Mkoa unaojiendesha wa Ningxia wa Kabila la Wahui, ni moja ya mikoa mitano inayojiendesha ya makabila madogomadogo nchini China. Ingawa mkoa wa Ningxia uko nyuma kiuchumi ikilinganishwa na mikoa ya pwani ya mashariki ya China, lakini mkoa huo una utamaduni wa jadi unaong'ara. Hivi karibuni mkoa huo umetangaza orodha ya aina za urithi wa utamaduni wa jadi usioonekana mkoani humo.
Mliosikia ni wimbo wa jadi uitwayo "Ua" unaofahamika sana kwa wakazi wa mkoa wa Ningxia.
Bonde la Mto Huanghe ni chanzo cha utmaduni wa taifa la China na katika mkoa wa Ningxia uliopo katika bonde hilo wanaishi watu wengi zaidi wa kabila la Wahui. Katika karne ya 11 dola la kifalme la Xixia lilitawala huko, ambako ni sehemu ya kaskazini magharibi ya China. Hivi sasa mkoani humo licha ya kuwepo kwa utamaduni uliorithishwa kutoka dola la Xixia, pia kuna aina nyingi za utamaduni usioonekana wa kabila la Wahui kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana, kama vile muziki wa ala, sanaa za mapambo ya mavazi, picha za kukatwa na muziki wa ala. Mkurugenzi wa kituo cha hifadhi ya utamaduni usioonekana mkoani humo Bw. Jin Zongwei alieleza kigezo cha kupima urithi wa utamaduni wa jadi usioonekana, alisema,
"Kwanza, utamaduni huo ni lazima uwe na historia ndefu, pili uwe na athiri kwa maisha ya wenyeji, na tatu uwe umerithishwa na vizazi vingi, na mpaka sasa uwe upo na unaendelea kuenea miongoni mwa wenyeji. Katika mkoa huo wakazi karibu wote ni wa kabila la Wahui, kwa hiyo uchunguzi unatiliwa mkazo zaidi miongoni mwa wakazi wa kabila la Wahui."
Bwana Jin Zongwei alisema, hivi sasa mkoani humo kuna makundi saba na aina karibu mia moja za utamaduni usioonekana, wilaya ya Longde kusini mwa mkoa huo inaongoza kwa kuwa na aina nane za utamaduni huo zikiwa ni pamoja na uchoraji wa kienyeji, picha za kukatwa, utarizi, sanaa ya uchongaji kwenye matofali, sanamu za kufinyangwa na mila za tambiko. Naibu profesa katika kituo cha utamaduni cha wilaya ya Longde Bi. Wang Lianxi alieleza kuwa ili kurithi na kuendeleza sanaa za jadi, kituo chake kilianzisha "makao ya sanaa", kwa mfano "makao ya utarizi", "makao ya picha za kukatwa", "makao ya sanamu za kufinyangwa", makao hayo yamevutia na yamewahamasisha wasanii wengi kuendeleza sanaa za kienyeji. Alisema,
"Mara kwa mara tunakwenda kwenye makao hayo kutoa uelekezaji, na kuwatangazia bidhaa za utamaduni wao. Kutokana na juhudi hizo, vijana wengi wanapenda kushiriki kwenye mafunzo kwa kufahamu umuhimu wa utamaduni wao, na kutokana na ustawi wa utamaduni wao, uchumi umepata maendeleo."
Mchezo wa "Fimbo ya Ukoo wa He" pia umeorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa utamaduni usioonekana katika mkoa wa Ningxia. Mchezo wa "Fimbo ya Ukoo wa He" umekuwepo kwa miaka 180, na hadi sasa imerithishwa kwa kizazi cha tano. Mchezo huo umechanganya riadha na gongfu. Lakini mchezo huo uko hatarini kutoweka kutokana na ukosefu wa warithi. Bw. He Jiangong ambaye ni mrithi wa kizazi cha tano cha riadha hiyo alieleza matumaini kuwa serikali itasaidia kuimarisha utamaduni wa mchezo huo. Alisema,
"Bila kuchukua hatua za haraka za kudumisha utamaduni huo na bila msaada wa serikali, utamaduni huo utatoweka, mbele ya babu zetu tutaona aibu na vizazi vya baadaye vitasikitika. Lakini urithi wake sio tu unategemea warithi kadhaa bali unategemea uenezi wake, matumaini yangu ni kuieneza riadha hiyo hadi kwenye shule za msingi na za sekondari na kuzifanya kuwa darasa la mchezo."
Ili kuhifadhi utamaduni wa jadi usioonekana, mapema katika miaka ya 90 ya karne iliyopita serikali ya mkoa wa Ningxia ilitunga sheria. Mwaka 2005 mkoa huo ulianzisha kituo kikuu cha hifadhi ya urithi wa utamaduni usioonekana, na mwaka 2006 "Sheria ya kuhifadhi urithi wa utamaduni usioonekana mkoani Ningxia" ilianza kutekelezwa. Mkurugenzi wa kituo hicho Bw. Jin Zongwei alisema,
"Tutahifadhi urithi wa utamaduni usioonekana kwa njia tatu, moja ni kuwa ili kuuwezesha urithi uendelee ni lazima kuupatia warithi na kuupatia fedha. Njia nyingine ni kuanzisha mafunzo katika shule kwa kuwaalika wasanii kuwafundisha wanafunzi, na njia nyingine ni kuviwekea sera na sheria vituo vyote vya utamaduni mkoani vishughulike na hifadhi ya urithi wa utamaduni huo usioonekana."
Bw. Jin Zongwei alisema, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2008 kazi ya uchunguzi wa urithi wa utamaduni usioonekana itakamilishwa na kitabu cha "Aina za Urithi wa Utamaduni Usioonekana Mkoani Ningxia" kitachapishwa, na hadi mwaka 2020 aina zote za urithi wa utamaduni usioonekana zitakuwa zimepata hifadhi nzuri.
|