Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-10-31 16:43:53    
Madarasa ya wanafunzi wa mkoa wa Xijiang ya shule za sekondari zilizoko katika miji mikubwa iliyoendelea nchini China

cri

   

Karibuni katika kipindi hiki cha makabila madogo madogo nchini China. Zamani kwa wanafunzi wa shule za sekondari wanaoishi kwenye sehemu za mbali za mkoa unaojiendesha wa kabila la Wauyghur wa Xinjiang magharibi mwa China, kusoma kwenye shule za miji mikubwa iliyoendelea kulikuwa ni ndoto tu, lakini tangu mwaka 2000 serikali ya China ianzishe madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang kwenye shule za miji mikubwa, ndoto ya wanafunzi wengi wa mkoa huo imetimia.

Kutokana na sababu za kihistoria, mazingira, uchumi na nyinginezo, kuna pengo kubwa kati ya mkoa wa Xinjiang na sehemu nyingine zilizoendelea nchini China katika shughuli za elimu. Ili kuusaidia mkoa wa Xinjiang kuwaelimisha watu wake wa makabila mbalimbali, mwaka 2000 serikali ya China iliamua kuanzisha madarasa kwa ajili ya wanafunzi wa sekondari wa mkoa wa Xinjiang kwenye shule za miji mikubwa iliyoendelea ikiwemo Beijing, Shanghai, Tianjin na Hangzhou.

Xepghet wa kabila la Wauyghur alianza kusoma kwenye darasa la wanafunzi wa Xinjiang la Shule ya Sekondari ya Chuo Kikuu cha Walimu cha Hangzhou baada ya kufaulu kwenye mtihani mwaka 2004, sasa yeye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu. Xepghet ni mwanafunzi maarufu sana kwenye shule hiyo, kutokana na kuwa yeye si hodari tu katika masomo yake, bali pia ana uhodari mwingine mbalimbali. Xepghet ni naibu mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi la shule hiyo, na mara kwa mara anashiriki kwenye shughuli za kukusanya habari. Baada ya kwenda kusoma Hangzhou, amepata fursa nyingi ya kufanya mawasiliano na wanafunzi wa mji huo. Wakati Xepghet anapofanya bidii katika masomo yake, anatilia maanani sana kujiendeleza katika shughuli nyingine. Alisema,

"Kufanya kazi baada ya masomo hakutegemei elimu peke yake, bali pia kunahitaji uwezo mwingine mbalimbali. Kushiriki kwenye mashirikisho ya shuleni kunaweza kunisaidia kuongeza uwezo huo."

Mama wa Xepghet bibi Risalet pia ana furaha kubwa moyoni kutokana na mtoto wake kupata fursa ya kusoma mjini Hangzhou. Alieleza kuwa wakati Xepghet alipoandikishwa na shule ya sekondari ya Hangzhou baada ya kufaulu mtihani, jamaa wote wa familia hiyo walijivunia sana. Sasa miaka miwili imepita, mtoto wa bibi Risalet amepata maendeleo makubwa katika masomo na uwezo mwingine, alisema,

"Shule za miji iliyoendelea zina mazingira mazuri na walimu wenye uwezo wa juu zaidi kuliko shule za Xinjiang, na mtoto wangu anaweza kupanua upeo wake katika shule ya Hangzhou."

   

Ili wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang waweze kuelimishwa vizuri katika shule za miji iliyoendelea, miji hiyo huchagua shule zake nzuri zaidi kuandaa madarasa kwa ajili ya wanafunzi hao, na kuwapa walimu wazuri. Walimu hao wana uwezo mkubwa wa kufundisha, na wanawatendea vizuri wanafunzi hao kutoka mkoa wa Xinjiang kama watoto wao wenyewe.

Nyumbani kwa Xepghet, mwandishi wetu wa habari alikutana na walimu wawili wa Shule ya Sekondari katika Chuo Kikuu cha Walimu cha Hangzhou, walikwenda kuwapokea wanafunzi wa Xinjiang waliokuwa wanarudi shuleni. Mwalimu mmoja anayeitwa Zhang Qi alisema,

"Tuliagiza tiketi za garimoshi kwa wanafunzi hao wa Xinjiang, na kuwasaidia kufunga mizigo, halafu tuliandamana nao kwenda nyumbani kwao mkoani Xinjiang."

Tangu madarasa ya wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang katika shule za sekondari yaanzishwe kwenye miji mikubwa iliyoendelea mwaka 2000, madarasa hayo yamepata mafanikio makubwa. Katika miaka saba iliyopita, yameandikisha wanafunzi zaidi ya 18,000 kutoka mkoa wa Xinjiang, na zaidi ya 3,400 waliohitimu masomo katika madarasa hayo walishiriki kwenye mtihani wa kujiunga na vyuo vikuu katika miji hiyo, na miongoni mwao asilimia 90 walifaulu na kupata fursa ya kujiunga na vyuo vikuu.

Behtiyar amehitimu masomo mwaka huu katika darasa la wanafunzi kutoka mkoa wa Xinjiang la Shule ya Tano ya Tianjin, sasa yeye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tianjin. Baba yake Bw. Ehet anafurahi sana, ameishukuru serikali ya China kwa kutekeleza sera ya kuunga mkono shughuli za elimu katika sehemu za makabila madogo madogo, alisema,

"Kwa kupitia kuanzisha madarasa ya wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang kwenye shule za miji iliyoendelea, serikali imetoa mchango mkubwa kwa wanafunzi wa makabila madogo madogo kuinua kiwango chao cha lugha ya kabila la Wahan na kuongeza uwezo wao mbalimbali, pia imesaidia maendeleo ya shughuli za elimu za Xinjiang. Kitendo hicho pia kimepunguza matatizo ya kiuchumi kwa familia za wanafunzi hao, hasa kwa familia maskini za wafugaji."

Kazi ya kuanzisha madarasa ya wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang kwenye shule za sekondari za miji mikubwa iliyoendelea ilifanywa kwa msaada wa wizara ya elimu, wizara ya fedha ya China na serikali ya mkoa wa Xinjiang na miji inayotoa madarasa hayo. Hadi sasa China imetenga yuan milioni 400 kwa ajili ya shule zilizoandaa madarasa hayo, ambapo miji inayotoa madarasa hayo inawapa wanafunzi wa mkoa wa Xinjiang kwenye madarasa hayo msaada wa fedha wa yuan elfu kumi hivi kwa mwaka, mbali na hayo, serikali ya mkoa wa Xinjiang pia ilitoa msaada wa yuan elfu 2.7 kwa kulipa nauli na bima ya matibabu kwa wanafunzi hao.