Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-11-06 10:08:17    
Mabomba ya kusafirisha gesi ya asili kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mji wa Beijing

cri

Mwezi Septemba mwaka 1997, gesi ya asili inayochimbwa mkoani Shaanxi ilianza kusafirishwa kuja mjini Beijing kwa bomba lenye urefu wa karibu kilomita elfu 1. Hadi sasa bomba hilo limetumika kwa miaka 10, na kila siku linasafirisha gesi ya asili kuja mijini Beijing na Tianjin.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 910 lilianza kujengwa mwezi Mei mwaka 1996. Linapita kwenye mikoa ya Shaanxi, Shanxi, Hebei, na miji ya Beijing na Tianjin, hilo ni bomba refu zaidi ambalo linapita kwenye sehemu zenye sura mbalimbali za kijiografia na linatumia mashine nyingi zaidi za kisasa. Hilo ni bomba la kwanza linalosafirisha gesi ya asili kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mjini Beijing. Kutokana na maendeleo ya uchumi ya mji wa Beijing, mwaka 2005 bomba la pili la kusafirisha gesi ya asili kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mjini Beijing lenye urefu wa kilomita 935 lilianza kutumika. Katika miaka kumi iliyopita, kwa ujumla mabomba hayo mawili yamesafirisha gesi ya asili mita za ujazo bilioni 17.5 za gesi ya asili, ambazo ni asilimia 95 ya gesi ya asili iliyotumika mjini Beijing.

Kutumia gesi wakati wa kupika chakula au kuchemsha maji ni jambo la kawaida kwa wakazi wa Beijing. Lakini wafanyakazi wamefanya kazi kubwa kusafirisha gesi ya asili kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mjini Beijing na kuhakikisha usalama wa kutumia gesi hiyo.

Kituo cha kutengeneza mabomba ya kusafirisha gesi ya asili cha tawi la Shirika la Mafuta na Gesi ya asili la China mkoani Shanxi kinashughulika na kazi ya kuhakikisha usalama wa mabomba hayo. Mkuu wa kituo hicho Bw. Wu Zhonglin alisema kikundi chake kinafanya kazi ya ukarabati wa mabomba ya kusafirisha gesi ya asili yanapoharibika, alisema,

"Hayo ni mabomba ya kipekee yanayohusiana na maisha ya wakazi na uchumi wa miji ya Beijing na Tianjin, hivyo tunakabiliwa na shinikizo kubwa. Tangu mabomba hayo mawili yaanze kutumika, haijatokea ajali kubwa. Tunajiita "kikundi cha kuzima moto", kwani tatizo likitokea kwenye mabomba hayo, tunatakiwa kufika huko mara moja na kutengeneza sehemu iliyoharibika, na tunatakiwa kufanya kazi haraka. Kama tatizo ni dogo, tunaweza kuhakikisha kuwa mabomba yanaanza kufanya kazi tena ndani ya saa 20."

Kutokana na hali ya utatanishi wa kijiografia kwenye sehemu ambako mabomba hayo yanapita, maafa ya kimaubile yakiwemo maporomoko ya udongo yanatokea mara kwa mara, tena barabara na madaraja yanajengwa karibu na mabomba hayo, hivyo mabomba hayo yanakabiliwa na matatizo mbalimbali. Ili kuhakikisha mabomba hayo yatafanya kazi kwa usalama, Shirika la Mafuta na Gesi ya asili la China limetumia teknolojia ya kisasa ya usimamizi ili kuhakikisha usalama wa mabomba hayo. Hali ya mabomba hayo inaweza kuoneshwa kwenye kompyuta za usimamizi mjini Beijing.

Mkurugenzi wa kituo cha tathimini ya usalama wa mabomba na maendeleo ya sayansi ya kampuni ya gesi ya asili ya Huayou ya Beijing ya Shirika la Mafuta na Gesi ya asili la China Bw. Dong Shaohua alieleza kuwa, wafanyakazi wanaweza kusimamia mashine kubwa kutoka mbali kupitia mfumo wa usalama. alisema,

"Tumeweka vyombo vya utambuzi kwenye mashine za kuleta mgandamizo, kutokana na vyombo hivyo tunaweza kutambua kama mashine hizo zinakabiliwa na matatizo na zina matatizo gani kwa kupitia mfumo wa kujigundua dosari. Na tunaweza kufanya marekebisho toka mjini Bejing."

Ghala ya malimbikizo ya gesi ya asili iliyoko kwenye mtaa wa Dagang mjini Tianjin pia ina mfumo wa kisasa wa tathimini ya usalama. Gesi ya asili yenye mita za ujazo bilioni 3 inaweza kutosheleza matumizi ya gesi ya asili mjini Beijing katika majira ya baridi kwa zaidi ya siku 15. Usalama wa ghala hilo unafanyiwa tathimini kwa kutumia teknolojia iliyoingizwa kutoka Russia. Meneja ananyesimamia akiba hiyo Bw. Wang Fengtian alieleza kuwa,

"Bado nchi yetu haina vigezo kamili vya kutathimini usalama wa akiba ya gesi ya asili, hivyo tumeanzisha utafiti kuhusu mambo hayo kwa kushirikiana na taasisi ya sayansi ya gesi ya asili ya Russia. Tunaweza kufanya tathimini kuhusu usalama wa malimbikizo ya gesi ya asili, na malimbikizo hayo yakikabiliwa na matatizo, tunaweza kuchukua hatua kutatua matatizo hayo kwa wakati."

Utoaji wa gesi ya asili kwa usalama umebadilisha miundo ya matumizi ya nishati mjini Beijing. Hivi sasa si kama tu wakazi wa Beijing wanatumia gesi ya asili ambayo haisababishi uchafuzi mkubwa, bali pia zaidi ya mabasi 4000 yanatumia nishati hiyo. Aidha, mkahawa wa kijiji cha michezo ya Olimpiki ya Beijing na mahoteli mia kadhaa yaliyosaini mikataba na kamati ya maandalizi ya michezo ya Olimpiki ya Beijing yanatumia gesi ya asili inayosafirishwa kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mji wa Beijing. Meneja mkuu wa kampuni ya Huayou Bw. Liu Lei alipozungumzia mchango utakaotolewa na mabomba hayo kwa michezo ya Olimpiki ya Beijing, alisema na furaha,

"Mabomba mawili yanayosafirisha gesi ya asili kutoka mkoa wa Shaanxi hadi mji wa Beijing yana uwezo wa kusafirisha gesi ya asili mita za ujazo bilioni 10, ambazo zinaweza kukidhi mahitaji ya mji wa Beijing wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing. Ili kuhakikisha utoaji wa gesi ya asili, pia tutalimbikiza gesi ya asili, na kukarabati mashine. Kama tatizo likitokea kwenye mabomba ya kusafirisha gesi hiyo, tutaweza kutumia akiba ya gesi. Tutahakikisha utoaji wa gesi ya asili wakati wa michezo ya Olimpiki ya Beijing kwa hatua mbalimbali."