ya China kuondoa matatizo, kuwahimiza wafanyabiashara wa kigeni kushiriki kwenye marekebisho ya viwanda, na kuendeleza biashara ya mipakani kwenye sehemu hiyo. Baada ya mkakati huo kutekelezwa kwa zaidi ya miaka minne, hatua za mageuzi na ufunguaji mlango wa sehemu hiyo zinaharakishwa kidhahiri, ujenzi wa miundo mbinu unaimarishwa zaidi, marekebisho ya miundo ya viwanda yamepata maendeleo mapya, na maisha ya watu yanaboreshwa siku hadi siku.
Ustawi wa sehemu ya kaskazini mashariki ya China pia unatoa fursa mpya kwa ushirikiano wa sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki, na kuleta fursa kubwa ya biashara kwa nchi mbalimbali za sehemu hiyo. Mfanyabiashara wa vifaa vya ujenzi kutoka Mongolia Bw. Otgon Baatar alitumai kufanya ushirikiano wa kibiashara na viwanda vya sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Alisema,
"Nimefahamishwa kuwa serikali ya China ilitoa sera mpya zenye unafuu kwa maendeleo ya sehemu ya kaskazini mashariki ya China, hii ni fursa nzuri kwetu. Sio tu katika shughuli za ujenzi, bali pia katika biashara za uagizaji bidhaa kutoka nje na uuzaji bidhaa nchi za nje, mimi pia natumai kutafuta wenzi wa ushirikiano nchini China."
Ingawa ushirikiano wa uchumi na biashara wa nchi mbalimbali za Asia ya kaskazini mashariki unaendelezwa kwa kasi, lakini pia bado kuna matatizo mbalimbali kama vile kiwango cha maendeleo cha nchi mbalimbali za sehemu hiyo kina tofauti kubwa, kiwango cha ushirikiano kati yao bado ni cha chini, na mfumo wa ushirikiano bado haujakamilika. Ili kukabiliana na changamoto mpya, naibu waziri mkuu wa China Bw. Zeng Peiyan alisema, China inatetea kuwa nchi mbalimbali zinapaswa kuimarisha mawasiliano na ushirikiano kwenye msingi wa kushiriki kwa usawa na kuwa na msimamo wa kufanya juhudi na kufungua mlango, ili kuhimiza maendeleo ya pamoja ya sehemu hiyo. Alisema,
"China inapenda kushirikiana na nchi husika kuharakisha ujenzi wa barabara, reli na bandari; kuimarisha mawasiliano ya uchumi, kupanua biashara, na kuinua kiwango cha kuwekeza kwenye nchi nyingine; China inatumai kuwa nchi mbalimbali za Asia ya kaskazini mashariki zitaendelea kuhimiza uhuru na urahisi wa biashara, kuchukua hatua zenye ufanisi, na kuboresha utaratibu na mazingira ya forodha, ukaguzi, karantini na visa ya biashara."
Kwa muda mrefu mkoa wa Jinlin wa China unafanya ushirikiano na nchi nyingine za Asia ya kaskazini mashariki katika uchumi na biashara, sayansi na teknolojia, nishati na mali ghafi. Mkuu wa mkoa huo Bw. Han Changfu alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, katika siku za usoni mkoa wa Jinlin utaendeleza kwa kina na kupanua mawasiliano na ushirikiano wa pande hizo, ili kuhimiza zaidi ushirikiano wa sehemu ya Asia ya kaskazini mashariki.
|